02/07/2026
VIFAA VYA UPAKO: JE, NI MAFUNDISHO YA KIBIBLIA AU TUMEJENGA FUNDISHO JUU YA MATUKIO?
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kile kinachoitwa vifaa vya upako.
Mafuta ya upako, chumvi ya upako, sabuni ya upako, maji ya upako, vitambaa vya upako, keki ya upako, na hata desturi ya kukanyaga mafuta vimepewa nafasi kubwa katika baadhi ya huduma.
Baadhi ya waamini wamefundishwa kwamba ukipaka mafuta fulani utapona, ukioga kwa sabuni maalumu laana itaondoka, ukiweka chumvi nyumbani mapepo yatakimbia, ukinywa maji yaliyobarikiwa utapata mafanikio, au ukikanyaga mafuta milango ya kiroho itafunguka.
Ninaandika makala hii kwa heshima kubwa kwa watumishi wote wa Mungu na kwa Kanisa la Kristo. Kusudi langu si kumshambulia mtu, dhehebu au huduma yoyote. Kusudi langu ni kutualika sote turudi kwenye mamlaka ya mwisho ya imani yetu—Neno la Mungu.
Swali si k**a vitu hivi vinaweza kutumika. Swali ni:
Je, Biblia inavifundisha k**a mafundisho ya Kanisa, au tumegeuza matukio maalumu ya Biblia kuwa mafundisho ya kudumu?
Hilo ndilo swali ambalo kila Mkristo anayelipenda Neno la Mungu anapaswa kujiuliza.
Mungu anaweza kutumia vitu vya kawaida
Kabla sijajibu hoja zinazotolewa leo, ni muhimu nikiri ukweli mmoja ambao Biblia inaufundisha wazi.
Mungu anaweza kutumia kitu chochote kutenda mapenzi yake.
Katika Agano la Kale na Agano Jipya tunaona mifano mingi.
Mungu alitumia fimbo ya Musa (Kutoka 4:1–5; 14:16). Kwa fimbo hiyo bahari iligawanyika na miujiza mingi ikatokea. Lakini nguvu hazikuwa ndani ya fimbo; zilikuwa kwa Mungu. Baada ya Musa kufa, hakuna mahali popote ambapo Israeli waliambiwa waihifadhi fimbo hiyo ili iendelee kufanya miujiza.
Mungu alimtumia Elisha kuweka chumvi kwenye chemchemi ya maji (2 Wafalme 2:19–22). Lakini Elisha alisema kwanza:
"BWANA asema hivi: Nimeyaponya maji haya."
Ni Mungu aliyekuwa ameponya maji, si chumvi.
Yesu alitumia tope kumponya kipofu (Yohana 9:6–7). Je, Yesu aliwaagiza wanafunzi wake watumie tope kila wanapoombea wagonjwa? Hapana.
Mungu alifanya miujiza kupitia vitambaa vilivyotoka kwa Paulo (Matendo 19:11–12). Lakini andiko linaanza kwa kusema:
"Mungu alikuwa akifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo."
Chanzo cha nguvu kilikuwa Mungu.
Hata kivuli cha Petro kinatajwa (Matendo 5:15–16), lakini Biblia haisemi kivuli kilikuwa na nguvu zake; kinaonyesha tu jinsi Mungu alivyokuwa akitenda kazi kupitia mtume wake.
Kutokana na mifano hii tunajifunza kanuni moja muhimu:
Mungu anaweza kutumia kitu chochote, lakini si kila alichotumia kinakuwa fundisho la Kanisa.
Tofauti kati ya tukio na fundisho
Hapa ndipo makosa mengi yanapoanzia.
Katika kutafsiri Biblia kuna kanuni muhimu sana:
Si kila tukio ni fundisho, na si kila mfano ni amri.
Mungu alitumia fimbo, lakini hakufundisha matumizi ya fimbo.
Alitumia chumvi, lakini hakufundisha matumizi ya chumvi.
Yesu alitumia tope, lakini hakufundisha matumizi ya tope.
Paulo alitumia vitambaa, lakini hakufundisha matumizi ya vitambaa.
Kwa hiyo, tukio linaweza kuonyesha jinsi Mungu alivyotenda, lakini haliwezi peke yake kujenga mafundisho ya kudumu kwa Kanisa.
Hoja ya kwanza: "Lakini Yesu aliwatuma wanafunzi wapake mafuta"Hii ni hoja yenye uzito, na haipaswi kupuuzwa.
Marko 6:13 inasema:
"Nao wakatoa pepo wengi, wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya."
Ninakubaliana kabisa kwamba wanafunzi walitumia mafuta.
Lakini je, andiko hili linafundisha kuwa mafuta ndiyo chanzo cha uponyaji?
Hapana.
Andiko halisemi nguvu zilikuwa ndani ya mafuta.
Zaidi ya hapo, baada ya kufufuka Yesu alipotoa Agizo Kuu alisema:
"Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya." (Marko 16:18).
Ni jambo la kufikirisha kwamba Yesu hakusema:
"Watawapaka mafuta."
Alisema:
"Wataweka mikono."
Hii inaonyesha kuwa nguvu hazikuwa kwenye mafuta bali katika mamlaka ya Kristo na imani.
Hoja ya pili: "Lakini Yakobo anaagiza kupaka mafuta"
Yakobo 5:14 inasema:
"Je! Mtu wa kwenu amepatwa na ugonjwa? Na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee wakimpaka mafuta kwa jina la Bwana."
Ndiyo, mstari huu upo.
Lakini tusiishie mstari wa 14
Tusome pia mstari wa 15.
"Na sala ya imani itamwokoa mgonjwa..."
Yakobo hasemi:
"Mafuta yatamponya."
Anasema:
"Sala ya imani..."
Kwa hiyo mafuta hapa ni ishara ya Roho Mtkatifu na huduma ya wazee wa kanisa, lakini chanzo cha uponyaji ni Mungu anayejibu sala ya imani.
Mafuta katika Agano la kale yalitumika kupaka Wafalme, manabii, na makuhani.
Zaidi ya hayo, Yakobo hasemi mgonjwa aende akanunue mafuta yenye chapa maalumu, wala hasemi mafuta yatoke kwa mtumishi mmoja pekee.
Anaelekeza kwa wazee wa kanisa na maombi kwa jina la Bwana.
Hoja ya tatu: "Lakini vitambaa vya Paulo vilikuwa na nguvu"
Matendo 19:11–12 ni mojawapo ya maandiko yanayotajwa sana.
Lakini mstari wa 11 unasema:
"Mungu alikuwa akifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo."
Ni Mungu aliyekuwa anatenda.
Vitambaa havikuwa chanzo cha nguvu.
K**a vitambaa vingekuwa fundisho la Kanisa, kwa nini Paulo hakulifundisha jambo hilo katika nyaraka zake? Kwa nini hakuliagiza kanisa la Korintho, Efeso, Filipi au Warumi litumie vitambaa vya upako?
Jibu ni rahisi.
Lilikuwa tukio maalumu, si fundisho la kudumu.
Je, chumvi ya upako ina msingi wa Biblia?
Hoja inayotolewa ni ya Elisha katika 2 Wafalme 2:19–22.
Lakini Elisha hakusema:
"Chumvi ina nguvu."
Alisema:
"BWANA asema hivi: Nimeyaponya maji haya."
Mungu ndiye aliyefanya muujiza.
Hakuna mahali popote ambapo mitume walifundisha matumizi ya chumvi kufukuza mapepo, kuvunja laana au kuleta mafanikio.
Je, kukanyaga mafuta kuna msingi wa Biblia?
Hoja kubwa hutolewa kutoka Kumbukumbu la Torati 33:24.
"Asheri atachovya mguu wake katika mafuta."
Lakini mstari huu ni sehemu ya baraka za Musa kwa kabila la Asheri.
Haukuwa agizo la ibada.
Haukuwa fundisho kwa Kanisa.
Mafuta katika muktadha huo yanaashiria rutuba, wingi na utajiri wa nchi.
Hakuna sehemu nyingine ya Biblia inayosema:
mkanyage mafuta ili mpokee upako;
mkanyage mafuta ili mapepo yakimbie;
mkanyage mafuta ili milango ya baraka ifunguke.
Kwa hiyo ni hatari kujenga fundisho juu ya mstari mmoja bila ushahidi wa Maandiko mengine.
Je, keki ya upako, sabuni ya upako na maji ya upako vinafundishwa?
Hakuna mahali popote ambapo Yesu aliwapa wanafunzi wake keki ya upako.
Hakuna mahali ambapo mitume walitengeneza sabuni ya upako.
Hakuna mahali ambapo Kanisa la kwanza lilifundisha matumizi ya maji ya upako k**a njia ya kupokea nguvu za Roho Mtakatifu.
Biblia inafundisha kuhusu Meza ya Bwana, lakini haifundishi "keki ya upako."
Revelation is not Doctrine.( Ufunuo si fundusho)
Leo tunasikia kauli k**a:
"Mungu alinifunulia nitumie chumvi."
"Roho Mtakatifu aliniambia watu wakanyage mafuta."
"Niliona maono ya keki ya upako."
Ninaamini Mungu bado anasema na watu wake.
Lakini lazima tukumbuke kanuni hii:
Revelation is not Doctrine.
Ufunuo binafsi si fundisho la Kanisa mpaka uthibitishwe na Maandiko.
Paulo anasema:
"Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho..." (2 Timotheo 3:16–17).
Na Waberoya walisifiwa kwa sababu:
"Walilipokea lile neno kwa utayari mwingi wa moyo,
wakayachunguza Maandiko kila siku waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo." (Matendo 17:11).
Pia tunaonywa:
"Msiamini kila roho, bali zijaribuni roho..." (1 Yohana 4:1).
Na tena:
"Yajaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema." (1 Wathesalonike 5:21).
Hakuna Mkristo anayepaswa kukubali fundisho kwa sababu tu limetokana na maono, ndoto au uzoefu wa mtu. Lazima lipimwe kwa Neno la Mungu.
Hatari ya kubadili alama kuwa sanamu.
Mfano mzuri ni nyoka wa shaba (Hesabu 21:8–9).
Mungu ndiye aliyeagiza atengenezwe.
Lakini baadaye watu wakaanza kuuchomea uvumba.
Mfalme Hezekia akauvunja (2 Wafalme 18:4), kwa sababu kile ambacho Mungu aliwahi kukitumia kilikuwa kimegeuzwa kuwa sanamu.
Hili ni onyo kwetu. Tusije tukahamisha imani yetu kutoka kwa Kristo na kuiweka kwenye mafuta, chumvi, sabuni, vitambaa au kitu kingine chochote.
Hitimisho
Ndugu zangu, lengo si kupinga miujiza, wala si kupinga maombi ya kupaka mafuta k**a yanavyotajwa katika Yakobo 5:14. Lengo ni kuhakikisha kwamba hatuendi zaidi ya yale yaliyoandikwa (1 Wakorintho 4:6).
Mungu bado huponya. Mungu bado hufungua milango. Mungu bado hufanya miujiza. Lakini nguvu haziko kwenye mafuta, chumvi, sabuni, vitambaa, maji au keki.
Nguvu ziko kwa Mungu, na hutenda kazi kupitia Kristo kwa Roho Mtakatifu, kwa njia ya imani.
Tusijenge mafundisho juu ya tukio moja, mstari mmoja au ufunuo wa mtu mmoja.
Tujenge mafundisho juu ya ushuhuda kamili wa Maandiko. Kwa sababu si kila tukio ni fundisho, na si kila ufunuo ni mafundisho ya Kanisa.
Neno la Mungu ndilo kipimo chetu na mamlaka yetu ya mwisho.
John Lobulu Nengala
Mtume wa kizazi Kipya.