Wizara ya Katiba na Sheria

Website

Wizara ya Katiba na Sheria The United Republic of Tanzania
Ministry of Constitutional and Legal Affairs

11/11/2026

TANZANIA YATAJA MAFANIKIO YA UTOAJI HAKI: MRUNDIKANO WA KESI WAPUNGUA, TEHAMA YATOA NEEMA.

Upatikanaji wa haki kwa wananchi unaendelea kupewa kipaumbele nchini Tanzania kupitia uimarishwaji wa miundombinu na utendaji kazi wa mhimili wa Mahakama, maboresho yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwabili wananchi wanapofuatilia haki zao.

Hayo yameelezwa jijini Geneva na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Abdallah Ulega, kwenye Mkutano wa 4 wa Tathmini ya Hali ya Haki za Binadamu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, ambapo amebainisha kuwa maboresho hayo yamepunguza mrundikano wa mashauri kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 5, huku wastani wa muda wa kumaliza kesi ukipungua kutoka siku 95 hadi kufikia siku 66 kwa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar, Mhe. Waziri amesema mrundikano wa mashauri umeshuka kutoka asilimia 43 hadi kufikia asilimia 18 na kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na matumizi ya teknolojia, ambapo zaidi ya mashauri 170,000 yamehitimishwa kupitia mfumo wa mahakama za kimtandao na kidijitali, hatua inayoongeza ufanisi na kasi ya utoaji haki.

11/11/2026

Mahakama zinazotembea, tafsiri ya sheria kwa Kiswahili, usikilizwaji wa mashauri kwa mtandao na huduma za msaada wa kisheria vimefanikiwa kusogeza haki karibu na wananchi kwa kuondoa vikwazo vya lugha, umbali na gharama.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), wakati akiwasilisha hotuba yake katika Mkutano wa 4 wa Tathmini ya Hali ya Haki za Binadamu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jijini Geneva.

Katika mkutano huo, Mhe. Ulega amesisitiza kuwa Tanzania inatambua mamlaka ya mahakama zake, huku akiwataka wadau wa ndani na nje kuheshimu uhuru wa Mahakama na kutoingilia maamuzi yake.

TANZANIA YAWASILISHA TAARIFA ZA MAENDELEO YA JAMII NA HAKI ZA BINADAMU UNGAJamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha ...
11/11/2026

TANZANIA YAWASILISHA TAARIFA ZA MAENDELEO YA JAMII NA HAKI ZA BINADAMU UNGA

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha taarifa mbalimbali kuhusu maendeleo ya jamii na hatua za kulinda haki za binadamu katika vikao vya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), vinavyofanyika Jijini New York, Marekani, kuanzia tarehe 1 Oktoba hadi 20 Novemba, 2026.

Taarifa zilizowasilishwa zimejikita katika masuala ya maendeleo ya wanawake, haki za mtoto, ulinzi wa haki za binadamu, haki za wakulima wadogo, watu wa asili, watu wenye ualbino na haki ya maendeleo.

Katika taarifa hizo, Tanzania imeeleza jitihada za kupanua huduma za elimu na afya, kuwawezesha wananchi kiuchumi, kulinda watoto, kupambana na ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino pamoja na kuimarisha usimamizi wa ardhi kwa kuzingatia sheria za nchi.

Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa maendeleo jumuishi na utekelezaji wa haki za binadamu katika ngazi ya jamii.

10/11/2026

Usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala umeelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kuleta amani na kuchochea maendeleo kwenye jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bw. Richard Kayombo, alipokuwa akiahirisha zoezi la siku kumi la utoaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria mkoani humo, huku akiisisitiza sekretarieti ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili kuendelea kulifanyia kazi suala hilo.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Bi. Grace Tete, amesema kuwa pamoja na makundi mengine yaliyonufaika na huduma hizo, wanawake wamejitokeza kwa wingi zaidi ikilinganishwa na makundi mengine.

Akitoa taarifa za utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mkoani Pwani, Mratibu wa kampeni hiyo ambaye pia ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Innocent Magesa, amesema kuwa zaidi ya wananchi 400,000 wamefikiwa na kunufaika moja kwa moja na huduma hizo.

06/11/2026

MKUU WA GEREZA LA WILAYA YA MAFIA APONGEZA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA AWAMU YA PILI

Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Mafia, S.S.P Castory Vicent Suline, amepongeza utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili kwa kuwafikia wafungwa na mahabusu na kuwapatia huduma za msaada wa kisheria, hatua inayowawezesha kufahamu haki zao na kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria.

Amesema kufikishwa kwa huduma hizo magerezani ni muhimu katika kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata fursa ya kusikilizwa na kupata msaada wa kisheria, huku akipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kusogeza huduma hizo hadi katika maeneo ya magereza.

Key Quotations from the Speech Delivered by the Minister for Constitutional and Legal Affairs, Hon. Abdallah Hamis Ulega...
06/11/2026

Key Quotations from the Speech Delivered by the Minister for Constitutional and Legal Affairs, Hon. Abdallah Hamis Ulega at the 4th Universal Periodic Review (UPR) session at the UN Human Rights Council in Geneva on November 5, 2026.

Nukuu Muhimu za Hotuba Iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, katika Mkutano wa 4 w...
06/11/2026

Nukuu Muhimu za Hotuba Iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, katika Mkutano wa 4 wa Tathmini ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Novemba 5, 2026."

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), tarehe  Novemba 5, 2026, anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tan...
04/11/2026

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), tarehe Novemba 5, 2026, anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Haki za Binadamu katika Duru ya Nne ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, Uswisi.

Waziri Ulega ataambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe, Mbunge wa Jimbo la Siha, Mhe. Saashisha Mafuwe pamoja na viongozi na wataalamu wengine kutoka Tanzania.

Ushiriki huo ni sehemu ya dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ulinzi, hifadhi na utekelezaji wa haki za binadamu kwa vitendo.

04/11/2026

TANZANIA KUENDELEA KUDHIHIRISHA DHAMIRA YA KUIMARISHA NA KULINDA HAKİ ZA BINADAMU KWA VITENDO KATIKA UMOJA WA MATAIFA

Tarehe 5 Novemba, 2026, Tanzania itawasilisha taarifa ya mafanikio ya Ulinzi wa Haki za Binadamu mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, Uswisi.

Taarifa hii inawasilishwa katika Duru ya Nne ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR).

Akizungumza jijini Geneva, siku moja kabla, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), amesema mapitio hayo ni fursa muhimu kwa Tanzania kueleza mafanikio yaliyopatikana, na kuwasilisha utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mapitio yaliyopita, pamoja na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha haki za binadamu.

Chini ya uongozi Thabiti na kupitia falsafa ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs), Tanzania imepiga hatua kubwa katika masuala ya Haki za binadamu.

Taarifa itakayowasilishwa ni ya Nne ambayo inaainisha - mafanikio na hatua zilizotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2026, zikiwemo katika maeneo ya utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, afya, elimu, upatikanaji wa maji na miundombinu. Hatua hizo zinaonesha juhudi za Serikali katika kuimarisha haki, usawa wa fursa na maendeleo jumuishi.

Maandalizi ya taarifa hiyo yalihusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mahakama, asasi za kiraia, taasisi za kidini, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine wa haki za binadamu.

Ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo pia unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa lenye ustawi, haki, ujumuishi na uwezo wa kujitegemea, huku utu wa binadamu, usawa wa fursa na maendeleo ya wananchi vikiendelea kuwa msingi wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

UPR ni utaratibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaozipa nchi zote wanachama fursa ya kupitia hali ya haki za binadamu katika nchi zao kwa misingi ya usawa, kuwasilisha hatua zilizochukuliwa na kupokea mapendekezo kutoka mataifa mengine kwa lengo la kuimarisha zaidi utekelezaji wa haki hizo.

04/11/2026

SERIKALI YAAHIDI KUPELEKA MAHAKAMA ZA MWANZO MAENEO YA MILIMANI SAME

Bungeni, Dodoma.

Serikali imesema itaweka kipaumbele ujenzi wa mahakama za mwanzo katika maeneo ya milimani wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ili kuwapunguzia wananchi, hususan wanawake wenye watoto, usumbufu wa kufuata huduma za haki maeneo ya tambarare.

Ahadi hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Zuena Athumani Bushiri, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga mahakama katika tarafa za milimani wilayani humo.

Mhe. Katimba amesema Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama, na kwamba katika bajeti ya mwaka 2025/2026 imejenga jengo la kisasa la Mahakama ya Mwanzo Gonja wilayani Same. Amebainisha ujenzi katika tarafa nyingine utaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.

Katika swali la nyongeza, Mhe. Bushiri amesema asilimia 75 ya wakazi wa Same wanaishi maeneo ya milimani, lakini tangu enzi za mkoloni hakuna mahakama ya mwanzo iliyojengwa huko. Aliuliza pia mpango wa haraka wa kukarabati mahakama chakavu zilizojengwa wakati wa ukoloni.

Mhe. Katimba alisema maeneo yenye changamoto za kijiografia, ikiwemo ya milimani, ni miongoni mwa vigezo vya kipaumbele katika kuchagua maeneo ya kujenga mahakama hizo.

“Mahakama kwa kadri itakavyokuwa inapata fedha, itaweka kipaumbele cha kujenga mahakama katika maeneo haya ya milimani,” amesema Mhe. Katimba.

Kuhusu uchakavu, amebainisha kuwa baadhi ya mahakama zilijengwa miaka mingi iliyopita na zinahitaji ukarabati. Amesema Mahakama imetekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati kwa takribani miaka mitano, na kwamba itaendelea kutafuta fedha ili kukarabati pia mahakama zilizochakaa, ikiwemo za Same.

Address

Government City, Mtumba
Dodoma
41207

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Wizara ya Katiba na Sheria posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share