Wizara ya Fedha

Website Contact the organization

Wizara ya Fedha Ukurasa Rasmi wa Wizara ya Fedha Tanzania.

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kujenga mfumo wa kodi wa haki, unaotabirika kuwezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji ...
21/10/2026

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kujenga mfumo wa kodi wa haki, unaotabirika kuwezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini, ili kufikia malengo ya Dira 2050 ya kujenga uchumi wa Dola za Marekani Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu, na ushauri wa kibiashara ya Ernst &Young-Tanzania, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha.

Mhe. Munde alisema kuwa kufikiwa kwa malengo ya Dira 2050 kunategemea juhudi za Serikali na ushirikiano wa karibu na sekta binafsi na kampuni za huduma za kitaalamu k**a EY Tanzania.

"Ili kufikia uchumi wa Dola za Marekani Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, tunahitaji uwekezaji wenye tija kutoka sekta binafsi, taasisi imara, na mfumo wa kodi unaochochea ushindani na ukuaji wa biashara ambapo Serikali imeazimia kuweka mazingira rafiki yatakayomwezesha mlipakodi kutimiza wajibu wake kwa hiari," alisema Mhe. Munde.

Mhe. Munde alifafanua kuwa ili kufikia malengo hayo Serikali itaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mapitio ya Mfumo wa Kodi, ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA), pamoja na kutenga asilimia 5 ya rasilimali za Serikali za Mitaa kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya masoko.

Aidha, alisema mifumo ya Tehama na uchanganuzi wa takwimu itaendeelea kuimarishwa ili kupunguza ulazima wa walipakodi kukutana ana kwa ana na maofisa wa kodi, pamoja na kufanya ukaguzi wa pamoja kati ya taasisi za udhibiti.

‘‘Serikali pia itaendelea Kutoa unafuu wa kodi wa mwaka mmoja kwa biashara ndogo mpya zilizoanzishwa, ili kuzipa nafasi ya kukuza mtaji na kutengeneza pamoja na kutekeleza mkakati wa MKUMBI II unaolenga kupunguza mlundikano wa ada na tozo, ambapo Wizara ya Fedha imetenga Sehemu Maalum ya Mapato Yasiyo ya Kodi (Non-Tax Revenue section) kuratibu eneo hilo’’ alifafanua Mhe. Munde.

Mhe. Munde alisisitiza taasisi za kitaalamu na washauri wa kodi kuendelea kutoa ushauri wenye maadili unaolinda uendelevu wa biashara na maslahi ya taifa kwa wakati mmoja, huku ukihimiza elimu ya kodi kuendelea kutolewa kwa jamii.

Mhe. Munde aliwaasa washiriki wa mkutano huo kutumia fursa hiyo ya kimkakati kujadili sera za kodi, fursa za uwekezaji na namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Huduma za Kodi wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na utoaji wa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu, na ushauri wa kibiashara ya Ernst &Young-Tanzania, Bw. Donald Nsanyiwa, alisema kuwa Mkutano huo una lengo la kujenga mfumo wa kodi wenye ufanisi, uwazi na unaochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani bila kuathiri shughuli za sekta binafsi.

Alisema mkutano huo utajikita katika maeneo makuu matatu ikiwemo kuimarisha ushirikiano wa hiari katika ulipaji kodi, kuziandaa biashara kukabiliana na mabadiliko ya kisheria na kisera, pamoja na kujenga uaminifu kati ya walipakodi na Mamlaka ya Mapato (TRA).

‘‘Tutajadili mapendekezo ya mbinu bora za kibiashara ambazo zinaweza kusaidia kuongeza utii wa sheria za kodi na wakati huo huo kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla. Tutarejea pia baadhi ya hoja na mapendekezo ya kikodi yaliyojadiliwa katika mwaka uliopita, pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali na namna mabadiliko hayo yanavyoweza kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini’’, alisema Bw. Nsanyiwa.

Aidha, Bw. Nsanyiwa aliongeza kuwa ni muhimu kuwa na majadiliano yenye kujenga ushirikiano kati ya wafanyabiashara, wataalamu wa kodi na Serikali, hasa katika kipindi ambacho kuna mabadiliko mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji.

Alisema katika mkutano huo, wataalamu wao watashirikisha uzoefu na maarifa kuhusu changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamizi na ulipaji wa kodi, pamoja na namna bora ya kuzitatua ili kuhakikisha kwamba mabadiliko yanayoendelea yanaeleweka vizuri na kwamba wafanyabiashara wanakuwa tayari kuyatekeleza.

Bw. Nsanyiwa aliongeza kuwa washiriki wa mkutano huo watapata fursa ya kujadili na kupata uelewa wa kina kuhusu namna ya kuboresha uelewa wa walipakodi kuhusu mifumo mipya ya kidijitali inayotumika katika usimamizi wa kodi kwa kuwa mifumo ya kidigitali imekuwa sehemu muhimu ya usimamizi wa kodi ili waweze kutumia mifumo hiyo kwa usahihi na kwa ufanisi.

Mkutano huo wenye kaulimbiu, (Bolder Thinking, Smarter Tax, Stronger Future), uliwakutanisha washiriki kutoka sekta ya umma na binafsi, wanadiplomasia, wawekezaji pamoja na wataalamu wa kodi.

Wizara ya Fedha imeanza kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kwa ajili ya ku...
21/10/2026

Wizara ya Fedha imeanza kikao cha ngazi ya wataalam cha mafungu yote yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kwa ajili ya kujadiliana kwa pamoja na kufanya tathmini ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mikakati ilyowekwa kwa kila fungu ili kufikia malengo ya mapato ya mwaka 2026/27.

Katika mwaka wa Fedha, 2026/27, Serikali imekadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 5.17 kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea na mashirika na taasisi za umma zilizo chini ya Msajili wa Hazina.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Bw. Amoury Amoury kwa niaba ya Kamshna wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka kimefanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mafungu yaliyoshiriki kikao hicho yanajumuisha Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Taasisi zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu (OWM-KVU), Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Madini, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashriki,Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,

Mafungu mengine ni, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Kamishna Jenerali wa Magereza. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Makao Makuu ya Polisi, Makao Makuu ya Uhamiaji, Mahak**a ya Tanzania na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema upatikanaji wa mitaji, uwekezaji katika viwanda na uboresha...
20/10/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema upatikanaji wa mitaji, uwekezaji katika viwanda na uboreshaji wa mazingira ya biashara ni muhimu katika kufanikisha malengo ya DIRA 2050, inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka takriban dola za Marekani bilioni 100 hadi dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza katika mkutano wa Wadau wa Mpango wa Fedha Mbadala na Ubunifu uliofanyika wakati wa kongamano la Tanzania Startup Week 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Mhe. Balozi Omar amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wawekezaji na wafanyabiashara kuwa na shauku na ujasiri wa kuwekeza mitaji, kwa kuzingatia uelewa wa watu wanaosaidiwa pamoja na sheria zinazosimamia shughuli hizo.

Ameeleza kuwa kufikia malengo ya Dira 2050 kunahitaji mabadiliko ya kiuchumi na kimuundo yatakayoongeza uzalishaji na kuimarisha sekta zenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Kwa sasa, kilimo kinachangia takriban asilimia 24 ya uchumi wa Tanzania, huku sekta ya viwanda ikichangia asilimia nane, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza mchango wa viwanda katika muundo wa uchumi” Alisema Mhe. Balozi Omar.

Kuhusu mwenendo wa uchumi, alisema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.6 mwaka 2024 na kufikia asilimia 5.9 mwaka uliofuata, huku lengo likiwa kufikia ukuaji wa asilimia 6.3 mwaka 2026.

Alibainisha pia kuwa mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini ya asilimia tano, sambamba na utulivu wa viwango vya ubadilishaji fedha na nakisi ya bajeti.

Katika eneo la mikopo, alisema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 33 kwa mwaka ulioishia Agosti huku sekta ya viwanda ikiwa haijaonesha maendeleo makubwa katika kunufaika na mikopo hiyo, jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha njia mbadala za upatikanaji wa mitaji, ikiwemo mitaji ya ubia (venture capital) na uwekezaji wa hisa binafsi (private equity).

Aidha, Mhe. Balozi Omar ameeleza kuwa Serikali imejizatiti kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya kodi, ikiwemo likizo ya kodi ya mwaka mmoja kwa biashara changa (startups) mpya na mabadiliko ya vizingiti vya kodi, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa biashara changa na kuongeza uwekezaji nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya DIRA 2050.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania,  Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameshiriki Mkutano ...
19/10/2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameshiriki Mkutano wa Mawaziri na Viongozi wa Ngazi ya Juu kuhusu Rasilimali Watu (Human Capital Ministerial Conclave), uliofanyika jijini Bangkok, Thailand, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia (WBG).

Mkutano huo ulijadili namna Akili Unde (AI) na teknolojia zinavyobadilisha mahitaji ya ujuzi katika soko la ajira, pamoja na umuhimu wa kuboresha mifumo ya elimu na mafunzo ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya waajiri na uchumi.

Aidha, washiriki walijadili mikakati ya kisera ya kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya ujuzi, ikiwemo ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs), matumizi ya teknolojia za kidijitali na mifumo bunifu ya ufadhili ili kupanua upatikanaji wa programu bora za mafunzo kwa wanafunzi na wafanyakazi.

Akichangia hoja iliyokuwa mezani, Dkt Mwamba alisema Tanzania kupitia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) umetenga dola za Marekani bilioni 14.6, sawa na asilimia 8 ya jumla ya dola za Marekani bilioni 183 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, kwa ajili ya elimu na maendeleo ya ujuzi.

Mpango huo ulioko katika DIRA 2050, unatarajia sekta binafsi kugharamia asilimia 70 ya uwekezaji wote uliopangwa, huku sekta ya umma ikichangia asilimia 30 iliyobaki.

Aliongeza kuwa, Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo wa Taifa (LTPP) umeweka malengo mahsusi ya uwekezaji wa sekta binafsi katika maendeleo ya ujuzi, yakiwemo kutoa mafunzo kwa watu milioni mbili katika ujuzi wa teknolojia za kisasa za uzalishaji viwandani, TEHAMA na nishati safi kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ifikapo mwaka 2040.

Aidha, Dkt. Mwamba amesema malengo mengine ni kuanzisha angalau programu 50 za ubia ifikapo mwaka 2030, vituo 200 vya kukuza na kusaidia biashara changa za vijana, pamoja na kutoa msaada kwa biashara ndogo na za kati 5,000.

Mkutano huo pia ulijadili hatua za kuhamasisha uwekezaji katika mafunzo, zikiwemo vivutio vya kikodi vinavyohusishwa na matokeo ya mafunzo, vinavyoweza kujumuisha punguzo la kodi la hadi asilimia 30; ubia katika ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya mafunzo; pamoja na mifumo ya ufadhili inayochanganya vyanzo mbalimbali vya fedha na inayozingatia matokeo.

Aidha, washiriki walisisitiza umuhimu wa kutambua ujuzi uliopatikana kupitia uzoefu wa kazi na njia zisizo rasmi, pamoja na kuweka mifumo ya kurasimisha ujuzi huo ili kuongeza fursa za ajira na kuwawezesha wafanyakazi kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Majadiliano hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika, kuongeza tija na kukuza ushindani wa uchumi katika mazingira yanayobadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia.

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania walipokutana na kufanya maz...
18/10/2026

Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania walipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), lililoko chini ya Benki ya Dunia, Bw. Ethiopis Tafara, jijini Bangkok nchini Thailand, ambapo wamejadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya sekta binafsi na upatikanaji wa ajira hususan kwa vijana.

Mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika utekelezaji wa Dira 2050 ya Tanzania, inayolenga kuibadilisha nchi kutoka uchumi wa dola za Marekani bilioni 100 wa sasa hadi hadi dola trilioni 1 katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa ili kufikia ukuaji huo kunahitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, hasa katika uwekezaji wa viwanda, miundombinu, na kilimo biashara, sekta zitakazochangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kuwa chanzo cha ajira za uhakika kwa vijana.

Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) la Benki ya Dunia, Bw. Ethiopis Tafara amesema Shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania kufanikisha malengo hayo ya Dira 2050 kwa kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia za kilimo (AgTech), huduma za afya, utalii na ujumuishaji wa kifedha.

Aidha, Bw. Tafara ameeleza nia ya Taasisi yake kuchangia maendeleo ya mpango wa Srikali ya Tanzania wa kuendeleza ushoroba wa kati (Central Corridor) ili uweze kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda huo kupitia usafirishaji wa mizigo na abiria na kusisimua shughui mbalimbali za kiuchumi katika ushoroba huo.

Sehemu kubwa ya mazungumzo yaligusia pengo la kifedha kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) ambapo IFC inapanga kufanya kazi na kampuni za teknolojia ya kifedha (fintech) na wafadhili wasio mabenki ili kutoa mikopo kulingana na takwimu za kitabia badala ya dhamana za kawaida.

Pande zote mbili zilionyesha dhamira ya kuharakisha miradi inayoendelea, hasa katika sekta za nishati na miundombinu ya kidijitali, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wake.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika kuimarisha ushir...
18/10/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Tanzania, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati, maendeleo ya rasilimali watu, nishati na miundombinu ya usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Mhe. Balozi Omar aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia juhudi za kupanua upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati, sambamba na mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika.

“Tanzania imenufaika na ufadhili wa IDA-20 wa dola bilioni 5.1 za Marekani, huku chini ya IDA-21 tukipangiwa dola bilioni 2.54 za Marekani na ahadi za ufadhili dola milioni 763.9, huku miradi mingine ikiendelea kuandaliwa kwa ajili ya utekelezaji” alisema Mhe. Balozi Omar

Akizungumzia ukubwa wa ushirikiano wa sasa kati ya Tanzania na Benki ya Dunia, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa jalada la miradi ya pamoja lina miradi 33 yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 8.8 za Marekani, ambapo miradi 30 ni ya kitaifa na mitatu ni ya kikanda, ambayo miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika eneo la usafirishaji, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika kuboresha Ushoroba wa Kati (Central Corridor), kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha bandari, reli na miundombinu mingine ya usafirishaji ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Serikali inalenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka njia ya usafirishaji na kuufanya kuwa Ushoroba wa Maendeleo na Ustawi wa Kiuchumi (Economic Prosperity Corridor), kwa kutambua na kuendeleza fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu hiyo.” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza Tanzania inathamini mchango wa Dkt. Kibwe katika kufanikisha majukwaa muhimu ya kimataifa yaliyofanyika nchini, yakiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Human Capital Summit) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Julai 2023, pamoja na Mkutano wa Mapitio ya Katikati ya Kipindi cha Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IDA) uliofanyika Zanzibar mwezi Desemba 2024.

Ameeleza kuwa mikutano hiyo imeipa Tanzania fursa ya kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya maendeleo ya Afrika na kimataifa, hususan katika kuboresha rasilimali watu, ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto za maendeleo barani Afrika.

Mhe. Balozi Omar alieleza matumaini ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mkurugenzi mpya atakayechukua nafasi hiyo Bi. Lonkhululeko Magagula, atakayechukua nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, ameipongeza Tanzania kwa hatua zilizopigwa katika kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Dunia, akibainisha kuwa thamani ya miradi ya maendeleo kati ya pande hizo imeongezeka kutoka takribani dola bilioni nne alipokuwa akianza majukumu yake hadi kufikia kiwango cha sasa.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa katika kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa anajivunia kushuhudia Tanzania ikifikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha kati.

Dkt. Kibwe alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kutumia fursa za uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya sekta ya madini, akieleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 30 zinazozingatiwa katika mpango wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya madini na rasilimali zake.

“Mpango huu unajumuisha maeneo muhimu matatu ambayo ni kuimarisha utawala na usimamizi wa sekta ya madini, kuendeleza miundombinu inayowezesha uchimbaji na usafirishaji wa madini, pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Dkt. Kibwe.

Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano na washirika wake wa maendeleo ili kutumia fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu katika kutekeleza miradi ya kimkakati na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, na maafisa wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kuhakikisha elimu...
18/10/2026

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kuhakikisha elimu ya bima inawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake, wajasiriamali na wananchi wa vijijini

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2025.

Mhe. Munde alisema kuwa lengo ni kuhakikisha bima inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania, kwa kuwa na uelewa wa umuhimu wake, namna ya kupata huduma na taratibu za kudai fidia wanapokumbwa na majanga mbalimbali.

“Elimu hiyo isiishie mijini pekee. Iwafikie wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake, waendesha pikipiki na bajaji, wafanyakazi, wajasiriamali na wananchi wa maeneo ya vijijini. Tunataka kuona bima inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania”, alisisitiza Mhe. Munde.

Alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma za bima ili kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo kwasababu sehemu kubwa ya wananchi bado hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa bima, namna ya kupata huduma za bima na namna ya kufuata taratibu za kudai fidia.

Aidha, Mhe. Munde alisisitiza umuhimu wa sekta ya bima katika kufanikisha azma ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance – UHI), kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya masuala ya afya pamoja na taasisi nyingine zinazohusika ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na kinga ya afya.

“Serikali inaendelea kuweka mkazo mkubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazopatikana kwa wote. Katika kutekeleza azma hii, Bima ya Afya kwa Wote ni eneo muhimu sana. Sekta ya bima ina nafasi kubwa katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata ulinzi wa afya zao kwa gharama nafuu” alisema Mhe. Munde.



Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa maslahi ya wateja wa huduma za bima yanalindwa na mwenendo wa watoa huduma wa bima unasimamiwa kwa weledi na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.



Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria ili kuhakikisha ukuaji thabiti wa sekta ya bima iliyo jumuishi na inayochangia katika maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hamad Bakar Hamad alisema Sekta ya bima nchini ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa Taifa, kulinda wananchi dhidi ya vihatarishi mbalimbali na kuchochea uwekezaji kupitia ukusanyaji wa rasilimali za muda mrefu.



Alisema ni muhimu kwa TIRA kuongeza juhudi za kupanua wigo wa huduma za bima, ikiwemo matumizi ya huduma za bima kupitia benki (bancassurance), bima ya Kiislamu (Takaful) na majukwaa ya kidijitali, ili kuongeza upatikanaji wa huduma, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi.



Aidha, Mhe. Hamad aliisisitiza TIRA na watoa huduma za bima kuimarisha matumizi ya teknolojia katika usajili, uuzaji wa bima, malipo na ulipaji wa madai ili kuongeza uwazi, kudhibiti udanganyifu na kuwafikia wananchi wengi zaidi huku akitilia mkazo kuwa maendeleo ya kidijitali yanapaswa kuambatana na ulinzi wa taarifa za wateja, usalama wa mifumo na uzingatiaji wa sheria na kanuni husika.

Awali, akitoa maelezo ya mwenendo wa Sekta ya Bima nchini, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, alisema Soko la bima nchini limeendelea kukua kwa kasi katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, likichangia kuimarisha uchumi na kuongeza fursa za ajira.

Alisema ukuaji huo umechangiwa na upanuzi wa huduma za bima, kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima na juhudi za wadau katika kuboresha huduma.

Dkt. Saqware alibainisha kuwa ajira katika sekta hiyo ziliongezeka kutoka takribani 3,000 hadi kufikia 6,474, huku ada za bima zilizokusanywa zikiongezeka kutoka Shilingi bilioni 824.3 mwaka 2020 hadi Shilingi trilioni 1.015 mwaka 2024.

Mafanikio hayo yanaonesha sekta ya bima inayozidi kuimarika katika kukuza shughuli za kiuchumi na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.

Aidha, matumizi ya huduma za bima yameendelea kuongezeka, hali inayoashiria kuimarika kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujikinga dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha hasara za kifedha.

Vilevile, Dkt. Saqware alisema kuwa Sekta ya Bima imeendelea kuchangia ustawi wa wananchi kupitia ulipaji wa madai na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya T...
17/10/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) katika kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana, kuendeleza elimu, kuvutia uwekezaji na kukuza sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la UNDP Duniani ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ubelgiji, Bw. Alexander De Croo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, jijini Bangkok, nchini Thailand.

Amesema ajira kwa vijana ni moja ya vipaumbele muhimu vya maendeleo ya Tanzania kutokana na muundo wa idadi ya watu nchini, ambao unaonesha kuwa sehemu kubwa ya wananchi ni vijana, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha kupata ujuzi, mitaji, teknolojia na masoko yatakayowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

Alisisitiza kuwa idadi kubwa ya vijana inaweza kuwa fursa muhimu ya kukuza uchumi iwapo itawezeshwa ipasavyo, lakini ikikosa fursa za kiuchumi inaweza kusababisha changamoto za kijamii na kiuchumi, hususan pale vijana wanapokosa matumaini ya maisha bora.

“Masuala ya ajira na vijana ni mapana sana. Tunahitaji kuhakikisha vijana wanapata ujuzi sahihi, mitaji nafuu ya kuanzisha biashara, teknolojia, maarifa na upatikanaji wa masoko ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya nchi,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu na miundombinu ya elimu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa idadi ya watu, huku akibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupanua usawa wa upatikanaji wa elimu kwa wavulana na wasichana katika ngazi mbalimbali.

Hata hivyo, alisema ukuaji wa idadi ya watu unaendelea kuongeza mahitaji ya shule, walimu, vitabu na miundombinu mingine, hivyo uwekezaji endelevu unahitajika ili kuimarisha upatikanaji wa elimu na kuboresha ubora wake.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutambua fursa za uwekezaji na kuandaa miradi inayoweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, akieleza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia hivi sasa inaendelea na zoezi la kubaini fursa za biashara na uwekezaji katika Ushoroba wa Kati (Central Corridor), unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya ndani ya nchi kupitia miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo reli ya kisasa (SGR), huku kukiwa na uwezekano wa kupanua fursa hizo hadi nchini Rwanda.

“ukanda huu una fursa kubwa katika sekta za kilimo, madini, utalii, usafirishaji na uendelezaji wa vituo vya usafirishaji na ugavi wa bidhaa (logistics centres), zinazoweza kuvutia uwekezaji na kuchochea uzalishaji pamoja na ajira” alisema Mhe. Balozi Omar

Pamoja na hayo alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kupitia mapendekezo ya k**ati zilizoundwa kuchunguza changamoto zinazokabili mfumo wa kodi na mazingira ya ufanyaji biashara ili kuboresha mfumo huo na kuimarisha mazingira ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkiu wa Shirika la Maendelo la Umoja wa Mataifa - UNDP, Bw. Alexander De Croo, alieleza utayari wa Shirika hilo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza ajenda za maendeleo ya nchi, ikiwemo kuwawezesha vijana, kuimarisha ujuzi na kukuza fursa za kiuchumi kupitia ushirikiano na Serikali, sekta binafsi na taasisi nyingine za maendeleo.

Alisema uwekezaji unapaswa kuangaliwa k**a mkakati wa muda mrefu wa maendeleo, hususan katika matumizi bora ya rasilimali za asili, ikiwemo madini adimu yanayohitajika katika mabadiliko ya mifumo ya nishati duniani.

Bw. De Croo alitoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania kwa kuandaa Mifumo Jumuishi ya Kitaifa ya Ufadhili wa Maendeleo (INFFs), itakayosaidia kuimarisha upatikanaji na uratibu wa rasilimali za kugharamia vipaumbele vya maendeleo.

Alisema UNDP, kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji na Ukuaji wa Tanzania, inalenga kubadilisha fursa hizo kuwa miradi yenye nyaraka na mipango madhubuti ya kifedha na kibiashara inayoweza kuvutia wawekezaji, kabla ya Mkutano wa uwekezaji unaotarajiwa kufanyika Juni 2027 nchini Tanzania.

“Tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika maandalizi ya mkutano huo na kutafuta ufadhili wa miradi ya miundombinu endelevu na uchumi wa buluu kupitia ushirikiano na Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi na kuongeza mchango wa uwekezaji katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi” alisema Bw. De Croo

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Enock Koola na Maafisa wengine wa Serikali na UNDP.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya...
17/10/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Abebe Selassie, kando ya Mikutano ya Mwaka ya IMF na Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Katika kikao hicho, Mhe. Balozi Omar alimshukuru Bw. Selassie kwa ushirikiano na mchango wake kwa Tanzania katika kipindi chote alichohudumu katika nafasi hiyo, hususan katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na IMF katika masuala ya uchumi na maendeleo na kujadili namna anavyoweza kutumia uzoefu wake katika nafasi nyingine alizonazo nje ya mfumo wa Benki ya Dunia.

Kikao hicho kilihudhiriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bw. Japhet Justine na Maafisa wengine waandamizi wa IMF na Serikali.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amekutana kwa mazungumzo ya pande mbili na Waziri wa Fedha na Uchum...
17/10/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amekutana kwa mazungumzo ya pande mbili na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Poland, Mhe. Andrzej Domański, kujadili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kifedha kati ya nchi hizo mbili, kikao kilichofanyika kando ya Mikutano ya Shirika la Fedha la kimataifa -IMF na Benki ya Dunia, jijini Bangkok, nchini Thailand.

Mazungumzo hayo yalilenga kutathmini maendeleo ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Poland, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati ya miundombinu kupitia Shirika la Bima ya Mikopo ya Mauzo ya Nje la Poland (KUKE), pamoja na kubaini fursa mpya za ushirikiano wa maendeleo.

Poland imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), unaolenga kuimarisha usafiri, kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika ukanda.

Viongozi hao wamejadili pia uwezekano wa kupanua ushirikiano katika maeneo yenye manufaa ya pamoja, kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania na fursa za uwekezaji zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza tija.

Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na washirika wake wa kimataifa ili kuvutia uwekezaji, kupata rasilimali za kufadhili miradi ya kimkakati na kuharakisha utekelezaji wa Dira 2050 kwa manufaa ya wananchi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, na baadhi ya maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha ya Tanzania na nchini Poland.

Address

Magufuli City, Treasury Street, Mtumba
Dodoma
40468

Opening Hours

Monday 09:00 - 16:30
Tuesday 09:00 - 16:30
Wednesday 09:00 - 16:30
Thursday 09:00 - 16:30
Friday 09:00 - 16:30

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Wizara ya Fedha posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to Wizara ya Fedha:

Shortcuts

Share