07/10/2026
TANESCO MKOA KAGERA YATOA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKA SAMBAMBA NA ZAWADI YA MAJIKO KWA MAMA LISHE KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI HIYO
Na: Sadam Salai - Kagera
Ikiwa ni siku ya tatu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kaulimbiu “Extra Mile”, TANESCO Mkoa wa Kagera imepiga hatua zaidi baada ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa vitendo kwenye mgahawa wa mama lishe eneo la Bilele Manispaa ya Bukoba.
Mama Lishe huyo pamoja na wananchi wa eneo hilo la jirani walipata fursa ya kujua faida za matumizi ya nishati hiyo baada ya maafisa kutoka TANESCO kutoa elimu hiyo mubashara na kujifunza namna teknolojia hiyo inavyoweza kurahisisha shughuli za mapishi, kuokoa muda na kuongeza usalama wakati wa kupika.
Wananchi waliohudhuria wameonesha kuvutiwa na teknolojia hiyo kutokana na faida zake, huku Mama Lishe wakipongeza TANESCO kwa kuwafikishia teknolojia inayoweza kurahisisha shughuli zao za kila siku.
Aidha, TANESCO imegawa majiko janja kwa baadhi ya Mama Lishe ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuchochea jamii kutumia teknolojia salama na rafiki katika shughuli za mapishi.