02/06/2026
TIRA YAPANGA KUTOA ELIMU YA BIMA KWA WATU MILIONI 27 MWAKA 2026/27
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis M***a Omar amebainisha hilo leo Juni 2, 2026 wakati wa Uwasilishaji wa Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti wa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/2027 bungeni jijini Dodoma ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imepanga kuimarisha zaidi usimamizi na maendeleo ya sekta ya bima nchini katika mwaka wa fedha 2026/27 kupitia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo usajili wa watoa huduma za bima 2,536 na utoaji wa elimu ya bima kwa wananchi milioni 27 kupitia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano na programu za uhamasishaji zitakazotekelezwa nchini kote.
Aidha Waziri ameeleza TIRA imepanga kuendelea kuboresha Mfumo Jumuishi wa Udhibiti wa Bima (Insurance Regulatory Integrated System - IRIS) kwa kuongeza teknolojia ya uchambuzi wa takwimu (Predictive Analytics) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta na kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA na hivyo kuongeza huduma bora kwa wananchi.
Katika kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni za bima imeelezwa TIRA imejipangia kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa wasajiliwa wa bima 618 nchini, hatua inayolenga kuhakikisha utoaji wa huduma za bima unazingatia viwango na matakwa ya kisheria.
Vilevile, TIRA itafanya tafiti mbili kuhusu mwenendo wa soko la bima nchini ili kupata taarifa muhimu zitakazosaidia katika maboresho ya sera, kanuni na mikakati ya kukuza sekta ya bima. Utekelezaji wa mipango hiyo unatarajiwa kuongeza uwazi, kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima na kuchochea ukuaji wa matumizi ya huduma za bima kwa wananchi na wadau mbalimbali nchini
Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware na Naibu Kamishna Bi. Khadija I. Said pia wamehudhuria uwasilishwaji huo.
02/06/2026
Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/2027.
01/06/2026
Kesho, tarehe 02 Juni 2026, Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis M***a Omar atawasilisha Bungeni jijini Dodoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau wa sekta ya bima kufuatilia kwa karibu uwasilishaji huu muhimu, unaobeba mwelekeo wa uchumi wa Taifa na maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Tuungane kufuatilia kwa pamoja.
/27
31/05/2026
TIRA UNGUJA YAHIMIZA WELEDI NA UADILIFU KWA MAWAKALA WA BIMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kupitia Ofisi ya Kanda ya Unguja Zanzibar, imeshiriki mafunzo maalum ya bima kwa mawakala wa Kampuni ya bima ya Heritage ambayo yamefanyika visiwani humo tarehe 30 Mei 2026, na kusisitiza suala la weledi na uadilifu katika utoaji wa huduma za bima.
Katika mafunzo hayo, Meneja wa TIRA Kanda ya Unguja Bw. Said Salum ameshiriki k**a mgeni rasmi wa ufunguzi wa mafunzo ambapo amewahimiza mawakala kuendelea kuzingatia weledi, uadilifu na kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni za bima katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, ameshiriki katika zoezi la kukabidhi zawadi maalum kwa mawakala waliofanya vizuri zaidi kutoka upande wa Unguja na Pemba kwa kutambua mchango wao katika kukuza sekta ya bima.
Sambamba na hilo, TIRA kupitia Ofisi ya Kanda ya Unguja imepokea tuzo ya shukrani kutoka kwa waandaaji wa mafunzo hayo kwa kutambua ushirikiano na mchango wake katika kusaidia na kuwawezesha wadau wa sekta ya bima visiwani Zanzibar.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Meneja wa Kanda ya Unguja, kwa niaba ya TIRA. Tuzo hiyo ni uthibitisho wa jitihada zinazoendelea kufanywa na TIRA katika kusimamia, kuendeleza na kuimarisha sekta ya bima pamoja na kuhakikisha wadau wake wanapata usaidizi na mwongozo stahiki kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.
31/05/2026
Bado Siku 2 kuelekea Uwasilishaji wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha 2026/2027
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar atawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/2027, tarehe 02 Juni 2026 jijini Dodoma, Bungeni.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inaendelea kuwahimiza wananchi na wadau wa sekta ya bima kufuatilia uwasilishaji huu muhimu wenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Ungana nasi kufuatilia.
26/05/2026
Je, mtoa huduma za bima unayemtumia ana leseni hai?
Hakiki kupitia tiramis.tira.go.tz au tembelea www.tira.go.tz kuona orodha watoa Huduma wenye leseni hai na halali.
TIRA, Kwa Soko Salama la Bima.
24/05/2026
TIRA YAUNGANISHA SEKTA ZA BIMA NA AFYA
Hatimaye, wiki ya Uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Huduma za Bima ya Afya imehitimishwa leo Mei 24, 2026, katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ambapo uzinduzi rasmi wa jukwaa hilo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.
Uzinduzi wa Jukwaa la Kitaifa la Huduma za Bima ya Afya jijini Dar es Salaam umetajwa kuwa hatua muhimu katika kuendelea kutoa elimu kuhusu bima na huduma za afya kwa wananchi.
Akihutubia wananchi waliohudhuria jukwaa hilo, Mhe. Mtambule alisisitiza umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya, akieleza kuwa magonjwa hutokea katika nyakati zisizotarajiwa, hivyo uwepo wa bima ni njia muhimu ya kumlinda mwananchi dhidi ya majanga ya ghafla.
“Lengo kuu la sera ya bima ni kumlinda mtumiaji wa huduma dhidi ya majanga yasiyotarajiwa,” alisema Mtambule.
Kupitia jukwaa hilo, Meneja wa TIRA Kanda ya Mashariki, Ndugu Kurenje Mbura, alitangaza rasmi ushirikiano kati ya sekta ya bima na huduma za afya, huku akiwaomba wadau wa afya kuwa mabalozi wa elimu ya Bima ya Afya nchini Tanzania.
Aidha, Mbura alieleza majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika utekelezaji wa mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, ikiwemo usajili wa vituo vinavyotoa huduma hizo.
Jukwaa hilo la wadau wa bima linatarajiwa kuendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini baada ya uzinduzi wake rasmi kufanyika jijini Dar es Salaam.
23/05/2026
TIRA YATOA ELIMU YA BIMA YA AFYA KWA WOTE KATIKA JUKWAA LA BIMA NA AFYA DAR ES SALAAM
Wananchi wameendelea kutembelea banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika Jukwaa la Bima na Afya linalofanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 20 hadi 24 Mei 2026. Katika jukwaa hilo, TIRA k**a msimamizi wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake na umuhimu wa huduma za bima ya afya kupitia TIRA kanda ya Mashariki.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TIRA, Bi. Innosencia Abdallah, mkazi wa Wilaya ya Kinondoni, amesema amefurahishwa na elimu aliyopata kuhusu majukumu mbalimbali ya TIRA, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko yahusuyo bima pamoja na kufahamu fursa zilizopo katika sekta ya bima k**a uwakala wa bima, udalali wa bima na huduma nyingine zinazohusiana na soko la bima.
Aidha, Meneja wa TIRA Kanda ya Mashariki, Bw. Kurenje Mbura, amesema jukwaa hilo limekuwa sehemu muhimu ya kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu kuhusu usimamizi wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo takribani wananchi wamepatiwa elimu hiyo hadi sasa na pia wadau mbalimbali wameshiriki katika jukwaa hilo wakiwemo NHIF, kampuni ya bima ya Strategies na kampuni ya bima mtawanyo ya Pan Afrique Re.
Kilele cha tamasha hilo ni hapo kesho tarehe 24 Mei 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Albert Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ataongoza ‘jogging’ maalum ya kuhamasisha masuala ya bima na afya. Jukwaa hilo limeandaliwa na FAGDI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.