06/05/2026
𝐌𝐊𝐀𝐓𝐀𝐁𝐀 𝐖𝐀 𝐔𝐌𝐀𝐋𝐈𝐙𝐈𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐉𝐄𝐍𝐆𝐎 𝐋𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐏𝐀𝐒𝐈 𝐘𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐆𝐀 𝐖𝐀𝐒𝐀𝐈𝐍𝐈𝐖𝐀
Tanga- Mei 6, 2026
Mkataba wa umaliziaji wa awamu ya kwanza ya jujenzi wa jengo la Kampasi ya Tanga umesainiwa leo jijini Tanga, kati ya mkandarasi M/s Intergo Company Limited na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa gharama ya TZS 3.778 bilioni.
Mkataba umesainiwa kwa niaba ya TPSC na Mkurugenzi wa Kampasi ya Tanga, Bi. Zawadi Rashidi, na kwa niaba ya mkandarasi na Mkurugenzi wa Intergo Company Limited, Bw. Gulam Abdul. Kwa upande wa mshauri elekezi, M/s Wakala wa Majengo (TBA), mkataba ulisainiwa na Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Tanga, Bw. Justo Lyatuu.
Utiaji saini umefanyika mbele ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba, Dkt. Ernest Mabonesho amesema kuwa ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha mkataba unatekelezwa kikamilifu na kwa ubora.
"Mkandarasi anatakiwa kuzingatia ubora wa kazi k**a ilivyoainishwa kwenye mkataba na kuhakikisha kukamilisha kazi ndani ya wakati uliokubaliwa" amesisitiza Dkt. Mabonesho
Utekelezaji wa mkataba unatarajiwa kuchukua mwaka mmoja (siku 365) na ukamilishaji wake unatarajiwa kufanyika kwa wakati ili jengo lianze kutumika.
Mradi unalenga kukamilisha jengo lenye madarasa 26 zitakazohudumia zaidi ya wanafunzi 2,500 kwa awamu moja, ofisi 24 za watumishi, kumbi mbili za mikutano na vyoo vya kisasa 18.
05/05/2026
𝙎𝙝𝙪𝙡𝙚 𝙮𝙖 𝙎𝙚𝙧𝙞𝙠𝙖𝙡𝙞 𝙆𝙚𝙣𝙮𝙖 (𝐊𝐒𝐆) 𝙒𝙖𝙩𝙚𝙢𝙗𝙚𝙡𝙚𝙖 𝐓𝐏𝐒𝐂
Ujumbe kutoka Shule ya Serikali Kenya (KSG), ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Prof. Nura Mohamed, umetembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) leo, Mei 5, 2026, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuanza kwa utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano uliosainiwa Ikulu, Mei 4, 2026, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto.
Katika kikao cha pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, chini ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, wamejadiliana kwa kina kuhusu mikakati ya kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo, huku lengo likiwa ni kuboresha utendaji wa utumishi wa umma kwa kuwajengea uwezo watumishi na Tafiti Tumizi.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho amesems kuwa, ushirikiano kati KSG na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) unalenga kuleta maendeleo makubwa na ufanisi zaidi katika sekta ya utumishi wa umma, kwa kujenga uwezo wa watumishi kupitia mafunzo na tafiti.
Aidha, alisisitiza kuwa, kutokana na uzoefu wa zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa KSG, ni fursa adhimu kwa TPSC kujifunza na kupata uzoefu wa kuboresha utumishi wa umma nchini Tanzania, ili kujenga utumishi wa umma imara.
Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa, mashirikiano pia yanalenga kujenga utumishi wa umma wenye tija, wenye kuzingatia matokeo, na kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wa Tanzania, Kenya, na jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kwa upande wake, Prof. Nura Mohamed alieleza kuwa, utekelezaji wa mkataba huo utaleta maendeleo makubwa kwa pande zote mbili, kwa kuimarisha mafunzo yanayozingatia ubora na haki za wananchi.
Prof. Mohamed amesisitiza kuwa, ushirikiano huo utahusisha pia kufanya tafiti za pamoja kuhusu kuboresha sera na huduma zinazohudumia jamii, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, ambazo ni haki yao ya msingi.
Ziara hiyo pia iliwapa nafasi ujumbe kutoka KSG kutembelea Makao Makuu ya Chuo, Kampasi ya Dar es Salaam na Kituo cha Mafunzo kwa njia ya Mtandao.
04/05/2026
𝗛𝗔𝗧𝗜 𝗬𝗔 𝗠𝗔𝗞𝗨𝗕𝗔𝗟𝗜𝗔𝗡𝗢 𝗬𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔𝗝𝗘𝗡𝗚𝗘𝗔 𝗨𝗪𝗘𝗭𝗢 𝗪𝗔𝗧𝗨𝗠𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗠𝗠𝗔 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗡𝗔 𝗞𝗘𝗡𝗬𝗔 𝗬𝗔𝗦𝗔𝗜𝗡𝗜𝗪𝗔
Dar es Salaam - Mei 4,2026
Hati ya makubaliano ya mashirikiano ya kuwajengea uwezo watumishi wa umma wa Tanzania na Kenya imesainiwa kati ya Dkt. Ernest Francis Mabonesho, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, na Prof. Nura Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa Shule ya Serikali Kenya (Kenya School of Government), mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto.
Hafla hiyo ilifanyika katika Ikulu, Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 4 Mei 2026.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya utumishi wa umma kwa kuimarisha mafunzo na ufanisi wa watumishi wa umma pamoja na kupanua ushirikiano wa kiutendaji kati ya nchi mbili.
02/05/2026
𝗧𝗣𝗦𝗖 𝗠𝘁𝘄𝗮𝗿𝗮 𝗞𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗠𝗮𝗮𝗱𝗵𝗶𝗺𝗶𝘀𝗵𝗼 𝘆𝗮 𝗦𝗶𝗸𝘂𝗸𝘂𝘂 𝘆𝗮 𝗪𝗮𝗳𝗮𝗻𝘆𝗮𝗸𝗮𝘇𝗶 𝗠𝗲𝗶 𝗠𝗼𝘀𝗶
Mtwara, Mei 1, 2026
Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara wameungana na wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali katika kuadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.
Sherehe za Maadhimisho zimefanyika kimkoa katika viwanja vya Nangwanda, Manispaa Mtwara, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa.
Katika maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Donald Msengi.
Sherehe hizo zilimehudhuriwa na wafanyakazi kutoka taasisi za sekta ya umma na binafsi.
01/05/2026
TPSC DAR ES SALAAM WASHEREHEKEA MEI MOSI 2026
Leo, watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Dar es Salaam na Makao Makuu wameungana na wafanyakazi wengine kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) viwanja vya Mnazi Mmoja. Kauli mbiu ya mwaka huu: “Kazi zenye Staha ni Nguzo ya Kwanza kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Albert Chalamila, amesisitiza wafanyakazi waendelee kufanya kazi kwa uaminifu na bidii kwa sababu wao ndio sura ya serikali. Amewakumbusha kuwa mfanyakazi mmoja anaweza kufanya serikali ipendwe au ichukiwe, hivyo kila mmoja wetu awajibike na aonyeshe uaminifu kazini.
Baada ya maadhimisho, hafla iliendelea Ukumbi wa Kilimanjaro ambapo wafanyakazi hodari walitunukiwa zawadi na Mkurugenzi wa Kampasi Bw. M***a Lugembe kwa niaba ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu.
Amesisitiza umuhimu wa kushik**ana, kufuata sheria na kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kufanikisha malengo ya chuo na taifa. Pia, menejimenti imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano na motisha kwa watumishi wote.
30/04/2026
Tunawapongeza kwa kuchaguliwa kuwa watumishi Hodari kwa 2026. Hongereni sana.
30/04/2026
𝐌𝐀𝐅𝐔𝐍𝐙𝐎 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐁𝐀𝐃𝐈𝐋𝐈𝐊𝐎 𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐃𝐈𝐉𝐈𝐓𝐈 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐔𝐒𝐈𝐌𝐀𝐌𝐈𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐑𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐌𝐀𝐋𝐈 𝐖𝐀𝐓𝐔 𝐍𝐀 𝐔𝐓𝐀𝐖𝐀𝐋𝐀 𝐘𝐀𝐌𝐀𝐋𝐈𝐙𝐈𝐊𝐀 𝐀𝐅𝐑𝐈𝐊𝐀 𝐘𝐀 𝐊𝐔𝐒𝐈𝐍𝐈
Pretoria, Afrika Kusini
Mafunzo ya wiki mbili kuhusu Mabadiliko ya Kidigitali katika Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu (Digital Transformation in Administration and Human Resource Training) kwa viongozi na maafisa waandamizi yamemaliza nchini Afrika Kusini tarehe 28 April, 2026 jijini Pretoria.
Mafunzo haya yaliyowezeshwa na wabobezi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Kidijiti nchini Afrika Kusini yaliandaliwa na kusimamiwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuanzia tarehe 19 hadi 28 Aprili 2026, yakilenga kuwajengea washiriki na uelewa wa kina kuhusu uongozi wa kimkakati, ubunifu wa kidijiti katika Usimamizi wa Rasilimali Watun a Utawala.
Katika mafunzo hayo, Washiriki walipata nafasi ya kujifunza mbinu bora za kisasa za uongozi na usimamizi wa rasilimali watu, pamoja na kubadilishana uzoefu na maarifa kutoka kwa wataalamu wa sekta mbalimbali za umma na binafsi nchini Afrika Kusini.
K**a sehemu ya Mafunzo, washiriki walipata fursa ya kutembelea mbali mbali ya hihistoria yakijumuisha Nyumba ya Makumbusho ya Mandela (Mandela House Museum Orlando) na Makumbusho ya Ubaguzi wa Rangi (Apartheid Museum) la Soweto.
Chuo cha Utumishi wa Umma kinatoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na wataalamu wa nje ili kuwapa washiriki maarifa mapya na kubadilishana uzoefu na wataalamu ili kuboresha Utumishi wa Umma Nchini.
29/04/2026
Dodoma - Aprili 29,2026
Maafisa wa Serikali ya Somalia waliopo nchini kwa ziara ya Mafunzo inayoratibiwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, wametembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma kwa mwaliko wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete.
Katika ziara hiyo, maafisa hao walipata nafasi ya kujifunza jinsi Bunge linavyofanya kazi na kuchukua uzoefu wa utendaji wa mfumo wa Tanzania.
Ujumbe huo uliongozwa na mwenyeji wao, Kaimu Katibu Mkuu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Nchi wa Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho.