21/04/2026
ZEEA YAKUTANA NA BALOZI WA ITALIA NCHI TANZANIA, YALENGA KUWAPATIA WAJASIRIAMALI FURSA ZA KIMATAIFA
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), ndugu Juma Burhan Mohamed, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Balozi Giuseppe Sean Coppola, kwa lengo la kutafuta na kufungua fursa za kiuchumi, zitakazowawezesha wajasiriamali wa Zanzibar kukuza biashara zao na kuongeza ushindani katika soko la ndani na kimataifa.
Mkurugenzi huyo amemueleza Balozi Coppola jinsi ZEEA inavyotekeleza majukumu yake katika kuwawezesha wajasiriamali, ikiwemo utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali, uwezeshaji wa mitaji, pamoja na kusaidia upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zao, ili kuongeza tija, kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi jumuishi.
Katika kuendana na mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa teknolojia, Mkurugenzi Juma amesisitiza kuwa ZEEA inahitaji kushirikiana na washirika wa maendeleo watakaosaidia kuwajengea uwezo wajasiriamali katika matumizi ya teknolojia za kisasa, ili kukuza uzalishaji wa bidhaa na huduma, sambamba na kuongeza ishandani katika upatikanaji wa masoko.
Naye Balozi Coppola ameeleza kuwa Serikali ya Italia inaandaa maonesho, programu na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali katika nyanja tofauti, ikiwemo kilimo, utalii na uchumi wa buluu, pamoja na sekta nyingine zenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Aidha, ameishauri ZEEA kuandaa wasilisho rasmi litakaloeleza kwa kina shughuli na mipango ya taasisi hiyo, ili kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano na namna ambavyo Serikali ya Italia na taasisi zake zinaweza kushirikiana na ZEEA katika kuwawezesha wajasiriamali kwa ufanisi zaidi.
10/04/2026
inawatakia kilala kheir katika majukumu mapya ya Ukuu wa Wilaya, mungu awatangulie kwa kila jambo
08/04/2026
MKURUGENZI MTENDAJI ZEEA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI KITUO CHA ZTBI TAWI LA PEMBA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Ndg. Juma Burhan Mohamed, amefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Kukuza na Kulea Wajasiriamali (ZTBI) Tawi la Pemba, kilichopo Michakaeni, Wilaya ya Chake Chake. Katika ziara hiyo, Ndg. Juma alisema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutawapa fursa wajasiriamali wa Pemba kupata mafunzo na ushauri wa kitaalamu ili kuimarisha biashara zao.
Mratibu wa ZEEA, Ndg. Haji Moh'd Haji, aliongeza kuwa kituo hicho kitawasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora na zinazotakiwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Alisema kuwa ZEEA inaendelea kufanya kazi kwa bidii kuwasaidia wajasiriamali wa Pemba kufikia malengo yao.
28/01/2026
Mratibu Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Kisiwani Pemba Haji Mohd Haji, amesema ufugaji wa nyuki kisasa unaenda kumuhifadhi na kumlinda Nyuki, ili asiweze kupotea kutokana na athari za mazingira hivi sasa.
Amesema nyuki ni Viumbe muhimu katika maisha ya mwanaadamu, licha ya changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa wafugaji wa nyuki.
Ameyaeleza hayo wakati akifungu mafunzo ya ufugaji wa nyuki Kisiwani Pemba, kufuatia uhitaji wa wajasiriamali baada ya tathmini ya ufuatiliaji wa ufugaji wa nyuki Pemba.
Amesema ZEEA imeamua kuazishwa shamba darasa la ufugaji wa nyuki Pamoja na upandaji wa mauwa ya sanflawa, ili kuwasaidia nyuki kupata chakula karibu.
22/08/2025
WAKALA wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar ZEEA Ofisi ya Pemba kwa kushirikiana na SEBEP imeweza kutoa mafunzo ya siku 30 kwa vijana 50 kutoka kisiwa cha Pemba, juu ya masuala ya upambaji, mafunzo hayo yakiwa na lengo la kuinua vipaji vya vijana na kuongeza ajira kwao, mafunzo hayo yamefunguliwa na afisa mdhamini Ofisi ya Rais Ikuluu Shuwekha Abdalla Omar
14/08/2025
WAKALA wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Ofisi ya Pemba, imetoa mafunzo kwa Wajasirimali juu ya umuhimu wa kujirasimisha na mafunzo ya tenda serikalini, ambayo yatawasaidia kuomba tenda mbali mbali zinazotangazwa na Serikali kupitia mitandaoni, mafunzo haya ya siku moja yamefanyika katika Ofisi za ZEEA Gombani