13/05/2026
Watumishi wa Divisheni ya Mashirika ya Umma NAOT Wakutana Kujadili Maboresho ya Ukaguzi
Naibu Mkaguzi Mkuu, Bw. Salhina Mkumba, amefungua kwa niaba ya CAG Kikao Kazi cha Divisheni ya Mashirika ya Umma kinachoanza leo Jumatano, Mei 13, 2026 jijini Dodoma.
Kikao kazi hicho kinalenga pamoja na masuala mengine mbalimbali kujadili utekelezaji wa Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha uliopita sambamba na maboresho ya Ukaguzi ujao lengo kuu likiwa ni kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi na kupanga utekelezaji wa maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ili kuboresha huduma za Ukaguzi kwa maslahi ya Taifa.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi walioshiriki kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi hicho ni pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Menenjimenti ya Rasilimaliwatu, Bw. Novati Mfalamagoha, Kaimu Afisa Masuuli, Bw. Aziz Dachi na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bi. Elieshi Saidimu.
Katika picha ni matukio mbalimbali ya ufunguzi wa kikao kazi hicho.
13/05/2026
CAG Ahimiza Wakaguzi Kuendelea Kujiongezea Ujuzi wa Taaluma ya Ukaguzi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles E. Kichere, amewataka Wakaguzi kuendelea kujijengea uelewa wa kina wa viwango vya taaluma ya ukaguzi, mifumo ya ukaguzi na masuala mbalimbali ya kitaaluma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi.
CAG amesema uelewa huo utawasaidia Wakaguzi kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kazi za ukaguzi, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora za ukaguzi zinazokidhi viwango vinavyotarajiwa.
Mafunzo ya awamu ya pili Endelevu ya Kitaaluma (CPD) kwa Wakaguzi yamefanyika mapema wiki hii kwa kuandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kupitia Kituo chake cha Mafunzo (NAA) kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania na kuhusisha jumla ya watumishi 376 wa NAOT.
Awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilifanyika kwa njia ya mtandao na kuhudhuriwa na Wakaguzi 610. Mafunzo hayo yamefanyika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya mifumo ya taarifa katika ukaguzi wa fedha, utawala bora na nafasi ya mkaguzi, ukaguzi wa manunuzi ya umma, maadili na mwenendo wa kitaaluma.
Katika picha ni matukio ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
05/05/2026
OFISI YA TAIFA YA UKAGUZI YAIBUKA NA VIKOMBE VIWILI KWENYE MICHEZO YA MEI MOSI 2026
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imeendelea kudhihirisha kuwa si mahiri tu katika majukumu ya ukaguzi, bali pia katika shughuli za michezo, mara baada ya kushiriki na kupata zawadi ya vikombe viwili katika mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Njombe kuanzia tarehe 13 hadi 30 Aprili 2026.
Jumla ya Taasisi 47 zilishiriki katika mashindano hayo yaliyohitimishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake ya Mei Mosi kwa Watumishi wa Umma ambapo NAOT ilishiriki kikamilifu ikiwa na Wachezaji 45, ambao walishiriki kwenye michezo tofauti ambayo ni pamoja na mpira wa miguu, netiboli, riadha, “draft”, “darts”, kurusha tufe, “pool table” na mchezo wa bao.
Katika michezo hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, NAOT iliweza kuibuka na ushindi wa vikombe viwili, ambapo ilishika nafasi ya pili katika mchezo wa kurusha tufe kwa wanawake kupitia mshiriki Bi. Furaha Kaboneka. Aidha, katika riadha mbio za mita 100 kwa Wanawake, Bi. Furaha Kaboneka alifanikiwa kupeperusha bendera ya NAOT kwa kuibuka mshindi wa tatu, mafanikio yaliyoiwezesha NAOT kujinyakulia vikombe hivyo viwili.
Akizungumzia mafanikio hayo kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu, Bw. Novati Mfalamagoha amesema, “Kwa niaba ya CAG nawapongeza sana Wanamichezo wote ambao wameipa heshima Ofisi, natoa wito kwa Waajiriwa wapya na wengine wote kujiunga na michezo lengo ni kuhakikisha tunaepuka magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni pamoja na shinikizo la damu na magonjwa mengine.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya NAOT, Bw. Benedict Sailes amesema, "Namshukuru CAG kwa kutuwezesha kushiriki kwenye michuano hii. Pia tunawashukuru wanamichezo wote kwa kujitoa kwao, Ofisi ya CEA Njombe na watumishi wake kwa kutupa “moral support”, pamoja na Viongozi wote wa “NAOT Sports Club” kwa ushirikiano wao mkubwa."
Katika picha ni matukio mbalimbali kuhusiana na tukio hilo.
01/05/2026
NAOT WAADHIMISHA SIKU YA WAFANYAKAZI DODOMA
Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) wameungana na Wafanyakazi wengine nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Maadhimisho ya Mei Mosi kila mwaka yanalenga kuimarisha mshikamano miongoni mwa Wafanyakazi, kuhimiza uwajibikaji na uadilifu kazini, pamoja na kutambua mchango wa Wafanyakazi katika ustawi wa uchumi wa Taifa.
Kitaifa, Maadhimisho ya mwaka 2026 yamefanyika Mkoani Njombe. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Katika picha ni matukio mbalimbali kuhusiana na ushiriki wa Watumishi wa NAOT kwenye maadhimisho hayo. .tanzania
01/05/2026
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles E. Kichere anawatakia Wafanyakazi wote Heri ya Sikukuu ya Mei Mosi 2026.
Kaulimbiu: "Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050."