29/07/2025
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA CLYDE &CO AFRIKA KUSHIRIKIANA KUWANOA MAWAKILI
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka kampuni ya Kimataifa ya uwakili ya Clyde & Co Afrika kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kufungua fursa ya mafunzo kwa Mawakili wa Serikali.
Naibu Mwanasheria Mkuu amekutana na ujumbe huo tarehe 25 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba Jijini, Dodoma.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi hiyo kwenye eneo la mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kurahisishia utendaji kazi.
Aidha, amesema kuwa wanatarajia taasisi hiyo kutoa mafunzo na ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya Sheria ikiwa ni pamoja na masuala ya Usuluhishi wa migogoro ya kimataifa, Sheria za mikataba ya kimataifa na masoko ya mitaji, sheria za Biashara na uwekezaji, Sheria za Miradi na Ujenzi, Sheria za Miundombinu, Sheria zinazosimamia Bandari, Viwanja vya Ndege na Reli, Masuala ya Nishati, Sheria za Madini, Sheria za mabenki na taasisi za Fedha, Akili mnemba/unde, usimamizi wa mikataba/miradi, maktaba mtandao (e-library) pamoja na fursa za kushikishwa (attachment).
“Tuko tayari kushirikiana nanyi katika maeneo haya ya mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Clyde & Co Afrika Bw. Peter Kasanda ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha na mafunzo kwenye masuala yote ambayo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapendelea kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali.
“Sisi tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi hii kubwa ya kisheria, amesema kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana nanyi katika masuala ya mafunzo ili kuweza kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
28/07/2025
HABARI PICHA
Ujumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno wamekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF Dkt. Rhimo Nyansaho na baadhi ya Wafanyakazi wa mfuko huo, mazungumzo baina ya Taasisi hizo yamelenga kubadilishana uzoefu katika eneo la Huduma kwa Wateja.
Ujumbe huo umekutana na PSSSF tarehe 24 Julai, 2025 katika Makao Makuu ya Mfuko wa PSSSF Jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Leila Muhaji, Wakili wa Serikali Mkuu Dkt. Jaba Shedrack, Afisa TEHAMA Mwandamizi Bw. Juma Mziray na Wakili wa Serikali Bw. Nyamhanga Nyamhanga.
27/07/2025
*HABARI PICHA*
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameshiriki mbio za marathon zijulikanazo k**a NBC Dodoma Marathon 2025".
Watumishi hao wameshiriki katika mbio za kilomita 10 zilizofanyika tarehe 27 Julai, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara baada ya kukamiliza mbio hizo, Bw. Nicolaus Sitta, ameushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwawezesha watumishi kushiriki katika mbio hizo.
"Tunawashukuru Viongozi wetu kwa motisha hii ya kutuwezesha kushiriki katika mbio hizi na tunawapongeza kwa juhudi zao za kuhakikisha watumishi wanashiriki katika michezo."
NBC Marathon 2025 Dodoma imelenga katika kuimarisha mapambanao dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi, kuboresha afya ya mama na mtoto na kufadhili wauguzi 100 kwa ajili ya watoro wenye changamoto ya usonji.
26/07/2025
NBC WAIALIKA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KUSHIRIKI MBIO ZA NBC MARATHON DODOMA
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Taifa ya Biashara ( NBC) na kukabidhiwa jezi maalum kwa ajili ya mbio za marathon zijulikanazo k**a " NBC Dodoma Marathon 2025."
Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 24 Julai, 2025 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba jijini, Dodoma.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameipongeza Benki ya NBC kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za umma katika kuimarisha ustawi wa jamii kupitia matukio ya michezo.
"Nawapongeza sana NBC kwa kutuona na kutupatia vifaa hivi kwa ajili ya kushiriki katika marathon hii na tunawaahidi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itashiriki kikamilifu, pia mbio hizi ni njia ya kuonyesha mshik**ano na mchango wetu katika maendeleo ya jamii." Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya NBC, Bw. Elvis Ndunguru akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC amezungumzia lengo la marathon ya NBC kwa mwaka 2025 ni kuimarisha mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi, kuboresha afya ya mama na mtoto na kufadhili wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto ya usonji, pia ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali.
“NBC tunaahidi kuendeleza ushirikiano ulipo baina yetu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuwa ofisi hii ni mdau wetu mkubwa”. Amesema Bw. Ndunguru
Katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NBC aliambatana na Mkurugenzi wa GSM Foundation Bi. Faith Gugu pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa NBC Bw. Godwin Semunyu.
NBC Dodoma Marathon 2025 inatarajiwa kufanyika tarehe 27 Julai, 2025 kwa kuwakutanisha washiriki kutoka sekta mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wafanyabiashara, wanafunzi na wanamichezo huku sehemu ya mapato ya mbio hizo ikielekezwa katika kuboresha masuala ya Afya.
22/07/2025
*MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ASHIRIKI KIKAO CHA KIMATAIFA CHA SHERIA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI*
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameshiriki kikao cha 58 cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za Biashara na Uwekezaji kinachofanyika kwa siku 2 kuanzia tarehe 21 hadi 22 Julai, 2025 Jijini Vienna, Austria. Kikao hicho pamoja na mambo mengine kilijadili taratibu za Utatuzi wa Migogoro kati ya Wawekezaji na Serikali katika Mikataba ya Mataifa.
Kikao hicho pia kilijadili mageuzi yanayokusudiwa kufanywa katika Sheria za Kimataifa za biashara. Mageuzi yanayopendekezwa ni pamoja kuhakikisha Sheria za Biashara za Kimataifa zinajali maslahi ya mataifa yanayoendelea, Tozo na gharama zinazotolewa na Mabaraza ya Kimatifa zina uhalisia, Kuwepo kwa uwazi na ufanisi katika mwenendo wa Mashauri, na Kuwepo na uwezekano wa kukata rufaa kwenye maamuzi ya mabaraza ya Usuluhishi ya Kimataifa.
Kupitia kikao hicho Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuweka taratibu za kushughulikia malalamiko ya wawekezaji mapema kabla haijawa migogoro (Mechanisms for prevention of Disputes).
Aidha, Tanzania kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kuwa mstari wa mbele kuchochea mageuzi kwenye utatuzi wa migogoro ya uwekezaji, kwa kusisitiza uwepo wa njia mbadala za utatuzi wa migogoro ikiwemo kutumia njia za upatanishi (amicable settlement).
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametembelea Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania nchini Austria na kupokelewa na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Austria Bw. Gerald Mbwafu, ambapo amemshukuru kwa mapokezi mazuri na kufanikisha ujumbe wa Tanzania kuhudhuria kikao hicho.
17/07/2025
HABARI PICHA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaongoza Watanzania kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini, Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameungana na Viongozi mbalimbali wa Serikali kushiriki katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, hafla hiyo imehudhuriwa pia na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
14/07/2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Julai, 2025.
Pichani Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari, (wakwanza kulia waliokaa) ni miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho.
(Picha kwa hisani ya Ikulu)
14/07/2025
HABARI PICHA
Ujumbe kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno wamekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna na baadhi ya Wafanyakazi wa Benki hiyo, mazungumzo baina ya Taasisi hizo yamelenga kubadilishana uzoefu katika eneo la Huduma kwa Wateja.
Ujumbe huo umekutana na Benki hiyo tarehe 14 Julai, 2025 katika Makao Makuu ya Benki ya NMB Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimbatana na Mkurugenzi Msaidizi Uratibu Bw. Ipyana Mlilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Leila Muhaji, Afisa TEHAMA Mwandamizi Bw. Juma Mziray na Wakili wa Serikali Bw. Nyamhanga Nyamhanga.
13/07/2025
*WANANCHI WASIFU HUDUMA ZA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI SABASABA*
Wananchi mbalimbali waliotembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam, wametoa pongezi kwa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakieleza kuwa zimekuwa zikiwasaidia kuelewa masuala ya kisheria na kuwapatia msaada wa changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake Bw. Andrew Msanya akizungumzia huduma zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa uwepo wa huduma za ushauri wa kisheria, elimu ya sheria na utatuzi wa changamoto mbalimbali umekuwa msaada mkubwa kwao, hasa kwa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kupata huduma hizo kwa urahisi.
"Nimefika hapa kwenye banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nilikuwa na changamoto ya masuala ya ajira nimepata maelezo mazuri na msaada wa kitaalamu kabisa, nimeelekezwa hatua za kuchukua". Amesema Bw. Msanya.
Naye Bi. Suzan Abias ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa huduma za kisheria kwenye maonesho hayo kwani huduma hizo zitawasaidia wananchi wengi kufahamu haki zao.
"Nawashukuru Mawakili hawa kwa kutoa maelezo mazuri juu ya mambo ya kisheria, nawashauri wananchi wenzangu wenye changamoto za kisheria mje kwenye banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali msaidiwe". Amesema Bi Suzan
Wakili wa Serikali Mwandamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Eneza Msuya ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maonesho hayo ili wapate ushauri wa kisheria, elimu pamoja na utatuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili.
"Tunawakaribisha wananchi wote kwenye banda letu watumie fursa hii kupata huduma za ushauri wa kisheria, elimu ya sheria pia tunatatua na kushughulikia changamoto mbalimbali za kisheria, huduma hizi tunazitoa bila malipo." Amesema Bw. Msuya
Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali liko katika Hema la Jakaya Kikwete banda namba 24, Maonesho ya Sabasaba yaliyoanza tarehe 28 Juni, 2025 yanaendelea hadi Julai 13, 2025
11/07/2025
HABARI PICHA
Wakili wa Serikali mkoa wa Arusha , Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Veritas S. Mlay amemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari katika ufunguzi wa Kongamano la Watunga Sera na wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamiii Barani Afrika (Africa Social Security Association - ASSA)
Kongamano hilo linafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) na linalenga kujadili jinsi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inavyoweza kuchangia maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa uchumi Barani Afrika bila kuathiri Utoaji wa mafao kwa walengwa.
Aidha, Kongamano hilo linazikutanisha nchi 14 ambazo ni Wanachama wa ASSA zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, South Sudan, Comoros, Sierra Leone, Ivory Coast, Gambia na Mali.
Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Kongamano hilo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango.