Regional Commissioner's Office-Mara

Call Directions Website Contact the organization

Regional Commissioner's Office-Mara Contact information, map and directions, contact form, opening hours, services, ratings, photos, videos and announcements from Regional Commissioner's Office-Mara, Government Organization, Musoma.

Ukurasa huu wa Facebook ya Mkoa wa Mara ni maalumu katika kuweka matukio mbalimbali yanayofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara katika kutekeleza majukumu yake.

MARA YAJIPANGA MAPOKEZI YA KIDATO CHA KWANZA 2028Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tar...
01/10/2026

MARA YAJIPANGA MAPOKEZI YA KIDATO CHA KWANZA 2028
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 30 Septemba, 2026 ameongoza kikao cha viongozi na watendaji wa Serikali Mkoa wa Mara kujadili maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kuhuisha mipango na mikakati ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuiwasilisha ofisini kwake ifikapo tarehe 15 Oktoba, 2026.
Mhe. Matambi amezitaka Halmashauri kuanza sasa utekelezaji wa mipango na mikakati yao na kuhakikisha inawashirikisha wadau wote kikamilifu ikiwemo wananchi, Wanamara wanaoishi nje ya Mkoa wa Mara na wadau wa maendeleo na kuangalia njia zote ambazo zinaweza kufanikisha upatikanaji wa miundombinu inayohitajika kabla ya kufikia mwaka 2028.
“Taarifa ya utekelezaji wa mikakati hiyo iwasilishwe kila baada ya miezi mitatu kuanzia tarehe 15 oktoba, 2026 katika vikao vya kupeana taarifa hatua zilizofikiwa, changamoto zilizojitokeza na hatua zilizochukuliwa katika ngazi ya Kata, Wilaya na hatimaye Mkoa”amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaka Halmashauri kuweka utaratibu wa kutambua michango yote ya wadau watakaoshiriki katika kufanikisha utekelezaji wa jukumu hii maalum katika maeneo yao na kutahadharisha kuhusu kuingiza siasa katika kutekeleza jukumu hili muhimu.
“Katika kutekeleza jukumu hili, wadau wote washirikishwe, angalizo yasiibuke maneno na hoja za kisiasa na kushutumiana, hili jukumu ni mahususi linalohitaji jitihada za kila Mwanamara kulifanikisha” amesema Mhe. Mtambi.
Brigedia Jenerali Mtambi amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kwa kuona umuhimu wa kufanya kikao cha tathmini ya maandalizi ya kupokea wanafunzi mapema ili kuandaa miundombinu na walimu wanaohitajika ili wanafunzi watakapoanza masomo waweze kupata huduma stahiki.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Ufundi Dkt. Elpidius Baganda ameeleza kuwa katika mwaka 2028 Mkoa wa Mara unategemea kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 155,910 katika shule zote za Halmashauri za Mkoa wa Mara na mahitaji makubwa yanayohitajika ni miundombinu na walimu watakaofundisha wanafunzi hao.
Dkt. Baganda ameeleza kuwa kutokana na idadi hiyo ya wanafunzi, Mkoa wa Mara unao upungufu wa miundombinu mbalimbali na tathmini iliyofanywa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa imebaini kuwepo kwa mahitaji ya jumla ya madarasa 1,556, madawati 97,567 na matundu ya vyoo 4,779 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Dkt. Baganda amesema Mkoa wa Mara umeandaa mkakati wa usimamizi na ufuatiliaji wa maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2028 wenye lengo la kuhakikisha maandalizi ya miundombinu na walimu wanaohitajika yanafanyika mapema ili wanafunzi wote waanze kidato cha kwanza Januari, 2026.
Dkt. Baganda amezitaka Halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu mahitaji ya miundombinu na namna wanavyoweza kusaidia kuboresha miundombinu ya Shule za Sekondari ili kufanikisha mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028.
Kikao hicho kimehudhuliwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Meya, Wenyeviti, Wakurugenzi na watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.

MTAMBI ATAKA UBINIFU KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI MARA Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mt...
01/10/2026

MTAMBI ATAKA UBINIFU KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI MARA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 29 Septemba, 2026 ameongoza jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali lililofanyika katika ukumbi wa uwekezaji na kuyataka mashirika hayo kuwa na ubunifu katika kutafuta rasilimali na kutekeleza miradi yao.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mhe. Mtambi amesema baada ya nchi mbalimbali kupunguza au kuondoa kabisa ufadhili kutokana na nchi hizo kubadilisha sera zao, vita vinavyoendelea vya Ukraine na Urusi na kuyumba kwa uchumi, mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuongeza ubunifu katika utendaji wao.
“Ubunifu utawasaidia kuangalia namna ambavyo mtakavyoweza kutumia teknolojia kurahisisha na kufanya kwa ufanisi baadhi ya mambo, kuanzisha ubia na taasisi nyingine na katika uendeshaji wa shughuli za mashirika yenu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameyataka mashirika hayo kuwa na ubinifu pia katika uibuaji wa miradi inayotekelezwa na kwa namna watakavyowashirikisha wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo na majukumu yao kwa ujumla.
Brigedia Mtambi ameyataka mashirika hayo kutanguliza uzalendo kwa nchi wakati wa kutekeleza majukumu yetu na kuwataka kuwa macho na mataifa yanayopanga mipango ya kuharibu nchi nyingine yanapitia katika Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutoa fedha za kuhamasisha machafuko, kuharibu maadili na tamaduni za nchi ya Tanzania.
“Endapo ustawi na utulivu wa nchi yetu ukateteleka, anayepata hasara kubwa ni sisi wananchi wa Tanzania na wanaoweza kunufaika ni mataifa ya nje. Ipendeni nchi yetu na kutanguliza mbele manufaa ya taifa letu wakati wote”amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali inatambua mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika utekelezaji wa Dira ya 2050 na kuyataka mashirika hayo kupanga mipango yake kuendana na mipango ya Serikali ili kusaidia kutekeleza malengo ya dira hiyo.
Mkuu wa Mkoa ameyataka mashirika yasiyo ya Kiserikali kusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa kutokea kwa El nino na maeneo mbalimbali kutapata mvua za wastani au juu ya wastani kutokana na utabiri kuonyesha kuwa Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa 17 nchini iliyo katika hatari ya kupata mvua kubwa.
Mhe. Mtambi ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuisaidia Serikali ya Mkoa wa Mara katika kuhamasisha na kutekeleza kampeni za kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuhawamasisha wanawake zaidi kuhudhuria kliniki na kufuata ushauri wa wataalamu, kuhamasisha usafi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Brigedia Jenerali Mtambi amezipongeza Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa jitahida zao katika suala la usafi wa mazingira na kuzitaka Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara kuiga mfano huo ili kuwa eneo safi na salama kwa binadamu, mifugo na wanyamapori.
Awali akiongea katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Bibi Neema Ibamba ameeleza kuwa madhumuni ya jukwaa hilo ni kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika Mkoa wa Mara, kujadili manufaa na changamoto za mashirika hayo katika jamii.
Bibi Neema ameeleza kuwa jukwaa hilo ni fursa pia kwa Serikali kuwasilisha maelekezo yake na mashirika hayo kupokea maelekezo ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
Bibi Neema ameeleza kuwa jukwaa hilo ni sehemu ya maandalizi ya Jukwaa la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali na kwa mwaka huu kauli mbiu ya jukwaa hilo ni “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani”.
Jukwaa la Mashirika yasiyo ya kiserikali limehudhuriwa na Msajiri wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mwakilishi wa Baraza la Mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi na watendaji wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali katika Mkoa wa Mara.

RC AWAPONGEZA WATUMISHI WA RS MARA KWA UTENDAJI ULIOTUKUKA Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Bregedia Jenerali Evans Alfred Mtam...
01/10/2026

RC AWAPONGEZA WATUMISHI WA RS MARA KWA UTENDAJI ULIOTUKUKA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Bregedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 29 Septemba, 2026 amewapongeza watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kwa utendaji uliotukuka kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha ustawi na maendeleo ya Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ametoa pongezi hizo wakati akipokea tuzo ya utendaji uliotukuka ya Mkoa wa Mara kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Makundi Maalum iliyokabidhiwa katika kongamano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lililofanyika Arusha tarehe 22-26 Septemba, 2026.
“Mimi ninaahidi kuendelea kuwapa watumishi ushirikiano ili Mkoa wa Mara uwe kinara na mfano bora katika masuala mbalimbali” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Ndugu Kusaya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuweka mazingira rafiki yanayowezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kuboresha utoaji wa huduma za umma.
Ndugu Kusaya ameahidi kuwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara hawatabweteka baada ya kupokea tuzo hiyo bali watafanyakazi yao kwa ufanisi na weledi ili kufanyavizuri zaidi na kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali.

KUSAYA ATAKA MABORESHO HUDUMA ZA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Geral...
01/10/2026

KUSAYA ATAKA MABORESHO HUDUMA ZA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 28 Septemba, 2026 ameongoza kikao cha tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PTJ MMMAM) kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji na kuzitaka Halmashauri kuboresha huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika Halmashauri zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Kusaya amezitaka Halmashauri kutoa kipaumbele kwa shughuli za PTJ MMMAM kwa kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na Wakurugenzi wa Halmashauri kushiriki vikao vya robo mwaka vya mpango huo.
“Wakurugenzi wa Halmashauri wahudhurie vikao vya robo mwaka vya utekelezaji wa programu hiyo katika Halmashauri zao na Mkoa upate taarifa na sababu za Mkurugenzi ambaye hajashiriki kikao ili uweze kuchukua hatua stahiki” amesema Ndugu Kusaya na kuongeza kuwa ametoa agizo hilo kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa programu ya PTJ MMMAM kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, amemuelekeza Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kuangalia uwezekano wa kuingiza bajeti ya shughuli za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika utekelezaji wa bajeti yam waka 2026/2027 ili utekelezaji wa shughuli hizo mbali na kuwa na bajeti ya wadau, upate pia bajeti ya mapato ya ndani.
Ndugu Kusaya amezielekeza Halmashauri kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vituo vya kulelea watoto na makazi ya watoto ili kuhakikisha kuwa watoto wanaoishi katika vituo hivyo wanapata malezi, makuzi na ujifunzaji stahiki kuendana na miongozo ya Serikali.
Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara amezitaka Halmashauri kuboresha utoaji wa chakula shuleni kwa wanafunzi na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kufanyavizuri katika utoaji wa chakula shuleni.
Ndugu Kusaya ameitaka Halmashauri ya Mji wa Bunda kuongeza jitihada katika utoaji wa chakula shuleni ikiwa ni pamoja na kuifanyia kazi michango iliyotolewa katika kikao hicho kwa ajili ya kuboresha utoaji wa chakula shuleni ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri.
Aidha, Ndugu Kusaya amezitaka Halmashauri kuboresha matumizi ya mfumo wa GoTHOMIS katika uagizaji wa dawa na vifaa tiba na kuipongeza Manispaa ya Musoma kwa kufunga mfumo huo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kuutumia katika kutoa huduma kwa wananchi.
Ndugu Kusaya amezitaka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama zilizoko kwenye mpango wa kujengewa nyumba salama kwa ajili ya kuwahifadhi watoto wanaokimbia ukeketaji katika maeneo yao kufuatilia upatikanaji wa maeneo ya kujenga nyumba hizo haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe ambao ndio watakelezaji wa PJT MMMAM katika Mkoa wa Mara, Katibu wa Dayosisi hiyo Mchungaji Philipo Kanwelle amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kuelekeza maboresho katika huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Mchungaji Kanwelle amesema ni muhimu kwa Serikali kuwa na bajeti ya utekelezjai wa shughuli za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika ngazi mbalimbali ikiwemo vijiji, kata na Halmashauri kutokana na umuhimu wa suala la malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika kujenga kizazi bora cha Tanzania ya baadae.
Aidha, Mchungaji Kanwelle ameeleza kuwa ni muhimu kuongeza ushirikiano na taasisi na wadau mbalimbali, kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto, usajiri wa vituo vya kulelea watoto mchana na kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya takwimu zinazohusiana na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu amezitaka Halmashauri amezitaka Halmashauri kuwahamasisha wananchi kuanzisha kuanzisha vituo vya kulelea watoto wakati wa mchana na hususan katika maeneo ya masoko na sehemu za shughuli za kiuchumi.
“Wananchi wakihamasishwa vizuri kuhusu umuhimu wa vituo hivyo, wanaweza kuwekeza katika kufungua na kuviendesha vituo hivyo katika maeneo ya masoko na shughuli za kiuchumi kwa kutumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri” amesema Dkt. Masatu.
Aidha, Dkt. Masatu amezitaka Halmashauri kutumia Siku ya Lishe na Afya ya Kijiji au Mtaa (SALIKI) katika kutoa elimu za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na kuhamasisha jamii na hususan wanaume kushiriki katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Aidha, Ndugu Masatu amezitaka Halmashauri zenye masoko makubwa k**a Halmashauri ya Mji wa Tarime na Manispaa ya Musoma kwenda kujifunza katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza au Manispaa ya Njombe kuhusiana na uanzishwaji wa vituo vya kulelea watoto wakati wa mchana.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Sehemu, Vitengo na wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Sekta ya Afya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Wakurugenzi na watendaji wa Halmashauri, wadau wa utekelezaji wa mpango wa PTJ MMMAM.

Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) limefanya mabadiliko ya tarehe za mitihani na upimaji wa kitaifa kwa mwaka 2026 kwa ...
01/10/2026

Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) limefanya mabadiliko ya tarehe za mitihani na upimaji wa kitaifa kwa mwaka 2026 kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba tarehe 02 Oktoba, 2026 anatarajiwa kuanz...
01/10/2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba tarehe 02 Oktoba, 2026 anatarajiwa kuanza ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Mara.

Tarehe 02 Oktoba, 2026 Mhe. Nchemba anatarajiwa kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kukagua Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na baadae kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo ya Nyamswa na Kibara.

Tarehe 03 Oktoba, 2026 Mhe. Waziri Mkuu atafanya kikao na watumishi wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma.

MARA YAFANYA KIKAO KAZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA PTJ MMMAM Kikao kazi cha wataalamu wanaohusika na utekelezaji ...
21/09/2026

MARA YAFANYA KIKAO KAZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA PTJ MMMAM
Kikao kazi cha wataalamu wanaohusika na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM) kimefanyika leo tarehe 21 Septemba, 2026 katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta mbalimbali kuhusiana na mikakati ya utekelezaji wa programu hiyo kwa ufanisi zaidi.
Dkt. Masatu amesema kuwa kikao hicho kimekuja baada ya kubaini pengo la uelewa kati ya wataalamu wa ngazi ya Mkoa na wataalamu wa Halmashauri kuhusiana na masuala mbalimbali katika utekelezaji wa programu hiyo kwenye sekta mbalimbali.
“Tumekutana leo hapa ili kupata uelewa wa pamoja kuhusiana na utekelezaji wa programu hii katika sekta maeneo yetu ili kupata uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa programu hii kwa ufanisi” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu amewaambia wataalamu hao kuwa kutokana na elimu watakayopewa kuhusiana na utekelezaji wa Programu hiyo itawasaidia washiriki kutambua mambo muhimu katika maeneo yao na kuwajengea uwezo ambao utatumika katika ngazi mbalimbali kuanzia kwenye familia, jamii na Taifa kwa ujumla ili nchi iweze kupata maendeleo.
Dkt. Masatu amesema Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii ni waratibu tu wa kusimamia utekelezaji wa programu hiyo, lakini ili kupata matokeo na manufaa zaidi ya mradi huo ni muhimu sekta zote zikashiriki katika kutekeleza mpago huo.
Amesema wataalamu wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji ni muhimu wauelewe mpango huo vizuri ili kuhakikisha chakula kinalimwa cha kutosha ili kusaidia wananchi kupata lishe na kukuza uchumi wao kwa kuuza ziada ya chakula kitakacholimwa.
Dkt. Masatu amewataka wataalamu wa kilimo kuwafundisha na kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Mara kulima zao la viazi damu ili kuongeza mapato yao kutokana na bei ya zao hilo kuwa kubwa na kuimarisha lishe na afya za wananchi kwani viazi hivyo vinasaidia kuongeza virutubisho na damu mwilini.
Mapendekezo ni kuhamasisha kilimo cha viazi damu (betruits) katika Mkoa wa Mara ili kupunguza changamoti ya upungufu wa damu kwa wananchi. Kuimarisha uratibu wa mpango huo katika ngazi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu hiyo Ndugu Charles Mashauri kutoka Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) Jimbo la Musoma na Ukerewe amesema kuwa Sekretarieti za Mikoa ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa mradi huu kati ya Serikali Kuu na watekelezaji wa mradi huu (Halmashauri) ili kuhakikisha sekta zote zinahusishwa katika utekelezaji wa mradi huo ili kupata matokeo yanayotarajiwa.
Ndugu Masahuri amewataka wataalamu kuimarisha ushirikiano baina ya wataalamu wa mradi huo na wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha malezi na makuzi ya watoto yanaimarishwa katika Nyanja zote ili kuweza kupata Taifa lenye watu wanaokusudiwa.
Kikao kazi hicho kimewahusisha wataalamu mbalimbali wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kutoka sekta za uzalishaji mali, mipango, Maendeleo ya Jamii, Habari na Elimu na Kamati ya Mkoa ya Usimamizi wa Sekta ya Afya (RHMT) pamoja na Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara.

MTAMBI AIPONGEZA UHAMIAJI KUANZISHA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA SENAPA Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Al...
21/09/2026

MTAMBI AIPONGEZA UHAMIAJI KUANZISHA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA SENAPA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 21 Septemba, 2026 amempokea Kamanda wa Uhamiaji wa Mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Thomas Kandy Fussy aliyefika ofisini kwake kujitambulisha baada ya kuhamia Mkoa wa Mara akitokea Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Mtambi ameipongeza Uhamiaji Mkoa wa Mara kwa kuanzisha vituo vya kutolea huduma ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) ili kurahisisha huduma za uhamiaji kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo jambo ambalo amesema linasaidia katika kukuza uchumi wa nchi.
“Katika kipindi cha msimu wa watalii wengi, huduma za uhamiaji zinatolewa katika vituo vya Kogatende na Seronela ili kuwarahisishia watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kupata huduma kwa urahisi, jambo ambalo linasaidia kukuza uchumi na kuiweka Tanzania katika ushindani wa soko la watalii” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amesema kwa sasa Mkoa wa Mara unapokea wawekezaji wengi wa kigeni hususan katika sekta za madini na kilimo na kuitaka Uhamiaji kuendelea kuimarisha huduma za uhamiaji ili kuwahudumia wawekezaji, watalii na wasafiri wengine wanaoingia na kutoka nchini Tanzania.
Mhe. Mtambi ameitaka Uhamiaji Mkoa wa Mara kuendelea kutoa elimu ya uhamiaji na uzalendo kwa wananchi na hususan katika Wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti kuhusu kuvuka mipaka ya nchi kwa kufuata taratibu za uhamiaji wanapoingia katika nchi jirani za Kenya na Uganda.
Brigedia Jenerali Mtambi amemhakikishia SACI Fussy ushirikiano kutoka kwa viongozi na wananchi wa Mkoa katika utekelezaji wa majukumu yake kwa muda wote atakapokuwa katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Kamanda Fussy amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kuahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mara katika kutoa huduma bora za uhamiaji kwa wananchi, watalii na wawekezaji.

KUSAYA AONGOZA MAPOKEZI YA ATCL MUSOMA Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 17 Septemba...
17/09/2026

KUSAYA AONGOZA MAPOKEZI YA ATCL MUSOMA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 17 Septemba, 2026 ameongoza mapokezi ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliyoanza safari zake za kawaida baada ya kusimama kwa muda mrefu kupisha upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Ndugu Kusaya ameipongeza ATCL kwa kutekeleza ahadi yake kwa kuanzisha safari za ndege kati ya Musoma na maeneo mengine kupitia Uwanja wa Ndege Musoma jambo ambalo amesema litaimarisha huduma za usafiri, kukuza uchumi kwa kuimarisha biashara na kurahisisha safari za watalii wanaoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Mapokezi haya yanaashiria kuanza tena kwa safari za ndege za abiria kutoka maeneo mbalimbali kuja katika Mji wetu wa Musoma. Niwaombe wananchi kutumia usafiri wa anga na fursa mbalimbali zinazotokana na usafiri wa anga kuboresha maisha na kujiimarisha kiuchumi” amesema Ndugu Kusaya.
Ndugu Kusaya ameitaka ATCL kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya safari mara baada ya idadi ya abiria na mizigo itakapokuwa ya kuridhisha ili kurahisisha huduma za usafiri katika Mkoa wa Mara na kuwataka wananchi kutumia usafiri wa anga kwa ajili ya kuboresha shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Meneja wa Uwanja wa Ndege Musoma Ndugu Frank Msofe ameeleza kuwa uwanja wa Ndege Musoma kwa sasa upo tayari kutoa huduma kwa usalama wa ndege za abiria baada ya upanuzi na ukarabati mkubwa uliofanyika na kuwahakikishia wananchi kuwa uwanja huo unakidhi vigezo vya kiusalama vinavyohitajika katika sekta ya anga.
Uwanja wa Ndege Musoma umepanuliwa na kukarabatiwa kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 35 kuanzia mwaka 2018 hadi 2026 ambapo upanuzi na ukarabati katika njia ya kutua na kuruka ndege na maegesho ya ndege yamekamilika na kuwezesha safari za ndege ya abiria kurejea baada ya kusimama kwa muda mrefu kupisha ukarabati huo.

RC AIPONGEZA JKT KWA KUTOA MAFUNZO YA UZALENDO KIDIGITALI KWA VIJANA Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans A...
17/09/2026

RC AIPONGEZA JKT KWA KUTOA MAFUNZO YA UZALENDO KIDIGITALI KWA VIJANA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Brigedia Jenerali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 17 Septemba, 2026 amefunga mafunzo ya vijana katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 822 Rwamkoma JKT na kulipongeza JKT kwa kuanzisha mafunzo ya uzalendo kidigitali kwa vijana.
Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo yaliyowahusisha vijana wa kujitolea na vijana kwa mujibu wa sheria, Mhe. Mtambi amewataka vijana waliopata mafunzo ya uzalendo kidigitali kuwa mabalozi wazuri katika utumiaji wa mitandao ya kijamii katika jamii.
“Ninatamani mafunzo haya yafundishwe pia katika shule za Sekondari na vyuo ili kupata vijana wengi zaidi wenye uzalendo katika matumizi ya mitandao ya kijamii hapa nchini” amesema Mhe. Mtambi na kuongeza kuwa mitandao ya kijamii ni mizuri sana ikitumika vizuri inauwezo wa kuwafundisha mambo mazuri ambayo yatasaidia katika kuwaletea maendeleo.
Mhe. Mtambi amesema mitandao ya kijamii ina mambo mazuri na mabaya na vijana wasipofundishwa uzalendo wanaweza kuitumia mitandao vibaya bila kujali madhara ya matumizi mabaya ya mitandao na kusistiza umuhimu wa vijana kufundishwa kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
Mhe. Mtambi amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa uratibu mzuri wa mafunzo ya jeshi la vijana na kupongeza maono yao ya kuwa na jeshi linalofanya shughuli zake kwa kuzingatia sayansi na teknolojia.
Mhe. Mtambi amesema Serikali inaendelea kujipanga kuhakikisha kuwa vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanajiunga na jeshi kabla ya kuendelea na mafunzo mengine ili kuwajengea vijana nidhamu na uzalendo na kuongeza kuwa kwa wale ambao hawakuchaguliwa kujiunga katika mafunzo hayo wamekosa mambo mazuri.
Mkuu wa Mkoa amelipongeza JKT kwa kuanzisha ufugaji wa samaki kwenye vizimba hapa nchini na kuitaka kuanzisha mashamba darasa ya kilimo, ufugaji nakadhalika ili wananchi waweze kwenda kujifunza ili kuboresha shughuli zao za uzalishaji mali.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania Brigedia Jenerali Gerald Juma Omar amesema mafunzo haya ni muhimu kwa ajili ya kuwaandaa vijana kwenda kujifunza fani mbalimbali baada ya kuhitimu.
Brigedia Jenerali Omar amewataka vijana waliohitimu mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri kwa kuyaishi mambo mazuri waliyojifunza na kutekeleza kwa vitendo viapo vyao walivyoapa katika hafla hiyo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwaleta vijana kwa ajili ya mafunzo ambayo amesema yanabadilisha mitazamo yao katika maisha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Shija Sahani Rupi amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoanzisha jeshi hilo na amewataka vijana hao kutekeleza mafunzo na viapo vyao kwa vitendo.
“Ninatamani mkirudi katika jamii ninyi mliyopata mafunzo muwe tofauti na wenzenu ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kwa uzalendo, nidhamu na ubunifu wa kujikwamua kiuchumi” amesema Brigedia Jenerali Rupi.
Akitoa taarifa Kaimu Mkuu wa Kambi hiyo Kanali Mkinga Kinana ameeleza kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa mafunzo ya awali ya kijeshi kwa ajili ya kuwajengea nidhamu na uzalendo vijana waliojiunga na mafunzo hayo.
Kanali Kinana amesema mafunzo hayo yameanza 27 Februari, 2026 kwa wahitimu wa kujitolea na tarehe 12 Juni, 2026 kwa waliosoma kwa mujibu wa sheria na yamehitimishwa leo kwa pamoja.
Kwa upande wao, wahitimu wa mafunzo hayo katika risala yao wameeleza kuwa wamejifunza mambo membi ikiwemo mafunzo ya kijeshi, ujasiriamali na utunzaji wa akiba na kuomba muda wa mafunzo uongezwe na kuwa mwaka mmoja.
Jumla ya vijana 2139 walianza mafunzo ya kujitolea na kwa mujibu wa sheria katika kikosi 822 JKT Rwamkoma na kati yao vijana 18 hawakufanikiwa kumaliza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro wakati 2,121 wakihitimu mafunzo hayo katika kikosi cha 822 JKT Rwamkoma kilichopo Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara.

Address

Musoma

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Regional Commissioner's Office-Mara posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to Regional Commissioner's Office-Mara:

Shortcuts

Share