14/05/2026
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amelishauri Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA), kuja na mwarobaini wa kukabiliana na changamoto zinazokwaza ufanisi wa ufanyaji biashara ya kimataifa miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza hilo.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume-Zanzibar.
Alionesha wasiwasi wake juu ya ongezeko la biashara ya mtandaoni, maendeleo ya teknolojia ikiwemo unde, big data, na changamoto za kiusalama zinazoathiri biashara ya kimataifa na alilitaka baraza hilo kuchukua jukumu la kuimarisha ushirikiano na kukuza taasisi za kisasa za forodha.
Mhe. Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali, usimamizi wa vihatarishi pamoja na matumizi ya teknolojia za ukaguzi ili kuongeza ufanisi katika udhibiti wa mipaka na ukusanyaji wa mapato.
Akitaja Dira ya Maendeleo 2050, Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na ujumuishaji wa mifumo ili kuendeleza biashara na kuvutia Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Nje (Foreign Direct Investment -FDI).
“Nina wahimiza wajumbe kutumia jukwaa la mkutano huu kuimarisha ushirikiano, kubadilishana maarifa na kutafuta suluhu za vitendo na nina wahimiza wageni kutembelea vivutio vya Tanzania ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, ameeleza kuwa TRA imeendelea kufanya maboresho makubwa ya mifumo ya forodha kupitia uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, uimarishaji wa mifumo ya usimamizi wa mizigo pamoja na kuunganisha huduma za forodha katika dirisha moja la utoaji huduma kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha biashara.
Mkutano huo wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA), unawakutanisha Wanachama kutoka Mataifa 24 na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa forodha, mageuzi ya kidijitali, usalama wa mipaka, uboreshaji wa biashara na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya forodha duniani huku ukilenga kuimarisha ustawi wa uchumi wa nchi wanachama wa ukanda huo.
14/05/2026
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameshiriki na kuongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia Masuala ya Fedha na Uchumi - Ngazi ya Makatibu Wakuu, uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha, ambao umejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika maeneo ya kiuchumi hususan hali ya mwenendo wa viashiria vya Uchumi Mpana kwa Nchi zote wanachama wa Jumuiya, ambayo yatawasilishwa katika Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elija Mwandumbya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib M***a, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursali Milanzi, na Wataalamu wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA, Benki Kuu ya Tanzania – BOT, na Ofisi ya Taifa ya Takwimu-NBS.
14/05/2026
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, amekiagiza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Fedha kuratibu ujenzi wa mchakato wa utekelezaji wa majukumu (business processes) za kidigitali ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, wakati akifungua mafunzo mafunzo ya Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani wa Wizara ya Fedha, kwa
Menejimenti ya Wizara hiyo, yaliyofanyika katika Hotel ya Morena mkoani Morogoro.
Alisema business processes mpya zinazotakiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa Mfumo wa Ununuzi (NeST), ufuatiliaji na udhibiti wa mapato kupitia big data analysis, ufuatiliaji wa miradi ya PPP, miradi ya alternative financing, ulipaji wa michango ya Serikali kwenye taasisi za kimataifa, na ufuatiliaji wa mapato yasiyo ya kodi.
Aidha, Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kimetakiwa kuhakikisha kuwa business processes hizo zinajengwa kwa mfumo wa kielektroniki ili kurahisisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ufanisi wa mifumo ya kiutendaji.
Bw. Sendo, alifafanua kuwa mafunzo hayo yataiwezesha Menejimenti na Watumishi wa Wizara kuelewa dhana na mbinu za udhibiti wa ndani, kujifunza namna ya kuchambua viashiria hatarishi, na kuimarisha business processes zilizopo.
“Mwongozo huu utakuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa njia za kidigitali, kuwezesha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kufanya tathmini kwa mujibu wa Mwongozo wa Kimataifa wa Ukaguzi wa Ndani wa mwaka 2024, na kuweka vigezo vya kupima ufanisi wa mifumo ya kiutendaji”, alisisitiza Bw. Sendo.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kufuatilia kwa umakini ili kuutumia Mwongozo huo kuboresha mfumo wa udhibiti wa ndani katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha uchumi wa taifa kupitia usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Naye Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Kenneth Nindie, alitoa rai kwa Idara zote za Serikali kuhakikisha wanatumia vizuri Mwongozo huo ili uweze kuwasaidia kuweka taratibu vizuri na malengo ya Wizara yanafikiwa kwa ufasaha.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Msaidizi Bw. Abraham Msechu, amesema kuwa mafunzo yatasaidia Menejimenti ya Wizara kupata uelewa wa Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani.
Akizungumzia mafunzo hayo mmoja wa washiriki, Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Madeni, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Khama, aliahidi kuyafanyia kazi mafunzo yote waliyopata katika Idara na Vitengo ili kufikia malengo ya Serikali katika udhibiti wa ndani.
Mafunzo hayo yamewajumuisha Menejimenti ya Wizara ya Fedha pamoja na Watumishi wa Wizara na Wawezeshaji kutoka Kampuni ya Ushauri (KPMG).
14/05/2026
Serikali inaendelea na zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu rasimu ya Kanuni za bima za lazima baada ya kukamilisha maandalizi ya rasimu ya Kanuni za bima hizo.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ilemela Mhe. Kafiti William Kafiti, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaandaa Kanuni za Bima za lazima ili kutekeleza Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 na kuongeza Mapato ya Serikali.
Mhe. Munde alisema kuwa Serikali, kupitia Sheria ya Fedha Namba 5 ya mwaka 2022, ilifanya marekebisho ya Sheria ya Bima Sura 394 ili kuongeza wigo wa bima za lazima kwa lengo la kuongeza kinga kwa majanga ambayo yana madhara makubwa kwa wananchi yanapotokea.
Alisema kuwa utekelezaji wa marekebisho hayo katika Sheria husika unailazimu Serikali kuandaa Kanuni, aidha kwa kuzingatia umuhimu wa suala hili alieleza kuwa Serikali imedhamiria kukamilisha mchakato huo mapema iwezekanavyo.
14/05/2026
Wizara ya Fedha, imeendelea kupitia upya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, kwa lengo la kuioanisha na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kupitia kikao kazi kilichowakutanisha watelekezaji wa ununuzi wa umma na ugavi katika ngazi za chini za Serikali za Mitaa, Shule za Msingi na Sekondari pamoja na vituo vya afya.
Mchakato huo ulianza kwa kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper, Jijini Dodoma, ambapo watekelezaji wa Ununuzi wa Umma katika ngazi za chini za Serikali za Mitaa, Shule za Msingi na Sekondari pamoja na vituo vya afya, walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Sheria hiyo.
Akizungumza wakati wa kufunga Kikao hicho, Kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma - Wizara ya Fedha, Bw. Alex J. Habara, Kamishna Msaidizi wa Idara hiyo Bi. Emma Komba, alisema mapitio hayo yanalenga kujenga mfumo wa kisasa unaojumuisha hatua zote za mnyororo wa ugavi, kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji wa mizigo, upokeaji, uhifadhi na utunzaji, usambazaji, hadi uondoshaji wa mali za umma.
Aliongeza kuwa mapitio hayo pia yamezingatia nguzo na malengo ya Dira ya Maendeleo 2050, ikiwemo ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, pamoja na maendeleo jumuishi na endelevu.
‘’Mapitio ya Sheria hii ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha kuwa masuala yote yanayohusu mnyororo mzima wa ugavi yanajumuishwa kikamilifu katika Sheria mpya, na kwamba mageuzi hayo yatakuwa chachu ya kuchochea maendeleo ya Taifa’’ alisema Bi. Emma.
Aliongeza kuwa Wizara ya Fedha, itazingatia na kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyowasilishwa kwa kuyachambua kwa kina ili kubaini maeneo ya kuboresha na kuweka misingi imara itakayosaidia Taifa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Paul Kadushi, alisisitiza kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu kwa watekelezaji wote wa ununuzi wa umma na ugavi ili kurahisisha utendaji kazi katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
‘’Sisi PPRA k**a wadhibiti wa ununuzi wa umma, sehemu ya nguvu ambayo tumeelekeza kwenye kutoa elimu kwa wazabuni na makundi maalumu, tunahitaji pia kuelekeza kwenu na kuwajengea uwezo ili muweze kutekeleza kazi za ununuzi wa umma kwa ufanisi zaidi’’ alisema Bw. Kadushi.
Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, imeipa Wizara ya Fedha, jukumu la kisheria la kupitia na kuhuisha sera, sheria, kanuni, miongozo, pamoja na maelekezo mbalimbali yanayohusu ununuzi wa umma na ugavi nchini.
13/05/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amewataka Watumishi wa Wizara ya Fedha na wananchi kwa ujumla kuwa makini na taarifa zisizo sahihi kuhusu lishe kupitia mitandao ya kijamii, ikiwemo taarifa zinazopinga matumizi ya vyakula vya wanga kwa watoto.
Rai hiyo imetolewa katika Ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha jijini Dodoma, wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za uchunguzi wa viashiria vya magonjwa ya moyo pamoja na elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo magonjwa ya moyo, kwa watumishi wa Wizara ya Fedha.
Dkt. Kisenge alisema kuwa utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya vyakula vya wanga inapaswa kuzingatia umri na hali ya afya ya mtu, kwani watoto na vijana wengi bado wanahitaji wanga kwa maendeleo yao ya mwili na akili, hususan wale wasiokuwa na changamoto za kiafya.
“Vijana na watoto wanahitaji vyakula vya wanga kwa ajili ya kupata nguvu na kusaidia ukuaji wa akili, upungufu wa wanga unaweza kusababisha watoto kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri na kujifunza”, alisema Dkt. Kisenge.
Alisisitiza kuwa jambo muhimu ni kuhakikisha watoto wanapata lishe kamili kwa ajili ya ukuaji wao.
Alisema kuwa mahitaji ya vyakula hubadilika kulingana na umri, akibainisha kuwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 wana vihatarishi zaidi vya magonjwa yasiyoambukiza ikilinganishwa na vijana.
Aidha Dkt. Kisenge, alitoa wito kwa Watumishi wa Wizara ya Fedha na watanzania kwa ujumla kula mlo kamili hususani vyakula vya asili zikiwemo mbogamboga na matunda ili kulinda afya za miili yao.
Akieleza kuhusu matumizi ya chumvi alisema kuwa wapo wanaopinga matumizi ya chumvi, alisema chumvi ni muhimu kwa maisha ya binadamu ikitumiwa kwa usahihi.
Vile vile amewataka Watumishi wa Wizara ya Fedha kuepuka matumizi ya yaliyopita kiasi ya pombe, vinywaji vinavyoongeza nguvu na kufanya kazi kupita kiasi, ametoa wito wa kupata mlo kamili, kufanya mazoezi na kuwa na utamaduni wa kupima afya.
Alisema kuwa utamaduni wa kupima afya unasaidia kupunguza gharama kubwa za matibabu na pia kumfanya mtumishi kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, alisema kuwa ili Wizara ya Fedha iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa, ni muhimu watumishi kuwa na afya njema.
Alisema ukosefu wa elimu kuhusu masuala ya afya unaweza kusababisha kupuuzwa kwa viashiria muhimu vya magonjwa vinavyohitaji kufanyiwa kazi mapema.
Bw. Mwenda aliishukuru JKCI kwa kutoa huduma hizo muhimu pamoja na ahadi ya kuendelea kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kila mwaka kwa watumishi wa Wizara ya Fedha.
Aidha, alisema watumishi wameonesha mwitikio mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo ili kupata elimu ya afya na huduma za uchunguzi kutokana na umuhimu wake.
Alibainisha kuwa watumishi wa Wizara ya Fedha watatumia vizuri elimu waliyoipata kuhusu mtindo bora wa maisha, lishe sahihi na umuhimu wa kufanya mazoezi, ili kuwa na afya njema itakayosaidia kutoa huduma kwa watanzania kwa ufanisi.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete - JKCI
13/05/2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Montfort Mlachila, kuhusu maendeleo ya uendelezaji wa ujuzi (Capacity Development) kupitia AFRITAC East.
Katika kikao hicho, Dkt. Natu ameishukuru AFRITAC East kwa kuendelea kuwezesha mafunzo kwa wataalam wa taasisi za Serikali ikiwemo Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akiomba ushirikiano zaidi katika kuandaa mafunzo yanayoendana na mahitaji na mabadiliko ya kidunia.
Kwa upande wake, Bw.. Mlachila alisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu fursa za mafunzo hayo na kuhimiza nchi wanachama wa AFRITAC East kuendelea kutoa michango ili kuiwezesha Taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa AFRITAC East, Bi. Clara Mira na maafisa wengine kutoka Tanzania na Taasisi hiyo.
13/05/2026
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Serikali ya Tanzania zimefikia makubaliano ya ngazi ya wataalamu kuhusu ukamilishaji wa tathmini za mwisho za Mpango wa Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii na Resilience Sustainability Facility (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hatua itakayoiwezesha Tanzania kupata ufadhili wa takribani dola za Marekani milioni 375.5 baada ya kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya IMF.
Fedha hizo kiasi cha dola za Marekani milioni 375.5 kitaifanya Tanzania inufaike na mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.052 za kusaidia miradi ya kiuchumi na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 563.8 za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi tangu utekelezaji wa program hizo uanze.
Hayo yamebainishwa na IMF kupitia Kiongozi wa Timu ya Wataalamu ya Shirika hilo iliyofanya ziara nchini, Bw. Nicolas Blancher, baada ya kikao cha kuhitimisha ziara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam, huku Timu ya Tanzania ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb).
Akitoa taarifa hiyo Kiongozi wa Timu ya Wataalamu ya Shirika hilo, Bw. Nicolas Blancher, alisema kuwa IMF imeridhishwa na utekelezaji wa programu hizo mbili huku ikibainisha kuwa malengo makuu ya kiuchumi yamefikiwa kwa kiwango kikubwa.
Bw. Blancher alisema kuwa malengo mapana ya programu hizo yamefikiwa, ukuaji wa uchumi umeendelea kuwa imara, mfumuko wa bei umeendelea kuwa thabiti na ndani ya kiwango kinacholengwa na Benki Kuu ya Tanzania, kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kimeendelea kuwa katika kiwango cha kuridhisha, huku matumizi ya Serikali katika sekta za elimu na afya yakiongezeka sambamba na hatua za kuimarisha ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali imeimarisha uthabiti wa uchumi jumla, imeongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatari nyingine za kiuchumi” alisema Bw. Blancher
Aliongeza kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.9 mwaka 2026 huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kubaki ndani ya lengo la Benki Kuu ya Tanzania la asilimia 3 hadi 5, na Taasisi hiyo imepongeza namna Serikali ilivyoweza kukabiliana na athari za changamoto za kiuchumi duniani ikiwemo vita vya Mashariki ya Kati kupitia sera madhubuti za kifedha na fedha.
“Utekelezaji thabiti wa bajeti, ukusanyaji mzuri wa mapato ya kodi, pamoja na kuendelea kulipa marejesho ya kodi na madeni ya ndani kwa wakati, ni hatua muhimu zitakazosaidia kuendeleza ukuaji wa sekta binafsi na kulinda matumizi ya kijamii katika afya, elimu na ulinzi wa jamii” alisema Bw. Blancher.
IMF imesema kuwa katika kipindi cha kati na mrefu, Tanzania ina nafasi nzuri ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa itaendelea kutekeleza mageuzi yatakayokuza mtaji rasilimali watu, kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.
“Kwa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya programu zinazoungwa mkono na ECF na RSF, ukuaji na maendeleo ya uchumi wa Tanzania yatategemea kuharakishwa kwa mageuzi ili kufikia malengo makubwa yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususan katika maeneo ya maendeleo ya rasilimali watu na sekta binafsi” alisema Bw. Blancher
IMF ilihitimisha kwa kusema kuwa, Vipaumbele muhimu ni pamoja na kuongeza zaidi mapato ya ndani ili kuunda nafasi ya kifedha kwa matumizi ya kijamii yenye kipaumbele huku ikiendelea kudumisha uwekezaji katika miundombinu; kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na uwekezaji; kuendeleza uhuru wa Benki Kuu; pamoja na kuboresha mazingira ya biashara.
Mageuzi endelevu ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi pia yatasaidia kuongeza ustahimilivu na uendelevu wa uchumi, ikiwemo kwa kupanua mifumo ya hifadhi ya jamii na kusaidia uwekezaji katika nishati jadidifu.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo ya mafanikio makubwa ya utekelezaji wa program hizo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), alisema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza program hizo kwa umakini mkubwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Aliihakikishia IMF kuwa Tanzania itaendelea kuwa makini katika matumizi ya Fedha hizo ili malengo yaliyowekwa ya kuwa na uchumi imara, thabiti na jumuishi yanafikiwa na kuleta tija kwa uchumi wa Taifa na maendeleo ya watu.
11/05/2026
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), kuhakikisha kuwa sekta ya uhasibu nchini inajengwa katika misingi imara ya maadili ili kuzalisha wataalamu wenye uadilifu, uwajibikaji na weledi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Mhe. Balozi Omar alitoa maagizo hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Bodi hiyo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema Serikali inaendelea kutegemea taaluma ya uhasibu k**a nguzo muhimu katika kuhakikisha usimamizi bora wa fedha, uwazi wa taarifa za kifedha pamoja na kuimarisha imani ya wananchi na wawekezaji katika mifumo ya kiuchumi nchini.
“Ni muhimu sana kwa NBAA kuhakikisha kuwa wataalamu wa kada ya uhasibu wanalelewa katika misingi ya maadili, uaminifu na uzalendo kwa sababu taaluma hii inagusa moja kwa moja usimamizi wa rasilimali za Taifa,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, aliipongeza NBAA kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua katika kuboresha taaluma hiyo ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa taarifa za fedha pamoja na kuendelea kusajili wahasibu na kampuni za ukaguzi nchini.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Sylvia Temu, alisema Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusimamia taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini huku ikiweka mkazo katika kujenga wataalamu wenye viwango vya kimataifa.
Alieleza kuwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, NBAA imefanikiwa kusajili Wahasibu Wahitimu (CPA Graduate Accountants) 8,864, Wahasibu wa ngazi ya Associate 6,631 pamoja na Wahasibu wa ngazi ya Fellow 529.
Aidha, CPA Prof Temu alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, kampuni mpya 22 za ukaguzi pamoja na kampuni 19 za kihasibu zilisajiliwa huku wahasibu 271 wakisajiliwa rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema kuwa hivi sasa imekamilisha kutengeneza Mfumo wa kisasa wa ukusanyaji wa taarifa za fedha unaojulikana k**a NBAA-VN ambao tayari umekusanya zaidi ya taarifa za fedha 11,000 kutoka kampuni mbalimbali nchini, ambao utasaidia kudhibiti udanganyifu wa taarifa za fedha, kuzuia kampuni hewa za ukaguzi na kuongeza uwazi katika sekta ya fedha.
“Tunataka kuhakikisha taarifa za fedha nchini zinakuwa salama, sahihi na zinapatikana kwa urahisi kwa taasisi husika za Serikali na Taasisi nyingine za sekta binafsi zikiwemo benki,” alisema CPA. Prof. Mzenzi
CPA. Prof Mzenzi aliongeza kuwa, zaidi ya wahasibu 2,149 wamepatiwa mafunzo kuhusu viwango vya kimataifa vya taarifa za fedha za uendelevu (Sustainability Financial Reporting), hatua inayolenga kuandaa wataalamu wanaozingatia mazingira, uwajibikaji na mabadiliko ya tabianchi katika utoaji wa taarifa za kifedha.