Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA

Share

MTENDAJI MKUU,
MAJENGO YA VETERINARI,
131 BARABARA YA NELSON MANDELA,
S.L.P 9254, DAR ES SALAAM. SIMU Na. +255 22286152
Barua: Pepe.

Mission
To enhance sustainable livestock productivity, food safety through provision of cost effective quality veterinary diagnostic and analytical services, production and marketing of veterinary products and conducting research on animal diseases. [email protected],
Tovuti: www.tvla.go.tz

01/05/2026

Heri ya siku ya Wafanyakazi Duniani

Photos from Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA's post 30/04/2026

Wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mwelekeo wa taasisi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 uliokuwa ukiwasilishwa na Mtendaji Mkuu, Stella Bitanyi, wakati wa kikao hicho kilichofanyika Aprili 28, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa TVLA, Temeke jijini Dar es Salaam.

30/04/2026

Kaimu Meneja wa Mipango, Masoko na Habari wa TVLA, Bw. Prosper Haule, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na rasimu ya mpango na bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TVLA kilichofanyika Aprili 28, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa TVLA, Temeke jijini Dar es Salaam.

30/04/2026

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, akitoa mwelekeo wa Wakala kwa mwaka wa fedha 2026/2027, wakati akiongoza kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TVLA kilichofanyika Aprili 28, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa TVLA uliopo Temeke jijini Dar es Salaam.

30/04/2026

WATUMISHI TVLA WATAKIWA KUONGEZA BIDII NA UBUNIFU

Na Daudi Nyingo

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, amewataka watumishi wa TVLA kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kuendeleza mafanikio yaliyopo, akisisitiza kuwa maendeleo ya TVLA yanategemea uwajibikaji wa kila mtumishi pamoja na kujivunia nafasi zao ndani ya taasisi.

Dkt. Bitanyi alitoa kauli hiyo Aprili 28, 2026, wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TVLA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TVLA, Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema TVLA imejipanga kuimarisha mazingira ya kazi ili kuongeza tija, akibainisha kuwa tayari kila kituo kimepatiwa gari jipya kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu, huku mipango ikiendelea ya kuboresha maabara ili ziendane na teknolojia ya kisasa.

“Ni muhimu kila mtumishi kuwa na nidhamu na bidii ya kazi, na kuhakikisha anaiwakilisha vyema TVLA popote anapokuwa. Sote tunapaswa kutambua kuwa hii ni taasisi kubwa yenye mchango wa moja kwa moja katika ustawi wa sekta ya mifugo na uchumi wa Taifa. Hivyo, kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo, TVLA itasonga mbele kwa kasi zaidi,” alisema Dkt. Bitanyi.

Sambamba na hilo, aliwataka watumishi kujikita katika tafiti za kisayansi, hususan katika shughuli za maabara, akieleza kuwa tafiti ni chachu ya ubunifu na msingi wa utoaji wa huduma bora.

Katika hatua nyingine, Dkt. Bitanyi alisema TVLA ina mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa chanjo za mifugo ili kukidhi mahitaji ya ndani na hata soko la kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa taasisi katika maendeleo ya sekta ya mifugo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na rasimu ya bajeti ya 2026/2027, Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mipango, Masoko na Habari, Bw. Prosper Haule, alisema kuwa hadi kufikia Machi 2026, TVLA imezalisha dozi milioni 107.59 za chanjo za mifugo.

Sambamba na hilo TVLA inaendelea na ujenzi wa kituo cha kanda ya kati mkoani Dodoma, pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri kwa kununua magari matatu. Aidha, imekarabati nyumba za watumishi katika vituo vya Tanga na Mwanza, huku ikiendeleza shamba la mifugo la Mivumoni Tanga na kuimarisha shughuli za utafiti pamoja na ununuzi wa vifaa vya maabara.

Kuhusu rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, alisema vipaumbele ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa chanjo, kuendelea na ujenzi wa maabara, pamoja na kujenga ukuta kuzunguka Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha.

Vipaumbele vingine ni kuendelea na ujenzi wa kituo cha TVLA kanda ya kati Dodoma, ukarabati wa Maabara Kuu ya Mifugo (CVL), ununuzi wa magari mawili, pamoja na upatikanaji wa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa maabara na ofisi katika kituo cha Kigoma.

Wakizungumza katika kikao hicho, viongozi wa TUGHE akiwemo Mwakilishi wa TUGHE Taifa, Bw. Haruna Migeyo, Mjumbe wa Baraza Kuu TUGHE Serikalini, Bw. Benjamin Bikulamchi, pamoja na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Jamila Semang'anda waliupongeza uongozi wa TVLA kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake.

Walisema mafanikio hayo yanaakisi utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinazojikita katika Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa.

MWISHO

30/04/2026

Afisa Masoko wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Fihiri Mbawala, akitoa ufafanuzi kwa Bi. Rauhya Omary, muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo la Manispaa ya Lindi, tarehe 22 Aprili 2026, kuhusu mbinu bora za kuhakikisha mazingira ya uhifadhi wa chanjo yanazingatia viwango vinavyotakiwa ili kudumisha ubora na ufanisi wake, wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zilizofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara.

30/04/2026

Afisa Habari wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Daudi Nyingo (kulia), akitoa elimu kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Hilda Nkole wa Manispaa ya Lindi, tarehe 22 Aprili 2026, kuhusu matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA, wakati wa ziara ya utoaji elimu iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.

30/04/2026

Afisa Habari wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Daudi Nyingo, akitoa elimu kwa Bi. Matrona Mbilinyi, muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo lililopo Halmashauri ya Mji wa Masasi, tarehe 21 Aprili 2026, kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa wafugaji juu ya matumizi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo iliyofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.

30/04/2026

Daktari Mtafiti Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Deogratus Kavishe, akitoa maelezo kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Beatrice Hinju wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara, tarehe 20 Aprili 2026, kuhusu matumizi sahihi ya chanjo na tahadhari muhimu za kuzingatia ili kuhakikisha ufanisi wake kwa afya ya mifugo, wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zilizofanyika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.

30/04/2026

Afisa Masoko wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Fihiri Mbawala, akitoa elimu kwa muuzaji wa duka la pembejeo za mifugo, Bi. Zakia Amri wa Manispaa ya Mtwara, tarehe 20 Aprili 2026, kuhusu umuhimu wa uhifadhi sahihi wa chanjo wakati wa ziara ya utoaji elimu ya matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026.

Photos from Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania-TVLA's post 30/04/2026

TVLA Yatoa Elimu kwa Wauzaji wa Chanjo za Mifugo Kusini mwa Tanzania

Na Daudi Nyingo

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kupitia Sehemu ya Mipango, Masoko na Habari, imeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya chanjo za mifugo inazozizalisha kwa kufanya ziara maalum katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026 ikiongozwa na wataalamu wa TVLA, akiwemo Afisa Masoko, Bw. Fihiri Mbawala pamoja na Daktari wa Mifugo, Dkt. Deogratus Kavishe.

Katika kipindi hicho, jumla ya maduka 32 yanayouza chanjo zinazozalishwa na TVLA yalitembelewa katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mtwara, zikiwemo Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Masasi.

Aidha, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, ziara hiyo ilifanyika katika Manispaa ya Lindi pamoja na Halmashauri za Mtama na Nachingwea.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Mbawala alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhakikisha wauzaji wanakuwa na uelewa sahihi kuhusu matumizi ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kupata matokeo bora na salama.

“Tunatoa elimu kuhusu namna sahihi ya kuhifadhi chanjo, usafirishaji wake, matumizi sahihi pamoja na tahadhari muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kulinda ubora wa chanjo na afya ya mifugo,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Kavishe alisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaalamu katika matumizi ya chanjo, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza ufanisi wa chanjo au hata kuleta madhara kwa mifugo.

Baadhi ya wauzaji wa chanjo walioshiriki katika mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na juhudi hizo za TVLA. Bi. Zakia Amri, muuzaji wa pembejeo za mifugo katika Manispaa ya Mtwara, alisema elimu hiyo imewasaidia kuongeza uelewa wao na kuboresha huduma kwa wateja.

“Awali tulikuwa hatuna uelewa wa kina kuhusu uhifadhi sahihi wa chanjo, lakini sasa tumepata maarifa yatakayosaidia kulinda ubora wa bidhaa tunazouza,” alisema.

Naye Bw. Juma Mgeni kutoka Wilaya ya Nachingwea alibainisha kuwa mafunzo hayo yameongeza imani kwa wateja wao.

“Wafugaji wanapopata maelezo sahihi kutoka kwetu, wanaamini zaidi bidhaa hizi na kuona matokeo mazuri kwa mifugo yao,” alieleza.

Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa TVLA wa kuhakikisha chanjo zake zinatumika kwa ufanisi uliokusudiwa, sambamba na kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji nchini.

MWISHO

Want your business to be the top-listed Government Service in Dar es Salaam?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Address


Nelson Mandela Road, Veterinary Complex In The Ministry Of Livestock And Fisheries Compound
Dar Es Salaam