30/05/2026
Menejimenti ya TCAA Yatembelea Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya CATC
Menejimenti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Jabiri K. Bakari, imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Majengo ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) uliopo njia panda ya Banana jijini Dar es Salaam, Mei 30, 2026.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Ziara hiyo pia ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Mamlaka kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Bakari alisema uongozi wa TCAA unaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kimataifa.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya Chuo cha CATC kutakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza rasilimali watu wenye ujuzi wa kitaalamu katika sekta ya anga sambamba na kupunguza utegemezi wa mafunzo ya nje ya nchi.
"Mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Hakikisheni kuwa utekelezaji wake unazingatia ubora, ratiba na viwango vya kimataifa," amesema Dkt. Bakari.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka TCAA Mhandisi Stephen Mwakasasa alisema ujenzi unaendelea kulingana na michoro na usanifu uliokubaliwa huku usimamizi wa karibu ukiendelea kufanyika ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa.
Ziara hiyo pia iliwezesha Menejimenti ya TCAA kupata maelezo kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, changamoto zilizopo na mikakati ya kuendelea kuboresha utekelezaji wake hadi kukamilika.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kunatarajiwa kuongeza uwezo wa taifa katika kutoa mafunzo ya kitaalamu ya anga na kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa na kampuni ya CRJE kutoka nchini China.
27/05/2026
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama na Ulinzi wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA), Mei 26, 2026 ilifungua warsha ya kikanda kuhusu Ubora wa Ndege na Uthibitisho wa Watoa Huduma za Ndege yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa usalama wa anga na uzingatiaji wa kanuni za usafiri wa anga katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Warsha hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam imewakutanisha wadhibiti wa usafiri wa anga, wakaguzi, wataalamu wa kiufundi pamoja na wadau wa sekta hiyo kutoka ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kuoanisha mifumo ya usimamizi na kuimarisha uwezo wa kiufundi katika masuala ya usalama wa anga na utoaji wa vyeti.
Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri K. Bakari, Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usalama wa Anga, Mhandisi Furaha Sanga, alisema kuwa ubora wa ndege pamoja na uthibitisho wa watoa huduma za ndege ni nguzo muhimu katika kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama, wenye ufanisi na endelevu. Alisema ukuaji wa sekta ya anga unaochochewa na ongezeko la safari za ndege pamoja na maendeleo ya teknolojia unahitaji wataalamu kuendelea kujengewa uwezo na mifumo ya usimamizi kuimarishwa.
Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi wa CASSOA, Bw. Paul Lukanga, alisema kuwa eneo la ubora wa ndege ni moja ya maeneo muhimu zaidi katika usimamizi wa usalama wa anga. Alieleza kuwa sekta nyingine zikiwemo huduma za uongozaji ndege na mifumo ya usalama wa anga husaidia na kuunga mkono shughuli za ubora wa ndege katika kuhakikisha usalama na ufanisi wa safari za anga.
Bw. Lukanga aliwahimiza washiriki kushiriki kikamilifu katika mijadala na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa usalama wa anga. Pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango na miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO SARPs) kwa ajili ya kuhakikisha usafiri wa anga unabaki kuwa salama na wa kuaminika ndani ya ukanda huo.
24/05/2026
Mei 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, alifanya ziara ya kikazi katika kituo cha TCAA kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo alitembelea maeneo mbalimbali muhimu ya kiutendaji ikiwemo Mnara wa Kuongozea Ndege, Kituo cha Udhibiti wa Anga, vitengo vya uhandisi, maeneo ya rada pamoja na miundombinu mingine muhimu inayosaidia usalama wa anga na huduma za uongozaji ndege.
Katika ziara hiyo pia alipata nafasi ya kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa kituo hicho k**a sehemu ya juhudi za kuimarisha mshik**ano wa taasisi, ubora wa utendaji kazi na utoaji huduma ndani ya TCAA nchini kote.
Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti ya TCAA >>www.tcaa.go.tz/
20/05/2026
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA amefanya kikao na Wadau wa Sekta ya Anga
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, tarehe 19 Mei 2026 alifanya vikao vya mashauriano na wadau wa sekta ya anga katika Makao Makuu ya TCAA yaliyopo Banana, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Vikao hivyo vilifanyika katika vipindi viwili tofauti ambapo kikao cha asubuhi kilihusisha wamiliki na waendeshaji wa mashirika ya Ndege ya ndani, huku kikao cha mchana kikihusisha wamiliki na waendeshaji wa mashirika ya Ndege kutoka nje yanayokuja na kufanya shughuli zao nchini Tanzania.
Vikao hivyo vilitoa fursa kwa wadau kufanya majadiliano ya wazi na ya kujenga na uongozi wa TCAA, ambapo walitoa maoni, uzoefu na kueleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya anga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa vikao hivyo, Dkt. Bakari alijitambulisha rasmi kwa wadau na kusisitiza dhamira yake pamoja na menejimenti ya TCAA kuhakikisha sekta ya anga nchini inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kukua zaidi.
Alieleza kuwa TCAA itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa sekta hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha maendeleo ya sekta ya anga nchini.
Dkt. Bakari pia aliwaeleza wadau kuwa TCAA ipo katika mchakato wa kuboresha na kuoanisha mifumo yake ili kurahisisha michakato ya biashara na kuongeza ufanisi wa huduma. Aliwataka wadau kuwa tayari kuunga mkono maboresho hayo pindi yatakapohitajika.
Aidha alitangaza kuwa TCAA inapanga kuanzisha namba maalum ya bure ya simu pamoja na dawati maalum la huduma kwa Wateja ili kurahisisha mawasiliano na kushughulikia changamoto zao kwa haraka zaidi.
Katika majadiliano hayo, wadau waliwasilisha mapendekezo, maoni pamoja na changamoto mbalimbali zinazoathiri shughuli za sekta ya anga. Akijibu hoja hizo, Dkt. Bakari aliwahakikishia wadau kuwa TCAA imepokea na kuzingatia masuala yote yaliyowasilishwa na kwamba menejimenti ya mamlaka hiyo itashirikiana kwa karibu na wadau kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi stahiki kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta ya anga nchini Tanzania.
Vikao hivyo Vya ushirikishwaji wa Wadau vinaendelea.