14/05/2026
SERIKALI YAKAMILISHA UJENZI WA KITUO CHA UMAHIRI CHA KIKANDA CHA MAFUNZO YA NISHATI JADIDIFU
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri cha Mafunzo ya Nishati Jadidifu katika Kampasi ya Kikuletwa ya Chuo cha Ufundi Arusha, iliyopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati safi na maendeleo ya teknolojia nchini.
Kituo hicho kimejengwa na Serikali kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EASTRIP), ambapo kimewekewa miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yenye viwango vya kimataifa katika sekta ya nishati jadidifu.
Kupitia kituo hicho, vijana kutoka Tanzania na mataifa jirani wanatarajiwa kupata ujuzi wa teknolojia ya nishati safi na endelevu, jambo litakalosaidia kupunguza utegemezi wa mafuta, kuongeza ajira kwa vijana, pamoja na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali na kutoa mafunzo, kituo hicho kinatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda kwa kusaidia upatikanaji wa nishati nafuu na rafiki kwa mazingira, huku kikichangia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya nishati zisizo endelevu.
Ujenzi wa kituo hicho unatajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na mkakati wa kikanda wa kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kutumia nishati salama, endelevu na yenye kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
13/05/2026
Ni kuanzia saa 1:30 kamili asubuhi ndani ya 𝗠𝗼𝗿𝗻𝗶𝗻𝗴 𝗘𝘅𝗽𝗿𝗲𝘀𝘀 𝗨 𝗙𝗠 mada yetu inahusu 𝗨𝘁𝗲𝗸𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮𝗷𝗶 𝘄𝗮 𝗠𝗸𝗮𝗸𝗮𝘁𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝗶𝘀𝗮𝘆𝗮𝗻𝘀𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝘂𝗷𝗲𝗻𝗴𝗮 𝗨𝗺𝗮𝗵𝗶𝗿𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝘂𝘀𝗼𝗺𝗮, 𝗞𝘂𝗮𝗻𝗱𝗶𝗸𝗮 𝗻𝗮 𝗞𝘂𝗵𝗲𝘀𝗮𝗯𝘂 (𝗞𝗞𝗞)
12/05/2026
Miundombinu ya elimu wilayani Sengerema mkoani Mwanza inaendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya elimu inayofadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia Programu ya EP4R, Global Partnership for Education (GPE) hatua inayochochea ongezeko la ufaulu na ujuzi kwa wanafunzi pamoja na wananchi kwa ujumla.
Katika Shule ya Sekondari Savana, utekelezaji wa mradi wa EP4R umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na utengenezaji wa seti 80 za meza na viti, hatua hiyo imepunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza utulivu wa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Mkuu wa shule hiyo, Daniel J. Lutonja amesema maboresho hayo yameongeza hamasa kwa wanafunzi na walimu, huku yakichangia kuboresha matokeo ya kitaaluma kutokana na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
Kwa upande mwingine, Kituo cha Walimu Sima (TRC) kimeendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya taaluma baada ya ujenzi na ukarabati wa kituo hicho.
Dismas M. Mabele, Afisa Elimu Kata ya Sima ambaye pia ni msimamizi wa kituo hicho, ameeleza kuwa Kituo cha Walimu Sima TRC kimekuwa na manufaa makubwa yakiwemo kuboresha ujuzi wa walimu, kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kukuza ubunifu katika ufundishaji, kutoa ushauri wa kitaaluma katika maeneo yenye changamoto na hatimaye kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika kata tatu zinazohudumiwa ambazo ni Sima, Buzilasoga na Igulumuki.
Katika hatua nyingine, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Sengerema (FDC) kimefanyiwa ukarabati na ujenzi wa miundombinu k**a jengo la utawala, mabweni ya wavulana na wasichana, jengo la madarasa mawili , karakana ya ufundi magari, karakana ya umeme na useremala, jengo la ICT na Maktaba, karakana ya ushonaji na uungaji vyuma, jiko na bwalo, darasa la uashi, darasa la chekechea (daycare) pamoja na jengo la madarasa mawili likiwa na ofisi mbili na stoo.
12/05/2026
Usikose kuunaungana nasi katika kipindi cha Amka na Bomba ndani ya 104.1 MHz Bomba FM Mbeya, ni kuanzia saa 3:00 kamili asubuhi tunaangazia 𝗨𝘁𝗲𝗸𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮𝗷𝗶 𝘄𝗮 𝗠𝗸𝗮𝗸𝗮𝘁𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝗶𝘀𝗮𝘆𝗮𝗻𝘀𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝘂𝗷𝗲𝗻𝗴𝗮 𝗨𝗺𝗮𝗵𝗶𝗿𝗶 𝘄𝗮 𝗞𝘂𝘀𝗼𝗺𝗮, 𝗞𝘂𝗮𝗻𝗱𝗶𝗸𝗮 𝗻𝗮 𝗞𝘂𝗵𝗲𝘀𝗮𝗯𝘂 (𝗞𝗞𝗞)
12/05/2026
Ujenzi wa Kituo cha Umahiri Afrika Mashariki cha Sayansi ya Moyo Awamu ya Pili katika eneo la Kampasi ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam unaendelea kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kituo hicho kinajumuisha Ujenzi wa hospitali ya mafunzo, kutoa mafunzo ya kitaalamu, na kusaidia tafiti mbalimbali zinazohusu magonjwa ya moyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, Mei 12, 2026 jijini Dar es Salaam, amekutana na kufanya mazungumzo na Kamati tendaji ya Usimamizi na Uongozi wa mradi huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa kupitia mradi huo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinapaswa kuongeza mitaala itakayowezesha kupokea wanafunzi wa kutosha kutoka nchi za Afrika Mashariki, ili kuimarisha dhima ya kituo hicho k**a ngazi ya kikanda ya umahiri.
Aidha, Prof. Nombo ameeleza kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kufuatilia miradi yote chini yake ili kuhakikisha inaleta tija katika kutoa elimu bora na kupongeza fursa kwa Watanzania ili kuchochea maendeleo endelevu ya taifa kijamii na kiuchumi.
12/05/2026
GPE, EP4R WARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ELIMU BUSWELU
Ujumbe wa wadau wa maendeleo ya elimu ukiwemo Global Partnership for Education (GPE) pamoja na Education Program for Results (EP4R) ukiongozwa na Morten Sigsgaard Mratibu wa Ushirika wa Nchi (GPE) umeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu inayotekelezwa katika Shule ya Msingi na Sekondari Buswelu, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo Mei 11, 2026, Morten amesema miradi hiyo imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hususan kwa wanafunzi wa elimu jumuishi.
Katika Shule ya Msingi Buswelu, inayohudumia wanafunzi 1,211 wakiwemo 176 wenye mahitaji maalumu, imefanikiwa kujenga bweni la wasichana wenye mahitaji maalumu kupitia ufadhili wa Serikali na GPE-LANES II.
Mradi huo umewezesha wanafunzi 80 kupata makazi salama ya bweni, huku huduma za bweni zikianza rasmi Mei 8, 2026 baada ya Serikali kuanza kutoa fedha za chakula.
Aidha, walimu na wanafunzi wameeleza mabadiliko chanya yaliyotokana na miradi hiyo, wakisema awali wanafunzi walikuwa wakisoma katika mazingira ya msongamano wa madarasa, lakini sasa wanapata nafasi ya kusoma katika mazingira bora na yenye nafasi ya kutosha, jambo lililoongeza umakini na ushiriki darasani.
Katika Shule ya Sekondari Buswelu, kupitia Programu ya EP4R, shule imepokea Shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vyenye viti na meza 100, mradi ambao tayari umekamilika na unatumika.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema awali walikuwa wakisoma wakiwa wamebanana kutokana na upungufu wa madarasa, hali iliyokuwa ikichangia usumbufu wakati wa masomo, lakini kwa sasa wanafurahia kusoma katika madarasa mapya yenye nafasi kubwa na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Uongozi wa shule ulieleza kuwa miradi hiyo imechangia kuboresha ufaulu pamoja na kuongeza hamasa ya kujifunza.
Wadua wa maendeleo walitoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuboresha mazingira ya kujifunzia nchini.
11/05/2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ni ya kuridhisha.
Akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi na Uongozi cha mradi huo kilichofanyika jijini Dar es Salaam Mei 11, 2026, Prof. Nombo ameeleza kuwa shughuli zilizopangwa kutekelezwa zimefanyika kwa kiwango kikubwa na kwa mafanikio.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na kuweka mikakati thabiti ya utekekezaji, ushirikiano wa wasimamizi na watekelezaji pamoja na usimamizi thabiti wa k**ati tendaji.
Ametoa rai ya kuendeleza juhudi hizo ili mradi huo unapoenda kukamilika ulete matokeo endelevu kwa taifa.