04/05/2026
HOJA YA KUHALALISHA MIRUNGI YAZUA MJADALA MKALI.
🌠🌠🌠🌠🌠🌠🌠
=================
Kauli ya Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Mariam Ditopile, ya kutaka kilimo cha mirungi ihalalishwe imeibua upinzani mkali kila kona, huku Ansaar Muslim Youth Centre (AMYC ikiitaja kuwa hatari kwa mustakabali wa taifa.
=================
Mbunge Ditopile alitoa pendekezo hilo Aprili 29, 2026 bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya kilimo, akidai mirungi inaweza kuongeza mapato ya taifa na kuwasaidia wakulima, huku akihoji msingi wa kisheria ulioifanya iwekwe katika kundi la dawa za kulevya.
Hata hivyo, AMYC wamesema hoja hiyo “si tu dhaifu kitaalamu, bali ni hatari kwa mustakabali wa taifa,” wakisisitiza kuwa kuhalalisha mirungi kunapingana moja kwa moja na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015.
Katika tamko lao refu na la kina kupinga hoja hiyo, AMYC wamesema “kuhalalisha mirungi kutasababisha kudhoofisha mamlaka ya sheria, kudharau juhudi za kitaifa za kupambana na dawa za kulevya, na kufungua mlango wa uhalifu na mmomonyoko wa maadili.”
Kuhusu hoja ya mapato, AMYC wameeleza kuwa ni “upotoshaji mkubwa” kudai mirungi inaweza kuleta maendeleo, wakionya kuwa faida za muda mfupi haziwezi kufidia madhara ya muda mrefu k**a gharama za matibabu ya uraibu, kupungua kwa nguvu kazi, pamoja na kuongezeka kwa umaskini na uhalifu.”
Aidha,wamekumbusha wajibu wa Serikali kulinda ustawi wa wananchi:
“Serikali ina wajibu wa kulinda afya na maadili ya jamii, si kukusanya mapato kwa gharama ya maisha ya wananchi.”
Wameongeza kuwa mirungi “hulewesha akili, husababisha utegemezi na hupunguza tija,” hivyo kuhalalishwa kwake ni “sawa na kuhalalisha uharibifu wa kizazi cha vijana.”
Kwa mtazamo wa kidini, taasisi hiyo imenukuu hadithi ya Mtume (rehema na amani zimshukie): “Kila kinacholewesha ni haramu,” na kufafanua kuwa wanzuoni wameweka wazi kuwa kila kinachoathiri akili, iwe ni kinywaji au kitu kingine, kinaingia katika hukumu hiyo.
AMYC pia wamegusia maslahi ya umma, wakisema: “Maslahi ya jamii yanapaswa kutangulizwa kuliko faida za kifedha,” wakionya kuwa kuhalalisha mirungi ni “kuweka fedha mbele ya utu wa binadamu.”
Katika ngazi ya kimataifa, wameeleza kuwa hatua hiyo inaweza kuiweka Tanzania katika mgongano na mikataba ya kudhibiti dawa za kulevya, na kuharibu taswira ya nchi.
Kwa msimamo wao wa mwisho, AMYC wamesisitiza: “Kuhalalisha mirungi si sera ya maendeleo — ni sera ya maangamizi,” huku wakiiomba Serikali ikatae pendekezo hilo na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Kauli hiyo inaongeza uzito wa mjadala
unaoendelea nchini kuhusu mustakabali wa zao la mirungi na athari zake kwa jamii.
Ukiacha tamko la AMYC, wadau wengi wametoa maoni mitandaoni kupinga vikali maoni ya mbunge huyo, wakiyataja k**a yamepotoka na baadhi wakisema mirungi itaongeza ulevi na kuliingiza taifa katika anguko zaidi la kimaadili.
Mwanamke mmoja, mkazi wa Chanika, anayeishi na mume mtumiaji wa mirungi, ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe amesema maoni ya mbunge, mwanamke mwenzao, yamemshtua mno.
Akifafanua alisema ndoa yake inatetereka kwa sababu ya ulevi wa mumewe wa mirungi na asingependa wanawake wengine wapitie shida anazopitia.
Alisema ukiacha madhara mengi ya kiafya anayopitia mumewe, uraibu umesababisha pesa zote kuishia kwenye matumizi ya mirungi.
Huko Kenya, wadau nao wametoa maoni wengi wakiisikitikia Tanzania kutamani mirungu ihalalishwe ilhali wao nao wanatamani ingeharamishwa nchini kwao.
Watangazaji wa radio maarufu ya 47 Alex Mwakideu na Captain Emmanuel Mwashumbe katika kipindi chao cha asubuhi wameonya Watanzania kuwa mirungi ina madhara mengi na ni bora iendelee kupigwa marufuku.
=================
CHANZO:
IMAAN: ISSN 5618 - NO. 582 (Mei 4, 2026)
=================
"Maarifa Kwa Wote"

01/05/2026
01/05/2026
16/04/2026
18/02/2026
08/02/2026
11/01/2026