11/05/2026
VIONGOZI WA WILAYA WAKUTANA NA WAFANYABISHARA SOKO KUU KAKONKO ILI KUWAHIMIZA KUJIPANGA KUPISHA MRADI WA MAJENGO YA GHOROFA.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col. Evance Mallasa kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli , wamefanya kikao na wafanyabiashara wa eneo la soko kuu la Kakonko, lengo kuu ikiwa ni kuwahimiza wafanyabiashara kuanza kupisha mradi wa ujenzi majengo ya ghorofa sehemu ya mbele inayoelekea barabara kuu.
Kikao hicho kimefanyika leo Jumatatu, Mei 11, 2026 katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ambapo viongozi hao walieleza kuwa ujenzi wa soko hilo ni sehemu ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza mapato ya halmashauri pamoja na kuwapatia wafanyabiashara sehemu bora na salama ya kufanyia shughuli zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Col.Mallasa aliwaomba wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kupisha eneo la ujenzi ili kuruhusu mradi huo kuanza kwa wakati, akisisitiza kuwa soko hilo litakuwa la kisasa na litawanufaisha wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla.
Aidha, alieleza kuwa wafanyabiashara watakaopisha maeneo yao watapatiwa kiasi cha shilingi laki tano (500,000) kila mmoja ili kuweza kuhamisha mizigo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli aliwataka wafanyabiashara kuona mradi huo k**a ni fursa ya maendeleo ya wilaya na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unatekelezwa kwa mafanikio.
Mradi huo wa ujenzi wa soko unatarajiwa kubadilisha taswira ya kibiashara katika Wilaya ya Kakonko na kuchochea ukuaji wa uchumi, kwa mapato ndani ya wilaya na kukuza uchumi wa wananchi.
08/05/2026
MKURUGENZI MTENDAJI ASISITIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA MAPATO
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli, amesisitiza usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi ya fedha za umma ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.sha watendaji wa kata, wakuu wa shule pamoja na walimu wakuu kilichofanyika katika ukumbi mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Mkurugenzi Ndaki aliwataka watendaji kusimamia kwa umakini miradi ya ujenzi ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, aliwataka watendaji kuhakikisha wafanyabiashara wana kata leseni halali za biashara ili kuongeza mapato ya halmashauri.
Pia alisisitiza nidhamu katika ukusanyaji na matumizi ya fedha kwa kuwataka watendaji kuepuka kutumia fedha taslimu (fedha mbichi) na badala yake kuhakikisha fedha zote zinawekwa kwenye akaunti husika ili kurahisisha ufuatiliaji na uwazi wa matumizi.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Ndaki pia aliwataka watendaji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo cha Parachichi, akieleza kuwa zao hilo linaweza kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kuchangia kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wao, watendaji wa kata, wakuu wa shule na walimu wakuu wameahidi kutekeleza maelekezo hayo kwa uaminifu na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ubora ili kuimarisha maendeleo ya Wilaya ya Kakonko.
04/05/2026
Kila la kheri kidato cha sita!
03/05/2026
MKURUGENZI NDAKI ANG'ARA USIKU WA WAFANYAKAZI BUHIGWE NA KUTUNUKIWA ZAWADI MAALUM YA PONGEZI
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndaki Stephano Mhuli amealikwa na kuhudhuria usiku wa Wafanyakazi Wilaya ya Buhigwe Jumamosi Mei 02, 2026 na kupata nafasi ya kutoa nasaha ya uzoefu wake katika usimamizi wa miradi ambapo alituzwa zawadi maalum na mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa, Hassan Rugwa.
01/05/2026
NENDENI MKATATUE KERO ZA WANANCHI: RC SIRRO
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka watumishi wa sekta za Umma na binafsi mkoani Kigoma kwenda kutatua kero kwa wananchi badala ya kugeuka kero kutokana na kushindwa kutatua changamoto za wananchi.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipohutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika kimkoa wilayani Uvinza.
Amesema waajiri na waajiriwa wote wana haki ya kutimiza wajibu wao ili kutoathiri maslahi na matokeo ya utendaji kazi kwa pande zote mbili. Aidha amesisitiza wafanyakazi mkoani hapa kuzingatia nidhamu ya muda katika maeneo yao ya utendaji kazi.
Katika kuonesha kuthamini mchango wa wafanyakazi, hafla hiyo imeshuhudia utoaji wa vyeti kwa wafanyakazi hodari waliotambuliwa kwa utendaji wao bora kazini. Hatua hiyo imeelezwa kuwa chachu ya kuongeza morali na kuwahamasisha watumishi wengine kufanya kazi kwa bidii na weledi zaidi.
Awali, risala ya wafanyakazi imesomwa na Mwenyekiti wa Vyama vya Wafanyakazi mkoani Kigoma, ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyakazi wametoa shukrani zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, ikiwemo kupandisha madaraja, kuongeza ajira pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya kazi.
Hata hivyo, katika risala hiyo wafanyakazi wameeleza changamoto wanazokabiliana nazo, hususan suala la baadhi ya waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Wamesema hali hiyo imekuwa ikiathiri haki za wafanyakazi na kuwataka waajiri wote kuzingatia wajibu huo kwa mujibu wa sheria.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo " Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050", yamesisitiza mshik**ano, uwajibikaji na ushirikiano kati ya waajiri na wafanyakazi k**a msingi wa maendeleo endelevu ya Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
01/05/2026
Dr.Simon Mafuru Benjamin, Daktari bingwa wa upasuaji ambaye amefanya upasuaji wa mafanikio zaidi ya 40 ndani ya miezi 6 akipokea cheti na zawadi ya mfanyakazi hodari akiwa mmoja wa wafanyakazi hodari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko waliopokea tuzo ya ufanyakazi hodari Wilayani Uvinza leo Ijumaa Mei mosi, 2026 na kukabidhiwa tuzo hiyo na mgeni rasmi, Balozi Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
01/05/2026
SALAMU ZA PONGEZI!
Menejimenti inapenda kutoa pongezi za dhati kwa Ndugu Ndaki Stephano Mhuli, kwa kuchaguliwa kuwa Mfanyakazi Hodari kwa ukamilishaji wa miradi kwa wakati na kwa ubora, miongoni mwa Wakurugenzi wote wa Mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amemkabidhi Ndugu Ndaki Mhuli, Cheti cha Pongezi pamoja na Tuzo ya Mshindi wa Kwanza katika usimamizi bora wa miradi ya maendeleo wakati wa sherehe za Sikukuu ya wafanyakazi Mei Mosi zilizofanyika Wilaya ya Uvinza kimkoa leo terehe 01 Mei, 2026,
ikiwa ni uthibitisho wa juhudi zake, weledi, uwajibikaji na uongozi madhubuti katika kusimamia rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi.
Mafanikio haya ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo endelevu na huduma bora kwa jamii.
Tunampongeza kwa dhati na kumtakia mafanikio makubwa zaidi katika majukumu yake ya sasa na yajayo.