16/09/2026
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mha. Leonard Msenyele, amewataka watumishi wa Mamlaka kuongeza uwajibikaji, juhudi na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu ya majisafi na usafi wa mazingira.
Mkurugenzi Msenyele ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Kanda ya Nyegezi na Kanda ya Kati, katika ziara ya kikazi yenye lengo la kutambulisha Menejimenti mpya ya MWAUWASA pamoja na kukumbushana kuhusu umuhimu wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Amesema watumishi wanafanya kazi kubwa katika kuhakikisha huduma inawafikia wananchi, hivyo kinachohitajika zaidi ni kuongeza bidii na kujituma katika majukumu yao.
“Naamini mnafanya kazi kinachohitajika ni kujituma kwa bidii, Wateja wanapokosa maji wanatuangalia sisi k**a mnakuwa na changamoto ya kuwafikishia maji, ni bora kusema mapema ili tuweze kuchukua hatua na kuboresha huduma,” amesema Mha. Msenyele.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesisitiza umuhimu wa kulinda na kutokwamisha nguzo kuu nne za Mamlaka ambazo ni uzalishaji, usambazaji, mauzo na makusanyo, akieleza kuwa nguzo hizo ni muhimu katika kuhakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amesema yuko tayari kufanya kazi kwa nguvu zote na watumishi katika kuendeleza Mamlaka, huku akiwaomba watumishi hao kumpa ushirikiano na kutomwangusha katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Ndugu Edward Range, amewakumbusha watumishi kuzingatia mambo mawili muhimu katika utendaji wao ambayo ni jitihada na uaminifu katika kazi, akieleza kuwa misingi hiyo ndiyo mtaji muhimu wa Taasisi katika kufikia malengo yake.
Watumishi wa Kanda ya Nyegezi na Kanda ya Kati wameipongeza Menejimenti mpya ya MWAUWASA kwa kukubali kupokea kijiti cha kuiongoza Mamlaka na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yao, hususani katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya majisafi na usafi wa mazingira.