31/05/2026
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na maji( EWURA) imefanya ziara ya ukaguzi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba(BUWASA) kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa Mamlaka hiyo na kuona k**a imefikia vigezo na viwango vilivyowekwa na EWURA katika utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa Mazingira.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA Bw.John Sirati kwa kushirikiana na timu ya EWURA, ambapo Mhandisi Joseph Ngeleja alisema kuwa ukaguzi huo unalenga kupima ufanisi wa Mamlaka katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi, ubora wa maji, usimamizi wa miundombinu, ukusanyaji wa mapato pamoja na utatuzi wa changamoto za wateja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA aliishukuru timu ya EWURA kwa kufanya ziara hiyo muhimu, akieleza kuwa tathmini hiyo ni fursa ya kujifunza na kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu.
“Mamlaka itaendelea kushirikiana kwa karibu na EWURA katika kuhakikisha viwango vya utoaji huduma vinaendelea kuimarika. Tathmini hizi zinatusaidia kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika kuwahudumia wananchi wetu,” alisema Bw John Sirati Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA.
Aidha, kikao hicho kilihusisha majadiliano mbalimbali kuhusu namna ya kuendelea kuboresha huduma za maji safi na usafi wa Mazingira kwa wananchi wa Bukoba sambamba na kuzingatia vigezo na miongozo inayotolewa na EWURA.
Timu hii iko Mkoani Kagera kwa ziara ya siku Tatu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA UHUSIANO, BUWASA
29/05/2026
29/05/2026
Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imefanya kikao cha pamoja na k**ati ya ushauri wa huduma za Nishati na maji ya EWURA Consumer Consultative Council (EWURA CCC) kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma kwa wateja na kutatua changamoto za malalamiko yanayohusu huduma ya maji kilichofanyika ukumbi wa mikutano BUWASA.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Bi Julieth Shangali aliwashukuruku EWURA CCC kwa kuona haja ya kukutana na kujadiliana namna ya kushirikiana kuboresha huduma ya maji na kutatua changamoto za wateja.
"Kikao hiki ni muhimu sana kwani kinalenga kuboresha huduma na kuweka mikakati ya kuboresha kwani EWURA CCC nyie ndiyo mko karibu zaidi na wateja naamini kupitia kikao hiki tunaenda kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma,"aliongezea Bi Julieth Shangali,Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano BUWASA.
Katika kikao hicho,pande zote mbili zilijadiliana kwa kina namna ya kuimarisha mawasiliano kati ya Mamlaka na wateja, kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za maji na taratibu za kuwasilisha changamoto zao.
Aidha viongozi waliohudhuria walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Taasisi na wananchi katika kuhakikisha huduma za maji zinakuwa bora ,salama na za kuaminika wakati wote.Pia walieleza kuwa maoni na malalamiko ya wananchi ni sehemu muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake,EWURA CCC iliahidi kuendelea kushirikiana na BUWASA katika kutoa elimu kwa watuamiaji wa huduma za maji pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maboresho yanayolenga kuongeza kuridhika kwa wateja.
Kikao hiki kilihudhuriwa na Menejimenti ya BUWASA,Bi Anadorice Komba,Afisa Mwandamizi huduma kwa wateja EWURA CCC (M),Bw.Najim Bwanika Mwenyekiti wa k**ati ya Watumiaji wa huduma za Nishati na maji (M) ,pamoja na Bw.Lenas Katabazi Mjumbe wa Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Nishati na maji Mkoa wa Kagera.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA UHUSIANO, BUWASA
29/05/2026
23/05/2026
Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA)imeendelea kutoa elimu kwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuhusu utunzaji na ulinzi wa miundombinu ya maji.
Akiongea kwenye Mkutano wa mtaa uliofanyika mtaa wa Bulibata Kata ya Buhembe Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano BUWASA Bi Julieth Shangali aliwafahamisha wadau hawa kuwa kumekuwa na wimbi la wizi wa dira za maji na tape za maji ambao umetokea kwenye baadhi ya kata za Manispaa ya Bukoba.
"Hivyo kupitia kikao hiki tumekuja kuwatahadharisha na kuwataka kuchukua hatua za kulinda dira na miundombinu ya maji kwa ujumla kwani endapo mteja ataibiwa dira ya maji atalazimika kulipia dira mpya ili aweze kuendelea kupata huduma ya maji".
Aidha Bi Julieth aliwaasa wadau kujenga tabia ya kulipia bili ya maji pindi anapoipata kwani kwa kufanya hivyo atakuwa amechangia katika kuboresha huduma na kuifanya iwe endelevu kwani kupitia bill za maji Mamlaka inaweza kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji ikiwemo za umeme na madawa.
"Kwa upande wa vilula vilivyofungwa kutokana na madeni Ofisi inaenda kuweka utaratibu wa kuvifungua ikiwa ni pamoja na kufuatilia wadaiwa waliokuwa wanavisimamia kwa kumtumia Mwanasheria wa Mamlaka ili madeni haya yaweze kulipwa na wananchi waendelee kupata huduma hii kwani vilula hivi vilijengwa kwa lengo la kusaidia wananchi wenye kipato cha chini ili waweze kupata huduma hii kwa gharama nafuu na kwa umbali mfupi" ,aliongeza Bi Julieth Shangali.
Akiongea kwenye kikao hiki Bi Devotha Koy Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa mteja aliwaomba wadau kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uvujaji wa mabomba ikiwa ni pamoja na kulipa bill zao kwa wakati kwa kutumia namba ya malipo inayotumwa kwenye bill zao na siyo kumpatia fundi hela
"Kwa wateja wenye madeni Ofisi iko tayari kuwarudishia huduma wanaodaiwa kwa kuingia mkataba wa kulipia deni kidogo kidogo huku wakiendelea kupata huduma ya maji", aliongezea Bi Devotha Koy.
Kikao hiki kilihudhuriwa na viongozi wa mtaa wa Bulibata ,Watumishi kutoka BUWASA pamoja na wakazi wa mtaa wa Bulibata.
IMETOLEWA NA KITENGO MAWASILIANO NA UHUSIANO, BUWASA.
21/05/2026
19/05/2026
Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Bukoba, BUWASA imefanya kikao na wakazi wa mtaa wa Kagondo, Karuguru kwa ajili ya kujadiliana kuhusu wimbi la wizi wa dira za maji uliotokea hivi karibuni mtaani hapo.
Akiongea kwenye Mkutano huo Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano,BUWASA Bi Julieth Shangali alisema kuwa BUWASA imepokea kwa uzito mkubwa taarifa za wimbi la wizi wa dira za maji ambao umeingia kwenye Kata ya Kagondo na kuitikia wito wa kikao kwa ajili ya kujadiliana namna ya kutokomeza wizi huu k**a ilivyofanyika kwenye maeneo mengine.
Aidha wadau walifahamishwa kuwa BUWASA kwa kushirikiana na jeshi la Polisi inaendelea na zoezi la kubaini wezi wa dira za maji ambapo dira 2 Kati ya 12 zilizoibiwa tayari zimepatikana na zoezi linaendelea.
Vile vile wananchi wameshauriwa kujengea dira zao Ili kuzuia wizi huo .
Naye Bi Devotha Koy Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa mteja aliwatakata wananchi kulinda dira zao za maji kwani endapo zitaibiwa mteja atalazimika kulipia dira mpya ili aweze kuendelea kupata huduma.
Hata hivyo wadau kwa pamoja walikubaliana kuanza ulinzi shirikishi ambapo BUWASA iliahidi kutoa vifaa vya kusaidia kufanikisha zoezi hili ikiwemo tochi.
Kikao hiki kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bukoba ,Uongozi wa mtaa na wananchi wa Kagondo Karuguru.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA UHUSIANO, BUWASA
19/05/2026