03/06/2026
🚀 𝐇𝐚𝐛𝐚𝐫𝐢 𝐧𝐣𝐞𝐦𝐚!
Suluhu ya Kodi App sasa inapatikana kwa Android na iPhone (iOS). 📱
Furahia huduma za Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) kwa urahisi, popote ulipo na wakati wowote, kiganjani mwako.
Pakua sasa na uanze kutumia.
01/06/2026
Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) na Wakala wa Kodi wa Denmark wamefanya kikao cha pamoja cha ushirikiano Wizara ya Fedha Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Kikao hicho kililenga kujadili na kubainisha maeneo muhimu ya ushirikiano yatakayochangia maendeleo endelevu ya Taasisi hizo mbili. Aidha, pande hizo zilijadiliana kuhusu kubadilishana uzoefu na mbinu bora za utendaji kwa lengo la kuongeza ulipaji kodi wa haiari na kupunguza gharama kwenye usimamizi na ukusanyaji wa kodi.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza chachu katika mlolongo mzima wa ukusanyaji wa kodi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau mbalimbali wa sekta ya kodi.
15/05/2026
Baadhi ya matukio katika picha za Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), uliofanyika tarehe 14–15 Mei 2026 mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani.
14/05/2026
Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya 4R’s ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kuimarisha mazingira ya ulipaji kodi wa hiari pamoja na kuongeza uaminifu kati ya mlipakodi na Serikali.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa TOST uliofanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Aidha, Bw. Mwenda amewataka wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuendelea kuzingatia ushirikiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufanikisha maono ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. Erastus Mtui, amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili na kufanyia kazi hoja mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
01/05/2026
Matukio katika Picha ni Wafanyakazi wa Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) ambao wameungana na Wafanyakazi wengine katika kusherehekea maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
29/04/2026
Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) inaendelea kuboresha huduma zake kwa kuhakikisha Wananchi wanapata huduma kwa urahisi, haraka na bila ulazima wa kufika ofisini.
Kupitia maboresho ya mifumo ya huduma kupitia simu za kiganjani, TOST inalenga kumfikia kila mwananchi popote alipo, ikiwa ni pamoja na watumiaji wa simu za kawaida ambazo sio za kupapasa, ili waweze kupata huduma muhimu kwa urahisi hata bila matumizi ya kifurushi cha intaneti.
Hii ni hatua muhimu katika kujenga huduma jumuishi, bora na inayomfikia kila mtu bila kujali aina ya simu anayomiliki. Maboresho hayo yanatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika mwisho wa Mwezi Mei 2026.