02/06/2026
Mkoa wa Njombe umezindua rasmi Michezo ya UMITASHUMTA NA UMISSETA 2026 jana katika viwanja vya shule ya sekondari Makambako tayari kwa kushiriki mashindano hayo ngazi ya taifa.
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMMISETA ngazi ya kitaifa yanatarajia kufanyika Mkoani Iringa Juni 6,2026 yakibeba kauli mbiu “Michezo na Sanaa Shuleni ,Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa”
25/05/2026
Mwenge wa Uhuru waridhishwa na uwekezaji wa huduma za afya za kibingwa Makambako.
Na. Lina Sanga
Tamko hilo limetolewa leo na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026,Ndg. Wazo Michael Mwang’onda mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Adags kilichopo Mtaa wa Lyamkena,na kuridhia kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho ambacho kitatoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Ndg. Mwang’onda amesema kuwa, uwekezaji huo uliofanyika na daktari mstaafu umetokana na Amani na utulivu katika taifa na kuwataka wananchi kulinda Amani na utulivu huo ili kuwavutia wawezezaji wengi Zaidi kuja kuwekeza nyumbani.
Waziri wa Kilimo ,Mhe. Daniel Chongolo (MB) amemshukuru Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa makundi maalum kupitia mikopo ya asilimia 10 na agenda ya matumizi ya nishati safi kwani inasaidia kutunza mazingira na afya za wananchi.
Pia, Mhe. Chongolo amepongeza uwekezaji wa maghala kwa ajili ya uuzaji wa pembejeo za kilimo uliofanywa na Ndg. Oraph Mhema, Mfanyabiashara wa pembejeo Makambako kwa kufanya uwekezaji wenye tija kwa wakulipa na kuwasogezea huduma ya mbolea jirani na makazi yao.
Mwenge wa Uhuru 2026 katika Halmashauri ya Mji Makambako umekimbizwa kilomita 108.3 na kupitia miradi 5 yenye thamani ya bilioni 4.86 ambayo ni ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Mlumbe,Mradi wa kituo cha afya cha Adags,Mradi wa ujenzi wa maghala ya pembejeo za kilimo Mhema zuku warehouse,mradi wa vijana wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 na mradi wa maji Mtaa wa Mlowa.
Mwenge wa Uhuru 2026 umezindua mradi 1,umetembelea na kukagua miradi 2 ,kuweka jiwe la msingi miradi 2 ambapo kati ya miradi hiyo miradi 2 ni ya sekta binafsi na miradi 3 ya Serikali.
23/05/2026
Halmashauri ya Mji Makambako yazindua jukwaa la vijana
Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako imezindua jukwaa rasmi la vijana (Vijana platform) ili kuwakutanisha vijana pamoja kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kujenga Taifa.
Akizungumza na vijana kabla ya kuzindua jukwaa hilo,Bi. Elice Simonile, Mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya jamii Mkoa wa Njombe ambaye alikua Mgeni rasmi, amewapongeza vijana kwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa jukwaa hilo na kutoa hoja zenye mashiko zinazowahusu vijana ili zifanyiwe maboresho.
Pia, amewasisitiza vijana kulinda Amani ya nchi na kuhakikisha jukwaa hilo linakua muhimili mkuu wa kudumisha Amani kwani Serikali imeweka jitihada kubwa katika kuwawezesha vijana, hivyo ni wakati wa vijana kuingia ofisi yoyote ya Serikali na binafsi kujifunza masuala mbalimbali ili kuongeza ujuzi na ubunifu sambamba na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kutambua fursa zilizopo.
Ametoa wito kwa vijana kuwa na subira katika kupata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali, kwani kuna sharia na utaratibu wa utoaji wa fedha hizo na zinatolewa kwa foleni hivyo vijana watambue kuwa kuchelewa kupata sio makusudi ya Serikali bali ni suala la mfumo ambao Serikali imeweka ili fedha hizo ziwafikie walengwa.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mhe. Robert Shejamabu amewataka vijana walioshiriki uzinduzi wa jukwaa hilo kujitofautisha na vijana wengine kwa kujitambua na kutambua walipotoka,kwani watoto wa wasaka tonge au mama ntilie ndiyo wanaoibadilisha dunia endapo watatambua wanataka nini na wafanye nini.
Awali,vijana walipata nafasi ya kuwasilisha hoja mbalimbali akiwemo Bw. Kemcho Kidava,Tyson Nziku na Neema Dononda waliiomba Serikali kupunguza bei ya pembejeo za kilimo ili kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo,kutoa mikopo ya asilimia 10 kutolewa kwa wakati ili vijana waweze kutimiza malengo pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uzalendo kwa vijana ili wawe na uelewa kabla ya kufanya maamuzi.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa Greencity sambamba na uzinduzi wa kongamano la vijana kuelekea siku ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mei 25, 2026.