Bi. Jasmine Hussein, mkazi wa Arusha na mama wa mtoto wa miaka 12 aliyefanyiwa upasuaji wa macho katika Kambi ya Makonda, ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa bila malipo, hadi walipo.
Kwa furaha, Bi. Jasmine amewashukuru wataalamu wa upasuaji kwa huduma hiyo iliyompa mtoto wake faraja na matumaini mapya. Anaamini kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mtoto wake ataweza kuona vizuri zaidi na kuendelea na maisha yake kwa furaha na kujiamini.
Hospitali ya Taifa Muhimbili
National and tertiary specialized hospital proving specialized and super specialized service
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha wameendelea kunufaika na huduma za matibabu zinazotolewa kupitia Kambi ya Afya ya Paul Makonda, ambapo hadi sasa zaidi ya wananchi 17,600 wamepatiwa huduma za uchunguzi, matibabu na ushauri wa afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo amesema hospitali imeongeza madaktari bingwa na bingwa bobezi katika kambi ya matibabu inayoendelea Arusha baada ya idadi ya wananchi wanaohitaji huduma kuzidi matarajio.
17/07/2026
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imelazimika kuongeza idadi ya wataalam wa huduma za macho katika Kambi ya Matibabu ya Makonda inayoendelea katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kutokana na ongezeko kubwa la wananchi wanaohitaji huduma hizo.
Akizungumza alipotembelea kambi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, amesema uamuzi huo umefikiwa kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi, huku zaidi ya watu 10,000 wakiwa tayari wamepata huduma mbalimbali za afya tangu kambi hiyo ilipoanza Julai 13, 2026.
Dkt. Kimambo amesema Muhimbili itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kibingwa. Amewahimiza wananchi kuendelea kutumia huduma zinazotolewa bila malipo na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili magonjwa yagundulike na kutibiwa mapema.
Kambi ya Matibabu ya Makonda inatoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo kwa wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani kupitia wataalamu kutoka hospitali mbalimbali nchini. Kambi hiyo inalenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi pamoja na kusaidia kubaini na kutibu changamoto mbalimbali za kiafya na inatahitimishwa Julai 19, 2026.
16/07/2026
Wananchi wa Jiji la Arusha wanaendelea kunufaika na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia kambi maalumu ya matibabu inayoendelea katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid. Huduma za upasuaji zinazotolewa ndani ya Gari Maalumu la Upasuaji zimeendelea kuwafikia wananchi wengi, huku idadi ya waliopata huduma hizo ikikaribia kufikia 100 tangu kuanza kwa kambi hiyo.
Miongoni mwa wanufaika hao ni Bw. Babuu Pasikali, aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo. Akiwa na furaha baada ya matibabu, amesema hakuwahi kufikiria kuwa angeweza kupata huduma hiyo kutokana na changamoto ya kifedha iliyokuwa ikimzuia kumudu gharama za upasuaji. Ameeleza kuwa kupitia kambi hiyo iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mh. Paul Makonda, ameweza kurejeshewa matumaini na sasa anaishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuleta Gari Maalumu la Upasuaji pamoja na wataalamu waliowezesha huduma hiyo kuwafikia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amesema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi ili kuwapa fursa ya kupata matibabu ya kiwango cha juu bila vikwazo vya gharama. Amesema mbali na huduma za matibabu, wananchi pia wanapata ushauri wa kitaalamu na elimu ya afya inayowasaidia kutambua, kuzuia na kudhibiti magonjwa mbalimbali.
Dkt. Kimambo ametoa wito kwa wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani kuendelea kujitokeza kwa wingi kabla ya kambi hiyo kuhitimishwa, ili waweze kufanyiwa uchunguzi, kupata matibabu stahiki na kunufaika na huduma zote zinazotolewa bila malipo na wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Amesisitiza kuwa huduma hizo ni sehemu ya jitihada za hospitali kuhakikisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi zinawafikia Watanzania wengi zaidi popote walipo.
16/07/2026
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Jullieth Magandi, amefungua mafunzo ya Usimamizi wa Fedha na Uwajibikaji (Financial Management and Stewardship Workshop) leo, Julai 9, katika Hoteli ya Golden Tulip, yakilenga kuimarisha uelewa wa viongozi wa ngazi mbalimbali hospitalini hapo kuhusu usimamizi bora wa fedha na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja, Dkt. Magandi amesema kuwa usimamizi wa fedha na uwajibikaji ni muhimu kwa kila kiongozi, na kuongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kufanya maamuzi sahihi yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma.
“Usimamizi wa fedha si jukumu la wataalamu wa fedha pekee. Kila kiongozi anayesimamia rasilimali ana wajibu wa kuhakikisha fedha zinatumika kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji. Nawasihi mtumie mafunzo haya k**a fursa ya kuongeza maarifa, kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo utakaowawezesha kutekeleza majukumu yenu kwa weledi zaidi,” amesema Dkt. Magandi.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo, pamoja na wasimamizi wa uendeshaji wa vitengo mbalimbali (Business Managers), ambapo wanapata uelewa kuhusu misingi ya usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya rasilimali na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu.
16/07/2026
Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji na Upandikizaji Figo kwa njia ya matundu madogo, Dkt. Emanuel Minja, ambaye ni Mtanzania anayefanya kazi nchini Marekani, amewahimiza madaktari wa Kitanzania waliopo nje (diaspora} kujenga utamaduni wa kuja nchini kushirikiana na wataalamu wazawa katika kubadilishana ujuzi na teknolojia za kisasa ili kuimarisha huduma za kibingwa na bingwa bobezi.
Dkt. Minja ametoa wito huo baada ya kuongoza jopo la madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanikisha upasuaji wa kisasa wa upandikizaji figo kwa njia ya matundu madogo kwa wagonjwa watatu.Ambapo hii ni mara ya pili kwa dkt minja kushiriki aina hii ya upasuaji
Amesema ushirikiano huo utaongeza uwezo wa wataalamu wa ndani na kuboresha huduma za upandikizaji figo nchini, huku matumizi ya upasuaji wa matundu madogo yakichangia kupunguza maumivu, madhara ya upasuaji, muda wa kulazwa hospitalini na kuwawezesha wagonjwa pamoja na wachangiaji wa figo kurejea haraka katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza baada ya kukutana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi, Dkt. Minja amesema wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya madaktari wa Kitanzania waliopo nje ya nchi na wataalamu wa Muhimbili kupitia utoaji wa huduma, mafunzo na ubadilishanaji wa uzoefu ili kuendelea kuinua ubora wa huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Dkt. Magandi amepongeza mchango wa Dkt. Minja kwa kuendelea kurejea nchini kushiriki katika utoaji wa huduma za kibingwa na kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili.
16/07/2026
Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wametakiwa kutumia rasilimali za taasisi kwa ufanisi na kimkakati ili kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wagonjwa na kuongeza thamani ya taasisi.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya Usimamizi wa Fedha na Uwajibikaji (Financial Management and Stewardship Workshop), mkufunzi katika warsha hiyo Prof. Goodluck Urassa amesema kuwa matumizi bora ya rasilimali ni wajibu wa kila mtumishi na yana mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya taasisi.
“Kila mtumishi anapaswa kutambua umuhimu wa nafasi yake, uwezo alionao na namna anavyoweza kuchangia katika matumizi sahihi ya rasilimali. Tunapaswa kupanga bajeti kwa ufanisi na kuhakikisha kila shilingi inayotumika inaleta thamani kubwa zaidi kwa wagonjwa na taasisi kwa ujumla,” amesema Prof. Urassa.
Ameongeza kuwa usimamizi wa rasilimali haupaswi kuachwa kwa wataalamu wa fedha pekee, bali ni jukumu la kila kiongozi na mtumishi anayehusika katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kusisitiza kuwa utamaduni wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha na rasilimali utasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji na kuboresha huduma zinazotolewa.
Mafunzo hayo ya siku moja yamewakutanisha wakurugenzi, wakuu wa idara na vitengo, pamoja na wasimamizi wa uendeshaji wa vitengo mbalimbali (Business Managers) na yamefanyika katika Hoteli ya Golden Tulip yakiwa na lengo la kuwawezesha viongozi hao kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa fedha, upangaji wa bajeti, matumizi bora ya rasilimali na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
16/07/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amewasili katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kujionea maendeleo ya Kambi Maalumu ya Matibabu inayoendelea kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi bila malipo kwa wananchi.
Ziara hiyo inalenga kufuatilia kwa karibu utoaji wa huduma, kuzungumza na wataalamu wa afya pamoja na wagonjwa wanaonufaika na huduma hizo, na kuendelea kuimarisha dhamira ya Muhimbili ya kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.
“Nilikuwa na hofu kwamba baada ya kufanyiwa upasuaji nisingeweza kuendelea na shughuli zangu za kawaida, lakini imekuwa tofauti, nimepata huduma ya upasuaji mdogo ndani ya viwanja vya Sabasaba na sasa narejea nyumbani salama bila changamoto.”
Christopher Andrew, mnufaika wa Huduma za Upasuaji Sabasaba
Click here to claim your Sponsored Listing.
Location
Category
Website
Address
Dar Es Salaam
