01/06/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe. Desderius Haule wamepokea vitenge kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Rizex For Life, Dkt. Riziki Nkya, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono na kuhamasisha viongozi na watumishi kushiriki katika Mtoko wa Familia unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Julai,2026 katika ukumbi wa Songea Klabu, Songea Mjini.
Akizungumza leo, tarehe 01Juni, 2026 Dkt. Riziki Nkya amebainisha kuwa lengo la Mtoko wa Familia ni kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Aidha, Dkt. Riziki ameeleza kuwa katika mtoko huo washiriki watapata kadi kwa gharama nafuu pamoja na vitenge. Alifafanua kuwa mtu mmoja (Single) atapata kadi kwa shilingi 70,000/=, Maalum ( V.I.P) shilingi 150,000/=, mume na mke (Couple) 170,000/=, meza ya watu kumi(10) shilingi milioni moja tu.
" Siku hiyo itapambwa na wanamuziki maarufu, MC mahiri na washiriki watapata mada motomoto kuhusu familia na burudani mbalimbali zitakuwepo." Aliongeza Dkt. Riziki.
01/06/2026
Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura alipotembelewa ofisini kwake leo tarehe 01 Juni, 2026 na wanafunzi wawili Laura K. Dalum na Line Johansen raia wa kigeni kutoka chuo cha Aarhus - Ujerumani.
Laura na Line wamefika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa lengo la kutembelea vituo vya afya kujifunza namna huduma za chanjo zinavyotolewa kwa makundi lengwa ikiwemo watoto wadogo.
Aidha, Mkurugenzi Kashushura amebainisha kuwa Laura na Line kufika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni udhihirisho wa umoja na ushirikiano wa Kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na mataifa mengine.
" Nchi yetu inazidi kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine, katika Halmashauri ya Mbinga tunaendeleza ushirikiano huo kwa kupokea wageni ambapo tutabalishana uzoefu katika mambo mbalimbali. K**a ambavyo Laura na Line wametoka Ujerumani kuja kujifunza tunavyotoa huduma za afya hususani Chanjo." Alieleza Kashushura.
Naye Mratibu wa huduma za Chanjo, ndugu George Machumu ameeleza kuwa kila mwaka Halmashauri imapokea marafiki kutoka nchi mbalimbali wanaofika kujifunza kuhusu huduma za chanjo.
Laura na Line wamefurahishwa namna ambavyo Serikali ya Tanzania na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wanavyoratibu huduma za Chanjo.
30/05/2026
VIJANA, WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO YA HALMASHAURI.
Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia kumi(10) inayotolewa na Halmashauri, kwani Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwezesha makundi yote katika jamii kujikwamua kiuchumi.
Hamasa hiyo imetolewa leo tarehe 30 Mei, 2026 na Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii ndugu Sapensia Mugarula kwenye kipindi cha Mbinga Yetu kinachorushwa hewani saa tatu asubuhi hadi saa nne katika Redio Hekima alipofika kuelezea jamii kuhusu fursa za mikopo na mambo mengine yanayohusu maendeleo ya jamii.
Sapensia Mugarula, alieleza kuwa Mbinga DC imetoa zaidi bilion 6 na vikundi vipatavyo 400 vimenufaika. Aliongeza kuwa mwitikio umeongezeka baada ya Serikali kufanyia marekebisho sheria ambapo kikundi cha watu watano (5) kila mtu anaweza kuwa na mradi wake na wakapata mkopo dhamana yao ni kikundi.
Sapensia alibainisha kuwa kwa sasa utaratibu wa kufuatilia mkopo unaanzia ngazi ya Kata ambapo walengwa watapewa mafunzo kisha kujaza taarifa zao kwenye mfumo wa wezesha ndipo K**ati zitafuatilia kikundi kujiridhisha kisha kupatiwa mkopo.
Aidha, Sapensia aliongeza kuwa mikopo imegawanyika katika makundi matatu, mikopo ya kiwango cha chini huanzia 500,000, kiwango cha kati huanzia milioni 10, na kiwango cha juu huanzia milioni 50 hadi 150 ambapo walengwa huchukua mkopo kwa ajili ya uwekezaji, akitolea mfano kikundi cha Vijana Kata ya Nyoni walipatiwa zaidi ya milioni 100 ambazo wamewekeza katika ujenzi wa nyumba ya kulala wageni (Guest House).
Sapensia alisisitiza kuwa mkopo si hisani hivyo kila anayekopa anatakiwa kuzingatia marejesho kwa kuheshimu fedha ya Serikali huduma iweze kuwafikia wengi zaidi.
29/05/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura anawatangazia wananchi wa maeneo ya Mkako na Kigonsera kuwa tarehe 30 Mei, 2026 ni siku ya usafi.
Mkurugenzi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao kufanya usafi wa mazingira.
29/05/2026
WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI WAHIMIZWA KULIPA MICHANGO YA UDHIBITI UBORA
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Ndugu Andrew Mbunda, amewahimiza Wakuu wa Shule za Sekondari kulipa michango ya Udhibiti Ubora ili kuiwezesha Ofisi ya Mdhibiti Ubora kutekeleza majukumu yake bila vikwazo.
Wito huo ameutoa leo tarehe 29 Mei, 2026 wakati akizungumza kwenye kikao kazi maalum kilichowakutanisha viongozi wa elimu na wakuu wa shule katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri, kilicholenga kukumbushana mambo muhimu yanayohusu maendeleo ya elimu ikiwemo kuongeza kasi ya kusimamia taaluma ili kuinua kiwango cha kujifunza na ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Aidha, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Mwalimu Abdallah Bundala alisisitiza kuwa jukumu la kwanza na la msingi la mkuu wa shule ni kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanakuwa bora, na kwamba hakuna muda wa kupoteza kwani ushindani wa kimkoa na kitaifa unaitaka Mbinga DC kuwa kileleni.
Bundala aliongeza kuwa wakuu wa shule wanapaswa kusimamia miradi ya maendeleo katika shule zao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi ya elimu ya kujitegemea inaleta matokeo tarajiwa hususani mradi wa mashamba ya kahawa, ufugaji wa ng'ombe na mabwawa ya samaki kwa shule zilizowezeshwa na ofisi ya Mkurugenzi.
Wakuu hao walisisitizwa katika matumizi ya mifumo ya elimu k**a Mfumo wa Taarifa za Shule ( School Information System) bila kusahau PEPMIS ambapo wametakiwa kusimamia taarifa zote zinazojazwa kwenye mifumo ziwe sahihi kulingana na utekelezaji wa majukumu husika.
Pia, Wakuu wa shule walikumbushwa kukaa vikao na wazazi msimu huu wa mavuno kuwahamasisha kuchangia chakula shuleni kulingana na utaratibu wa Halmashauri wa Chakula Day.
29/05/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura anawatangazia wananchi wote kuwa kuanzia tarehe 01 Juni, 2026 kutakuwa na zoezi la kugawa matone ya vitamini A na dawa za minyoo kwa watoto kuanzia umri wa miezi sita (6) na kuendelea.
Huduma hizi zitatolewa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vililivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Mkurugenzi ametoa wito kwa wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto kupata huduma ili kuimarisha afya zao.
28/05/2026
MBINGA DC YANG’ARA UMITASHUMTA: WANAFUNZI 9 WACHAGULIWA TIMU YA MKOA
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga (Mbinga DC) imeendeleza kishindo chake katika sekta ya michezo baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa, ambapo jumla ya wanafunzi tisa (9) wamefanikiwa kuchaguliwa kuwakilisha timu ya Mkoa wa Ruvuma katika mashindano ya Taifa.
Alizungumza leo tarehe 28 Mei, 2026 katika viwanja vya Halmashauri Afisa Elimu Msingi na Awali, Mwalimu Patricia Mbigili alibainisha kuwa mafanikio hayo yamekuja baada ya mchujo mkali na ushindani wa hali ya juu uliohusisha halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma, huku vipaji kutoka Mbinga DC vikitawala katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, pete, wavu, na riadha.
Wanafunzi hao tisa waliochaguliwa wameonesha viwango vya hali ya juu vilivyowakosha makocha na jopo la uteuzi wa mkoa. Wanatarajiwa kuungana na wenzao kutoka halmashauri nyingine kuunda timu imara ya Mkoa wa Ruvuma itakayochuana katika ngazi ya Taifa.
"Hii ni fursa ya dhahabu kwa vijana wetu. Kuchaguliwa kwa wanafunzi tisa ni uthibitisho kuwa Mbinga DC kuna vipaji vya kufariji na tunajivunia kazi kubwa inayofanywa na walimu pamoja na idara ya michezo." Alieleza mwalimu Patricia Mbigili.
Aidha, Mwalimu Patricia Mbigili alibainisha kuwa kung'ara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kumechangiwa na kuanza mazoezi mapema kuanzia ngazi ya shule, kata, na tarafa kabla ya mashindano ya mkoa kuanza. Ushirikiano wa karibu kati ya Walimu wa Michezo (Wakuu wa Vituo) na Idara ya Elimu Msingi (Sanaa, Utamaduni na Michezo) uliosaidia kubaini na kulea vipaji sahihi, pamoja na hamasa ya wazazi katika kuunga mkono michezo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Andrew Mbunda amewapongeza wanafunzi wote walioshiriki na kuwataka wale waliobahatika kuingia timu ya mkoa kwenda kupambana kwa nidhamu, bidii, na uzalendo ili kuiletea sifa Mbinga DC na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Wazazi na walezi wameombwa kuendelea kuwapa ushirikiano watoto wao kwani michezo kwa sasa si burudani tu, bali ni ajira na sehemu ya kukuza taaluma na akili ya mwanafunzi.
27/05/2026
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori anawatakia wananchi wa Mbinga na Watanzania wote Sikukuu njema ya Idi Al- Adha.
Tusheherekee kwa amani na utulivu.
27/05/2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ndugu Joseph Kashushura anawatakia wananchi wa Mbinga na Watanzania wote Sikukuu njema ya Idi Al-Adha.
Tusheherekee kwa amani na utulivu.