04/07/2023
WAZIRI WA MADINI MHE. DKT DOTTO MASHAKA BITEKO AFUNGUA ZAHANATI YA KIJIJI NYAMISHIGA
Julai 3, 2023
Waziri wa Madini nchini Mheshimiwa Dkt Dotto Mashaka Biteko jana amefungua zahanati na kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika Kijiji cha Nyamishiga, Kata ya Lunguya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Akizungumza katika ufunguzi wa zahanati hiyo Mhe Dkt Biteko amewapongeza Kikundi cha Wanawake wachimbaji wadogowadogo (TAWOMA-MSHIK**ANO) ambacho kilijitolea kutekeleza ujenzi wa Zahanati hiyo pamoja na kununua gari vyote vikiwa na thamani ya Tsh Milioni 289.
Mbali na kukishukuru kikundi hicho Dkt Biteko pia amewapongeza Viongozi mkoani Shinyanga kwa namna wanavyotetea na kusimamia maslahi ya wachimbaji wadogowadogo. "Kwa Shinyanga hakika mna viongozi makini sana, mnaye Mama Mndeme mkuu wa Mkoa huu anapambana sana kuwatetea wachimbaji, kwahilo nampongeza sana lakini pia mnaye Mkuu wenu wa Wilaya Mhe Mboni anachapa kazi haswa, watu hawa hawalali kwa ajili ya kuwatetea ninyi." Amesema Dkt Biteko.
"Kipekee kabisa nimpongeze na nimshukuru sana Mbunge wa Jimbo hili Mhe Iddi Kassim Iddi anahangaika mno kuwapigania wachimbaji hawa, amekuwa akinifuata kila mara kunieleza changamoto mnazokutana nazo nami nashirikiana naye katika kutatua changamoto hizo na kiukweli Mbunge wenu anastahili pongezi nyingi sana kwenye hili" Aliongeza Dkt Biteko.
Aidha, Dkt Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha sekta ya Madini nchini hususani kundi la wachimbaji wadogowadogo ambao hapo awali walionekana hawawezi kuendesha shughuli za uchimbaji lakini chini ya utawala wake ametoa kipaumbele kwa kundi hilo na mafanikio yanaonekana.
Awali akimkaribisha Mhe.Dkt Biteko Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Christina Mndeme amemshukuru Waziri huyo kwa kutenga muda kuja Shinyanga na kuwaunga mkono katika shughuli hiyo ambapo pia alimuomba afikishe shukrani za Mkoa huu kwa Rais Dkt Samia kutokana na fedha nyingi za maendeleo alizozileta katika mkoa huu.
01/07/2023
DKT. MSONDE AFANYA ZIARA HALMASHAURI YA WILAYA YA MSALALA.
Julai 1, 2023
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kitengo cha Elimu Dkt Charles Msonde amefanya ziara ya siku moja katika Halmashauri ya Msalala kwa lengo la Kukagua miradi mbalimbali ya sekta ya Elimu ambapo ametembelea na kukagua Ujenzi wa shule mpya ya Msingi Bulyanhulu pamoja na Ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Segese.
23/06/2023
Juni 22, 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo hadi kufikia Juni 19, 2023 Halmashauri ilikuwa imevuka lengo ikiwa imekusanya asilimia 102 ya mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Pongezi hizo amezitoa kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Msalala kilichoketi jana kwa ajili ya kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (C.A.G) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2022.
Akitoa pongezi hizo Bi Mndeme alisema kuwa Halmashauri ya Msalala imekuwa Halmashauri ya mfano kwa kasi yake ya ukusanyaji mapato na kwamba mafanikio hayo ni kutokana na jitihada na ushirikiano wa pamoja uliopo baina ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Waheshimiwa madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na wataalamu wote kwa ujumla.
Aidha Bi Mndeme alielekeza Halmashauri ya Msalala kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato, kuzingatia taratibu za manunuzi ya vifaa na mali mbalimbali za Halmashauri, Kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinapelekwa benki kwa wakati kabla ya kuzitumia na kuhakikisha maeneo yanayomilikiwa na Halmashauri yanakuwa na hati lengo ikiwa ni kuepusha hoja zisizo za lazima.
Awali akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (C.A.G) kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mweka hazina wa Halmashauri Bw. Gordon Dinda alibainisha kuwa hadi kufikia Juni 2022 Halmashauri ya Msalala ilikuwa na Hoja 59 ambapo mpaka sasa hoja 28 zimefungwa na hoja 31 zinaendelea kutekelezwa na kwamba kwa mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri hii imepata hati safi.
Akifunga mkutano huo wa Baraza la Madiwani Makamu mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Frola Clement Sagasaga alimshukuru Bi Mndeme kwa pongezi na maelekezo yake na kwamba wao k**a viongozi wa Halmashauri wataendelea kusimamia misingi ya uwajibikaji uwazi na usimamizi bora wa fedha za Halmashauri ili kuhakikisha Halmashauri inaendelea kupata hati safi. Mwisho alimuomba Bi Mndeme afikishe shukrani za wanamsalala kwa Rais Dkt Samia Suluhu kutokana na fedha nyingi za miradi alizozitoa kwenye Halmashauri hii.
21/06/2023
TANGAZO LA MKUTANO WA BARAZA LA MADIWANI.
idd_kassim_idd
05/06/2023
Baadhi ya picha za matukio katika maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani ambapo Halmashauri ya Msalala imefanya maadhimisho hayo katika viwanja vya Shule ya Msingi Kakola 'A' Kata ya Bulyanhulu.
11/03/2023
Afisa Utamaduni na Michezo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bw Emmanuel Paul ameongoza na kushiriki Bonanza la michezo la watumishi wa Serikali.
Bonanza hilo limefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Segese na kushirikisha watumishi wa kada tofauti tofauti kutoka ukanda wa Segese na ukanda wa Kakola.
Akizungumza katika Bonanza hilo Bw Paul amesema kuwa michezo hiyo ni maandalizi ya kuelekea Mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa serikali za Miitaa Tanzania (SHMISEMITA) ambayo yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu jijini Mwanza na akaongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala inajiandaa mapema ili kuhakikisha inaenda kung'ara katika mashindano hayo.
02/03/2023
KAMPUNI YA BARRICK KUPITIA MGODI WAKE WA BULYANHULU IMETENGA KIASI CHA TSH BILIONI 1.9 KWA AJILI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI MBALIMBALI YA KIMAENDELEO K**A SEHEMU YA KURUDISHA HISANI KWA JAMII (CSR) NDANI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA MSALALA KWA MWAKA 2023.
Hayo yamezungumzwa leo na Kaimu Meneja Mahusiano wa Mgodi huo Bi Zuwena Senkondo katika kikao cha Kamati ya maendeleo ya jamii kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri na Kuongozwa na Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Profesa Siza Tumbo.
Akitoa ufafanuzi juu ya mpango wa fedha hizo Bi Senkondo amesema kuwa Mgodi huo unaendelea kurudisha hisani kwa jamii kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ili kuleta tija kwa wananchi. "Kwa mwaka huu tunatarajia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati k**a vile mradi wa kilimo cha Korosho unaolenga kuongeza kipato kwa wananchi lakini pia kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri. Miradi hiyo itakuwa endelevu na hata ikitokea mgodi wetu unafungwa basi wananchi wataendelea kunufaika na miradi hiyo" alisema Bi Senkondo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya CSR kwa mwaka 2021 na 2022 Mratibu wa CSR Bw George Magembe alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili Halmashauri imetekeleza miradi mingi katika sekta ya Afya, Elimu, Maji na Uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kupitia fedha hizo na kwamba Sekta ya afya ndiyo ilipewa kipaumbele ambapo zahanati za vijiji18 zimejengwa na kukamilika huku pia baadhi ya vituo vya afya vikiongezewa huduma.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Prof Tumbo alielekeza kuwa Sekta ya elimu nayo lazima iangaliwe na kwamba kiasi cha fedha kitengwe kwa ajili kuongeza ufaulu wa wanafunzi mashuleni ikiwemo kuhakikisha wanapata chakula ili waweze kupata muda wa masomo ya ziada badala ya kurudi mapema majumbani. Mbali na maelekezo hayo Prof Tumbo aliwapongeza viongozi wa Halmashauri chini ya Mwenyekiti wake Mhe Mibako Mabubu kwa usimamizi mzuri wa miradi ya CSR.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Ndg Charles Fussi alimshukuru Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga kwa kufika kwake na kwamba maelekezo yote aliyoyatoa yeye na menejimenti nzima ya Halmashauri watahakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa ndani ya muda uliopangwa.
17/02/2023
TAREHE 17. 02. 2023
Mkataba wa ununuzi wa Mabomba yatakayotumika kwenye ujenzi wa Mradi wa maji wa Nduku - Busangi umesainiwa mapema leo Asubuhi.
Utiaji saini huo umefanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kahama na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mhe. Mibako Mabubu
Kukamilika kwa Ujenzi wa Mradi wa maji wa Nduku - Busangi itakuwa ni mwarobaini wa changamoto ya uhaba wa maji katika kata nyingi za Halmashauri ya Msalala na hivyo kuongeza wigo wa maendeleo hususani ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya kata hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala inaendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na serikali yake kwa ujumla kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Halmashauri hii.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano serikalini
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.