18/07/2026
WALIMU WA SHULE ZA SEKONDARI USHETU,WAPONGEZWA,WAPANGA MIKAKATI YA KUONDOA ZERO KATIKA MITIHANI YA TAIFA
USHETU DC
JULAI 18,2026
Walimu wote wa shule za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu leo wamekutana katika kikao maalum cha kutoa pongezi kwa shule na walimu waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, sambamba na kuweka mikakati mipya ya kuendelea kuinua kiwango cha elimu ndani ya halmashauri.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Amali Nyamilangano kiliongozwa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ambaye alikuwa mgeni rasmi. Pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, Afisa Elimu wa Mkoa, Afisa Elimu wa Halmashauri pamoja na viongozi na wadau mbalimbali wa elimu.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwapongeza walimu na shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita, pamoja na kujadili mikakati itakayosaidia kuongeza ufaulu na kuboresha zaidi sekta ya elimu katika shule zote za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, alisema halmashauri imejipanga kuhakikisha inaondoa kabisa matokeo ya sifuri (Zero) katika shule zote za sekondari. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu, viongozi wa shule na kubadilishana uzoefu kati ya shule ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kusambaza huduma ya umeme katika taasisi za umma, ikiwemo shule. Alieleza kuwa hadi sasa zimebaki shule nne pekee ndani ya Halmashauri ambazo bado hazijapatiwa umeme.
Katika kikao hicho, Meneja wa TANESCO aliyeshiriki aliwahakikishia washiriki kuwa Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kupeleka umeme katika shule tatu kati ya hizo, huku akiahidi kuwasilisha maombi ili shule moja iliyobaki nayo ipatiwe huduma hiyo.
Kikao kilihitimishwa kwa zoezi la utoaji wa vyeti na zawadi kwa walimu pamoja na shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya mwaka 2025 na 2026, ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi zao na kuhamasisha ari ya kufanya vizuri zaidi.

18/07/2026
17/07/2026
17/07/2026