30/09/2026
HOSPITALI YA AMANA YASHIRIKIANA NA SEKRETARIETI YA MKOA KUWASAIDIA WALIOREJEA NCHINI KUTOKA AFRIKA KUSINI
Sekretarieti ya Mkoa ya Mkoa wa Dar es salaam kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana pamoja na maafisa ustawi wa jamii wametakiwa kuweka utaratibu wa kusikiliza na kufuatilia mahitaji ya kila mtanzania aliyerejea nchini kutoka Afrika Kusini kwa kathmini na kutambua mahitaji yake ya dharura, hali ya watoto wake, ujuzi alionao na kazi anayoweza kufanya ili kutafuta utaratibu mzuri wa kuwasaidia.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi Dkt. Gunini Kamba wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa katika hafla ya Uzinduzi wa Programu Maalum ya Huduma za Uchunguzi na Matibabu ya Meno, Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii kwa Watanzania waliorejea nchini kutoka Afrika ya Kusini iliyofanyika katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.
Ameongeza kuwa zaidi ya watu 40 miongoni mwa waliorejea tayari wametengenezewa meno bandia yatakayo wasaidia kurejesha uwezo wa kutafuna, kuzungumza kwa kujiamini,kurejesha tabasamu ambapo kunaweza kuwa mwanzo wa kupata tena matumaini na ujasiri wa kushiriki katika maisha ya jamii.
“Nimefurahi kuwa pamoja nanyi katika kukabidhi meno bandia na kuzindua huduma hii kwa watanzania wenzetu waliorejea kutoka Afrika Kusini, napenda kuanza kwa kuwaambia: karibu nyumbani Ninyi ni sehemu ya familia yetu, na mna nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu”amesema Dkt. Kamba
Aidha ametoa rai kwa Watanzania kuacha tabia ya kumuhukumu mtu kwa sura yake, hali ya meno yake au changamoto alizopitia badala yake kuwasikiliza na kuwapa nafasi ya kuanza tena.
Pamoja na hayo amewataka wataalam kuhakikisha kuwa kila mtu anayehitaji matibabu ya uraibu, huduma za afya ya akili au msaada wa ustawi wa jamii aunganishwe na huduma stahiki kwa heshima na usiri.
Kwa upande mwingine ameipongeza Hospitali ya Amana kwa kutambua mahitaji ya waliorejea na kuyafanyia kazi kupitia Rafiki wa Amana Foundation kwani Kuwapokea ni hatua ya kwanza na kuwasaidia kujenga maisha yao upya ni wajibu unaohitaji ushirikiano wetu sote.