03/08/2026
MADIWANI KUWENI WABUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIJANA, MSIISUBIRI SERIKALI – MASALU
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mwanza, Ndugu Seth MASALU , amewataka madiwani wa kata zote 191 za Mkoa wa Mwanza kuwa wabunifu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan vijana na wanawake, badala ya kusubiri Serikali pekee ichukue hatua.
Ndugu Masalu ametoa wito huo alipokuwa Mgeni Rasmi katika semina ya Fursa ya Mafunzo ya Ujasiriamali iliyoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali Eve Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Diwani wa Kata ya Lwanhima, Jijini Mwanza.
Katika hotuba yake, alisema maendeleo ya jamii yanahitaji ushirikiano kati ya viongozi, taasisi zisizo za kiserikali, sekta binafsi na wananchi wenyewe. Alisisitiza kuwa madiwani wana nafasi kubwa ya kuanzisha na kuhamasisha miradi na programu za kuwawezesha wananchi kiuchumi katika maeneo yao.
Aidha, aliwahimiza madiwani kushirikiana kwa karibu na taasisi k**a EVE Foundation Tanzania ili kuendelea kuleta fursa za mafunzo, uwezeshaji na mikopo nafuu kwa vijana na wanawake, hatua ambayo itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kukuza ujasiriamali na kuinua uchumi wa jamii.
Semina hiyo iliwakutanisha wananchi na wajasiriamali wa Kata ya Lwanhima, ambapo walipata elimu ya ujasiriamali na kutambulishwa fursa ya mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na EVE Foundation Tanzania kwa lengo la kukuza biashara na kujenga uchumi imara.
Kulinda na Kujenga Ujamaa