22/06/2026
MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIKOPO YA 10% YAANZA DODOMA, RC SENYAMULE ASISITIZA UREJESHAJI NA TIJA
Na Mwandishi Wetu ,
DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, tarehe 22 Juni 2026 amefungua rasmi mafunzo ya usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalumu yanayofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Senyamule alisisitiza umuhimu wa usimamizi bora wa mikopo hiyo ili kuongeza tija kwa walengwa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Alisema mafunzo hayo yanakuja wakati Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuimarisha utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo maafisa wa Halmashauri katika tathmini ya wakopaji, usimamizi wa mikopo, mikakati ya urejeshaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali. Pia aliwataka viongozi na watendaji kuzingatia uwazi, haki na nidhamu katika usimamizi wa mikopo hiyo, huku akiwahimiza wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati ili mfuko huo uwe endelevu.
“Mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo maafisa wa Halmashauri wanaohusika na usimamizi wa mikopo hiyo katika maeneo ya tathmini ya uwezo wa wakopaji, usimamizi wa hatari za mikopo, mikakati ya urejeshaji wa mikopo pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali” - Amesema Senyamule.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliipongeza CBE kwa mafanikio yake ya kitaaluma, ikiwemo kushika nafasi ya 10 miongoni mwa vyuo vya elimu ya juu Nchini, na kuitaka kuendelea kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10.
Kwa upande wake, Mkuu wa CBE Kampasi ya Dodoma, Prof. Edda Tandi Lwoga, alisema chuo hicho kinaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali bila ada kwa wanawake, vijana na wajasiriamali wadogo, ambapo katika kipindi cha miaka mitano, jumla ya wajasiriamali 4,500 wamepatiwa mafunzo, pamoja na wahudumu wa mabasi 2,418 na mawakala wa mali zisizohamishika 45.
Prof. Lwoga pia aliwapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri za Lindi, Babati na Karatu kwa kutenga bajeti na kuwawezesha Maafisa wao kushiriki mafunzo hayo, akiwahimiza kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu.
Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026 yakiwashirikisha maafisa kutoka Halmashauri mbalimbali, ikiwemo Babati na Karatu.
13/06/2026
KERO YAKO WAJIBU WANGU
TABASAM NA SAMIA
11/06/2026
GHALA LA FORODHA LA CIWAYE KUFUNGUA FURSA MPYA SEKTA YA USAFIRISHAJI DODOMA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma RS
Wafanyabiashara, wasafirishaji na wadau wa sekta ya ugavi wametakiwa kutumia fursa ya Ghala la Forodha la 'Ciwaye Trading Company Limited' lililozinduliwa katika eneo la Chinangali II, Chamwino mkoani Dodoma, ili kuongeza ufanisi wa biashara na kupunguza gharama za usafirishaji.
Akizindua ghala hilo Juni 10, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, alisema uwekezaji huo utaongeza tija katika shughuli za usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Wafanyabiashara, wasafirishaji na wadau wa sekta ya Ugavi, tutumie kwa ukamilifu fursa zinazotolewa na Ghala hili kuongeza tija na kupunguza gharama za biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa, tumekuwa tukiongea na wenzetu wa usafirishaji kuhakikisha tunapunguza gharama za usafirishaji kwa kutumia hatua tunazoweza kuzichukua ili kuhakikisha shughuli mnazofanya zinakuwa na tija”. Mhe. Dkt. Nchemba
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alisema ghala hilo litaimarisha shughuli za uhifadhi, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa, hatua itakayoongeza mchango wa Mkoa wa Dodoma katika biashara ya ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bi. Happy N. John, alisema Ciwaye Trading Company Limited itaendesha ghala hilo kwa kuzingatia sheria na kanuni za forodha, kulinda usalama wa mizigo, kuchangia mapato ya Serikali na kutoa ajira kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Wahabi Matengo alisema maghala ya forodha husaidia kurahisisha biashara kwa kuahirisha ulipaji wa kodi kwa bidhaa zilizohifadhiwa, kuongeza mtiririko wa fedha na kuboresha upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.
Mradi wa Ghala la Forodha la Ciwaye ulianza Januari 2025 na kukamilika Aprili 2026 kwa gharama ya shilingi bilioni 300 chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu, Bw. Daniel Robina Ligoha Chiwaye. Mradi huo unalenga kuboresha huduma za uhifadhi wa mizigo na forodha, kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa ugavi Nchini.
10/06/2026
WANANCHI DODOMA WAHAMASISHWA KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma RS
Mratibu wa Damu Salama Mkoa wa Dodoma, Bi. Jane Kiango, ameongoza kampeni ya uhamasishaji na uchangiaji damu kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa damu katika kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa huduma hiyo.
Kampeni hiyo imefanyika leo, Juni 11, 2026, katika viwanja vya Stendi ya Daladala Sabasaba jijini Dodoma, ambapo wananchi walipata elimu na hamasa ya kujitokeza kuchangia damu kwa hiari.
Akizungumza katika tukio hilo, Bi. Kiango alisema kuwa kila tone la damu linaweza kuwa tumaini la maisha kwa mgonjwa anayehitaji huduma ya dharura.
"Damu yako inaweza kuwa sababu ya tabasamu la mtu mwingine. Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hili muhimu kwa afya ya jamii yetu," alisema.
Alieleza kuwa kampeni hiyo inaendelea kuanzia Juni 1 hadi 14, 2026 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.
Aidha, Bi Kiango amewahamasisha Wananchi kushiriki uchangiaji damu kwa hiari, akibainisha kuwa damu husaidia kuokoa maisha ya wagonjwa hospitalini, wakiwemo wajawazito, watoto na majeruhi wa ajali.
Kampeni hiyo inaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Tone Moja la Ubinadamu, Changia Damu, Okoa Maisha."
# KazinaUtuTunasongaMbele